Mahakama ya Hakimu Mkazi Kiteto Mkoani Manyara imemuhukumu kifungo cha miaka 30 Jela, Yerenia Chidaka, Mkazi wa Kijiji cha Dongo Wilayani Kiteto, baada ya kufanya ngono na kumtia mimba Mtoto wake wa miaka 16.
Mtuhumiwa amekiri kosa hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mosi Sasy, na kusema hataki kuisumbua Mahakama na kusema aliamua kumpa mimba Mtoto wake huyo ili asiolewe na Mwanaume wa Kabila la Wakamba.
Imeelezwa kuwa Baba huyo alipomuuliza Mke wake juu ya suala la kutotaka Mtoto wao aolewe na Wakamba, Mkewe alimjibu kwa dhihaka kwamba kama hataki aolewe basi amuoe yeye na ndipo alipoamua kumpa ujauzito.
Alipotakiwa kujitetea, Mtuhumiwa aliiomba Mahakama impunguzie adhabu kwakuwa shetani alimpitia kutenda kosa hilo, huku Mwendesha Mashtaka wa Polisi Mahakamani hapo Inspekta Wilfred Mollel, akisema Jeshi la Polisi halina taarifa kama Mtuhumiwa aliwahi kufanya kosa zaidi ya hilo na kumwomba Hakimu kumpa adhabu inayostahiki.