Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mwenyekiti wake Rais DK JAKAYA KIKWETE ilikutana Dodoma May 5 2014 ili kujadili na kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwemo mchakato wa Bunge la Katiba ambalo limesitishwa mpaka mwezi wa nane.
Akitoa mapendekezo ya Kamati Kuu, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Nape Nnauye amesema licha ya kutoa mapendekezo yatakayofanikisha upatikanaji wa katiba mpya, chama hicho kimepinga vitendo vya baadhi ya wabunge kupinga waziwazi kwenye majukwaa juu ya kuendelea kwa bunge Maalum.
Namkariri akisema ‘kamati kuu pia inasikitishwa na juhudi za makusudi za baadhi ya watu au vikundi vya watu kuamua kuendeleza upotoshaji kuhusu mchakato mzima wa mabadiliko ya katiba, wameamua kupotosha kwa kwenda barabarani, kufanya mikutano au kuzungumza na Waandishi wa habari kupotosha baadhi ya mambo’
Kwenye sentensi nyingine Nape amesema chama chake hakipo tayari kuwabembeleza wajumbe waliosusia kuhudhuria vikao kwa kusisitiza ‘hatuna mpango wa kuzungumza nao na tunampango wa kushughulika nao mtaani wanakokwenda, sio sisi na wala hatuna mpango wa kuishawishi Serikali wala viongozi wa kitaifa kuwabembeleza kuwarudisha bungeni, mimi nadhani waendelee kukaa barabarani’