Mvutano kati ya watawala wa kijeshi na jumuiya ya ECOWAS waongezeka baada ya taasisi hiyo kuamua jeshi lake la dharura lipelekwe Niger kurudisha utawala wa kikatiba
Mivutano inaongezeka kati ya watawala wapya wa kijeshi wa Niger na jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Magharibi mwa Afrika ECOWAS baada ya jumuiya hiyo kupitisha uwamuzi jana usiku wa kutuma jeshi lake la dharura kurudisha utawala wa kidemokrasia Niger.
Usiku wa kuamkia leo Ijumaa, Jumuiya ya ECOWAS ilitangaza msimamo wake kwamba imeshatowa maagizo ya kupelekwa kile ilichokiita kikosi cha dharura kurudisha utawala wa kikatiba nchini Niger baada ya muda wa hadi Jumapili iliyopita,iliyoutowa wa kurudishwa madarakani rais Bazoum kupita bila ya hatua hiyo kuchukuliwa.Tangazo hilo lilitolewa katika mkutano wa kilele mjini Abuja na rais wa tume ya ECOWAS Omar Touray.
“Mamlaka ya ECOWAS inatowa maagizo kwa kamati ya wakuu wa majeshi kukiweka tayari kikosi cha dharura cha ECOWAS kwa ukamilifu wake mara moja. Viongozi wameweka wazi kwamba wamechukua uamuzi huu kufanya wajibu wao na kwa mujibu wa mipango na azma yao. Haina maana kwamba wanakinyongo dhidi ya nchi yoyote au mtu yoyote.Huu ni msimamo wa kikanda”
Jumuiya hiyo imeendelea pia kulaani hatua ya kushikiliwa kwa rais Mohammed Bazoum,familia yake na maafisa wa serikali yake.
Saa kadhaa kabla ya uamuzi huu wa ECOWAS maafisa wawili kutoka nchi za Magharibi waliliambia shirika la habari la Associated Press kwamba jeshi la Niger lilimwambia mwanadiplomasia wa ngazi za Juu wa Marekani kwamba watamuua rais Bazoum ikiwa nchi jirani zitajaribu kuingilia kijeshi kuurudisha utawala wake.