Benki ya Stanbic Tanzania imetilia mkazo ahadi yake ya kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha elimu kwa kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi katika shule za serikali.
Benki hiyo ilitoa ahadi hiyo wakati wa hafla fupi iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Kimara ya kukabidhi madawati 50 yenye thamani ya TZS 4,500,000 milioni, ambayo walikabidhi kwa taasisi hiyo ya elimu.
Msaada huo ni sehemu ya kampeni inayoendelea ya benki hiyo ilitwayo Stanbic Madawati Initiative, inayolenga kupunguza uhaba wa madawati mashuleni kwa kuchangia madawati nchi nzima na kupanda mti mmoja kwa kila dawati linalotolewa ili kuhakikisha uwiano katika mfumo wa ikolojia wa mazingira.
Madawati hayo yalikabidhiwa na Mkuu wa kitengo cha Wateja Binafsi wa benki ya Stanbic, Bw. Omari Mtiga kwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe.Heri James katika hafla iliyofanyika shuleni hapo mwishoni mwa wiki.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Mtiga alisema, ”tunatambua juhudi zinazofanywa na serikali katika kuboresha sekta ya elimu, na tumejipanga kuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi hizo kwani tunaamini kuwa elimu bora ni muhimu katika kujenga jamii yenye watu wenye uelewa mpana, ambao ni chachu ya maendeleo ya sekta mbalimbali za uchumi wa taifa.”
Aliongeza kuwa dhumuni la benki hiyo kuendelea kujitolea kusaidia sekta ya elimu ni kusukama gurudumu la maendeleo ya nchi kwa kuunga mkono ndoto za jamii ndani ya maeneo inayofanyia kazi.”Kupata nafasi ya kuchangia maendeleo ya elimu nchini Tanzania ni heshima kwetu kwani tunawawezesha wanafunzi kutimiza ndoto zao na kuchochea kufikia dira ya taifa ya kuleta maendeleo kwa kila mtanzania,” alisema Omari Mtiga.
Akizungumza katika hafla hiyo Mhe. James alisema kuwa mchango wa Benki ya Stanbic ni kielelezo kuwa juhudi za serikali kuweka mazingira rafiki kwa taasisi za fedha na taasisi nyingine kufanya biashara zinazaa matunda, hivyo kuziwezesha taasisi hizo kuwekeza katika jamii.
Mhe. James alisema pamoja na juhudi zake zote, serikali haiwezi kuendeleza sekta zote kwa wakati mmoja kwa asilimia 100 kwa sababu fedha za taifa zinagawanywa kwa sekta zote kulingana na mahitaji. Aliwataka wadau kuunga mkono juhudi za serikali ili kukidhi mahitaji ya wananchi
“Serikali yetu imewekeza katika ujenzi wa madarasa, hata hivyo, kuna uhaba wa madawati, hivyo mchango wa Stanbic wa madawati haya leo unaunga mkono juhudi za serikali za kuboresha mazingira ya elimu katika shule hii, kuwezesha watoto kufikia ndoto zao.” Aliongeza.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi wa serikali za mitaa, wanafunzi wa shule hiyo na wafanyakazi kutoka Benki ya Stanbic.