Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu HESLB Tanzania imetangaza awamu ya tatu (Batch III) ya wanafunzi 2,518 waliopangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 6.9 bilioni kwa mwaka wa masomo 2023/2024. Wanafunzi hawa 2,518 ni wapya wa mwaka wa kwanza wanaojiunga na taasisi mbalimbali za elimu ya juu zilizopo nchini kwa ajili ya masomo ya shahada za kwanza (Local Undergraduate Degrees).
Kufuatia kutangazwa kwa Awamu ya Tatu, jumla ya wanafunzi wapya wa shahada za kwanza waliopangiwa mikopo imefikia 73,078 na thamani ya mikopo yao ni TZS 210.8 bilioni. Itakumbukwa kuwa, wanafunzi 56,132 wa Shahada ya Kwanza walipangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 159.7 bilioni katika Awamu ya Kwanza (Batch I) iliyotangazwa Ijumaa, Oktoba 20, 2023. Aidha, Awamu ya Pili (Batch II) yenye wanafunzi 14,428 waliopangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 44.2 bilioni ilitangazwa Ijumaa, Oktoba 27, 2023.
Baada ya kutangazwa kwa Awamu ya Tatu, hivi sasa HESLB inakamilisha maandalizi ya kufungua dirisha la rufaa ambalo litakuwa wazi kuanzia Jumatano, Novemba 8, 2023 ili kuwapa fursa waombaji mkopo kuwasilisha maombi ya kuongezewa au kupangiwa mkopo, kwa wanafunzi ambao hawajapangiwa katika Awamu Tatu zilizotangazwa. Serikali imetenga TZS 731 bilioni kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza kwa mwaka 2023/2024 kwa ajili ya wanafunzi 220,376. Kati yao, wanafunzi 75,000 wanatarajiwa kuwa ni wanufaika wa mwaka wa kwanza baada ya kukamilishwa kwa uchambuzi wa maombi ya rufaa yatakayowasilishwa.
Aidha, HESLB inapenda kuwafahamisha wanafunzi wa ngazi ya stashahada walioomba mikopo ya elimu kuwa uchambuzi wa maombi yao unakamilishwa na orodha ya waliopangiwa mikopo kwa mwaka 2023/2024 itatangazwa Alhamisi, Novemba 9, 2023.