Machafuko makali katika gereza la wanawake nchini Honduras siku ya Jumanne yamesababisha takriban wanawake 41 kuuawa katika mlipuko wa ghasia ambazo rais wa nchi hiyo alilaumu magenge ya mitaani ya “mara” ambayo mara nyingi yana nguvu kubwa ndani ya magereza.
Wahasiriwa wengi walichomwa moto lakini pia kulikuwa na ripoti za wafungwa waliopigwa risasi au kudungwa visu kwenye gereza la Tamara, yapata kilomita 50 (maili 30) kaskazini magharibi mwa mji mkuu Tegucigalpa, alisema Yuri Mora, msemaji wa wakala wa uchunguzi wa polisi wa Honduras.
Takriban wafungwa saba wa kike walikuwa wakitibiwa katika hospitali ya Tegucigalpa kwa majeraha ya risasi na visu, wafanyikazi walisema.
“Timu za uchunguzi zinazoondoa miili zinathibitisha kuwa zimehesabu 41,” Mora alisema.
Vyombo vya habari vya eneo hilo vilimhoji mfungwa mmoja aliyejeruhiwa nje ya hospitali ambaye alisema wafungwa wa genge linalohofiwa la Barrio 18 walivamia sell na kuwapiga risasi wafungwa wengine au kuwachoma moto.
Rais wa Honduras Xiomara Castro alisema ghasia hizo “zilipangwa na maras kwa ujuzi na kukubali mamlaka ya usalama”.
Makumi ya ndugu na jamaa waliokuwa na wasiwasi na hasira walikusanyika nje ya gereza ili kujaribu kujua hatima ya wapendwa wao.