Serikali ya Kenya na upinzani hivi leo wanatarajiwa kuanza mazungumzo yanayolenga kutafuta muafaka baada ya maandamano ya vurugu kupinga uchaguzi uliopita pamoja na kupanda kwa gharama ya maisha.
Mazungumzo haya yanayoenda kuratibiwa na rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, yanatarajiwa kutoa suluhu ya mvutano unaoendelea kati ya kinara wa upinzani Raila Odinga na Serikali, ambapo kila upande ulichagua timu ya watu watano.
Muungano wa upinzani Azimio uliongoza maandamano mwezi Machi na Julai dhidi ya utawala wa rais William Ruto kupinga kile walichosema ni kupanda kwa gharama ya maisha na kutaka mageuzi katika tume ya uchaguzi kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki.
Maandamano hayo yalionekana kuzidi baada ya serikali kutangaza kuongezwa kwa ushuru katika baadhi ya bidhaa kwa kile rais Ruto alisema hatua hiyo inalenga kuimarisha maendeleo nchini mwake.
Makundi ya kutetea haki za binadamu nchini humo yanasema karibia watu 30 walifariki katika maandamano hayo wakati upinzani ukisema rekodi zake zilionyesha watu 50 waliuawa.
Timu ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga inataka kujadili gharama ya maisha na mageuzi ya uchaguzi baada ya kushindwa katika uchaguzi mwaka jana, lakini serikali inasisitiza kuwa tayari inafanya kazi kurekebisha mfumuko wa bei na kupunguza gharama ya bidhaa za kimsingi.
Upinzani ulisimamisha maandamano mwezi Aprili na Mei ili kuruhusu mchakato sawa wa mazungumzo ya pande mbili, lakini maandamano yalianza tena baada ya mazungumzo kuvunjika.