Ni wiki moja sasa imekatika tangu Klabu ya Everton kuweka historia ya kuwa klabu ya kwanza ya Ligi Kuu England kucheza mechi kwenye ardhi ya Tanzania na Afrika Mshariki kwa ujumla ambapo walicheza na dhidi ya Gor Mahia katika Uwanja wa Taifa DSM.
Pamoja na mchezo huo ambao Everton walishinda mabao 2-1 Wachezaji wa Everton walipata nafasi ya kutembelea sehemu mbalimbali ikiwemo Shule ya wanafunzi wenye mahitaji maalum ya Uhuru Machanganyiko, Albino United, Hospitali ya Pugu na sehemu nyingine kadha wa kadha wakiwa na ujumbe wa ‘Together Inspired’ ama ‘Kwa pamoja tumehamasika’.
Kuonesha uhalisia wa ujumbe huo wa Everton ni pale baadhi ya wachezaji wa Everton walipotembelea Uwanja wa Uhuru Jumatano July 12 na kukutana na timu ya watu wenye ulemavu wa ngozi ya Albino United ambao walikuwa sehemu ya ujio huo wa Everton.
Wachezaji watatu wa Everton, Michael Keane, Mohamed Besic na Tom Davies walifika Uwanja wa Uhuru na kuwakuta Albino United wakifanya mazoezi chini ya kocha wao Alex Kashasha ambapo licha ya kufanya nao mazoezi, waliongoza pia zoezi la kugawa zawadi kwa wachezaji wa Albino United ambazo ni shin guards, mipira, jezi, Kamba za kuruka, pampu za kujazia mipira pamoja na vifaa vingine vya kimichezo.
Wachezaji Michael Keane na Tom Davies walipata nafasi ya kuongea na waandishi wa habari waliokuwepo uwanjani siku hiyo na kueleza hisia zao baada ya kukutana na timu hiyo ambapo Tom Davies ambaye ni nahodha wa timu ya Taifa la England chini ya miaka 19 akisema ni mara yake ya kwanza kukutana na timu ya mpira wa miguu iliyoundwa na watu wenye ulemavu ili kufikisha ujumbe kwa jamii.
>>>“Hii ni mara yangu ya kwanza kuona timu kama hii lakini nimeona umoja kati yao na inaleta picha nzuri ukiwa hapa. Wote ni marafiki na nina Imani kocha ataweza kuwasaidia sana, kwakweli nina furaha sana kuwepo hapa.”
Mbali ya kuwa ni mara yake ya kwanza pia alisema mpira wa miguu ni mchezo unaoleta watu pamoja na kuwashauri Albino United kuendelea kufurahia kucheza pamoja.
“Ni vizuri kuwa hapa kuona timu inavyocheza na kufurahia wanachokifanya na hiyo ndio maana halisi ya soka na michezo kwa ujumla ya kuwaleta watu pamoja. Ninachopenda kuwaambia ni kuwa waendelee kufurahia kwani ndio kitu kizuri kufanya na nina Imani kuwa kocha atawasaidia.” – Michael Keane.
Beki wa kati wa Everton, Michael Keane alieleza hisia zake baada ya kuja kukutana na wachezaji hao.
“Ni ngumu sana kwao na nimekuwa nikisikia kuwa wanapitia hali ngumu sana. Kwa hiyo, kwa wao kuja pamoja na kufurahia ni jambo zuri sana. Ni vigumu kuona timu kama ya Albino United kwa Uingereza kwani huwa wanachukuliwa kama watu wasiokuwa na mchango kwenye jamii. Hivyo kuona watu wanapata shida sio jambo rahisi hata kidogo.” – Michael Keane
Keane alimalizia kwa kusema wana kila sababu ya kuendelea kufurahia kile wanachokifanya na wacheze kwa bidii “Ningependa kuwaambia kuwa waendelee kufurahia katika kile wanachokifanya na nina furaha kuwa hapa kuwaona walivyo na umoja ni jambo zuri.” – Michael Keane
Ni jambo zuri kuona wachezaji wa Everton wakija na kutoa mchango wao kwa watu wenye uhitaji maalumu na kueleza uzoefu wao katika hilo kama ambavyo wamesema kwenye kauli mbiu Together Inspired. Bila shaka wameweza kutoa hamasa kubwa sana kwa wachezaji wa timu ya Albino United ambayo imeamua kutumia mpira wa miguu kama sehemu ya kufikisha ujumbe wao kwa jamii.
VIDEO: Gor Mahia vs Everton: Full Time 1-2 (ALL GOALS JULY 13, 2017)