Viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) Alhamisi wameagiza kikosi chake ‘kuwa tayari kurejesha utulivu wa kikatiba’ nchini Niger, kulingana na maazimio yaliyosomwa mwishoni mwa mkutano wa kilele huko Abuja.
Jumuiya hiyo ya kikanda imeagiza “kutumwa kwa kikosi cha ECOWAS kurejesha utulivu wa kikatiba nchini Niger”, Rais wa Tume ya ECOWAS Omar Touray amesema baada ya mkutano huo usio kuwa wa kawaida.
Haikuwezekana mara moja kubainisha maana ya kupelekwa kikosi hiki kwa Niger.
Rais wa Nigeria Bola Tinubu, mkuu wa ECOWAS, amesema kabla ya kusomwa kwa maazimio hayo, anatumai “kufikia azimio la amani”, na kuongeza: “hatua zote ni muhimu”.
“Hakuna chaguo ambalo limetengwa, ikiwa ni pamoja na matumizi ya nguvu kama njia ya mwisho. Ikiwa hatutafanya hivyo, hakuna mtu mwingine atakayefanya hivyo kwa ajili yetu,” ameongeza.
Rais wa Côte d’Ivoire, Alassane Ouattara, amewaambia waandishi wa habari kabla ya kuondoka kwenye mkutano huo “kwamba ECOWAS iliingilia kati siku za nyuma huko Liberia, Sierra Leone, Gambia na Guinea-Bissau” wakati utaratibu wa katiba ulikuwa hatarini.
“Leo, Niger inakabiliwa na hali kama hiyo na ninataka kusema kwamba ECOWAS haiwezi kuikubali,” ameongeza.