Mwanamke mmoja huko nchini Kongo anayeshukiwa kuwa mteka nyara alikamatwa siku ya Alhamisi na anazuiliwa huko Bukavu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambapo msichana aliyemteka alipatikana akiwa amekufa na kukatwa viungo vyake, maafisa wa eneo hilo walisema.
Mwanamke huyo mwenye umri wa takriban miaka 30, “Ombeni Malekera, ambaye si tukio lake la kwanza la uhalifu huo inasemekana amewahi kuwateka nyara watoto wawili (mtoto wa miaka mitatu na dada yake wa miaka mitano) kutoka kwenye familia moja tangu Jumanne, Agosti 1”, Patience Bengehya. , meya wa wilaya ya Bagira huko Bukavu, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini, aliiambia AFP.
“Mwili wa msichana huyo wa miaka mitano ulipatikana Jumatano kwenye ukingo wa mto, ukiwa umekatwa jinsia yake na ulimi wake,” alisema.
Kupatikana kwa mwili huo kulizua taharuki miongoni mwa wakazi.
Misako ambayo imeanzishwa imewezesha kumpata mvulana huyo wa miaka mitatu ambaye “alikuwa ameleweshwa” nyumbani kwa Ombeni Malekera, alisema meya wa Bagira, mtaa maarufu.
“Watu wenye hasira walitaka kulipiza kisasi lakini maafisa wa kutekeleza sheria waliingilia kati, na mwanamke huyo alipelekwa katika ofisi ya mwendesha mashtaka wa Bukavu na kesi yake itaanza hivi karibuni”, alisema Bw Bengehya.
Mume wa anayedaiwa kuwa mtekaji nyara pia alikamatwa na anazuiliwa katika sero ya kituo cha polisi “kwa sababu za uchunguzi”, alisema.