Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla amewahakikishia Wafanyabiashara na wawekezaji kuwa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuweka mazingira Bora ya biashara pamoja na kutatua changamoto za Wafanyabiashara.
RC Makalla amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Biashara Mkoani humo lenye lengo la kusikiliza changamoto za Wafanyabiashara na kuweka mikakati ya endelevu ya utatuzi wa changamoto za kibiasha zitakazowasilishwa.
Katika kikao hicho RC Makalla amewashukuru Wafanyabiashara na wawekezaji kwa kuvunja rekodi ya makusanyo makubwa ya Kodi Halali ambapo zaidi ya shilingi trilioni 10 zilikusanywa na TRA kwenye Mkoa huo.
Aidha RC Makalla amewahakikishia Ulinzi na usalama Wafanyabiashara ikiwa ni pamoja na kukomesha matukio yote ya uhalifu ikiwemo vibaka, panya road na majambazi.
Pamoja na hayo RC Makalla amesema Serikali ya Mkoa huo ipo hatua za mwisho kukamilisha ujenzi wa one stop center ya Biashara itakayokwenda kumaliza tatizo la urasimu.
Kuhusu suala la Kariakoo kufanya biashara saa 24, RC Makalla amesema Serikali ipo hatua za mwisho kukamilisha mchakato huo.