Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani ametoa mwito wa kushughuliwa hali ya wahamiaji barani Ulaya.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani amesema hayo na kubainisha kwamba, vifo vya wahamiaji katika Bahari ya Mediterania ni kidonda kilicho wazi na kwamba, kidonda hiki kinapaswa kushughuliwa kwa bandeji na dawa na viongozi wa kisiasa wa Ulaya.
Akionyesha kusikitishwa na vifo vya mara kwa mara vya wahamiaji katika maji ya Bahari ya Mediterania, Papa Francis amesema inasikitisha kwamba, tangu kuanza mwaka huu karibu watu 2000 wakiwemo wanawake na watoto wamekufa maji wakiwa njiani kuelekea Ulaya.
Katika ibada ya kila wiki ya Angelus, kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 86 aliwaombea watu 41 walioripotiwa kupotea Jumatano na wenzao wanne walionusurika na kupelekwa kwenye kisiwa cha Italy cha Lamepdusa.
Msemaji wa shirika la UN linaloshughulikia wakimbizi, IOM mwishoni mwa wiki alisema kwamba takriban watu 2,060 wamekufa kwenye bahari ya Meditarrenean tangu mwanzo wa mwaka, wakati 1,800 miongoni mwao wakipotea
Wahamiaji wengi wanatokea nchi za Afrika za chini ya Jangwa la Sahara na wengi wao huwa wanakufa maji kutokana na kutumia vyombo dhaifu sana kama mitumbwi ya plasitiki kuvuka mikondo mikali ya bahari kubwa ya Mediterania.
Ripoti zinaonyesha kuwa, wahamiaji 400 walifariki dunia katika kipindi cha miezi mitatu ya awali ya mwaka huu katika bahari ya Mediterania.