Zaidi ya watoto elfu moja nchini Uingereza wamefanyiwa upasuaji kutokana na kushambuliwa na mbwa wanaowekwa nyumbani katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Shirika la habari la Irib limenukuu ripoti rasmi iliyotolewa na vyombo husika nchini Uingereza kuwa karibu asilimia 40 ya watoto waliofanyiwa upasuaji nchini kutokana na kushambuliwa na mbwa mwaka uliopita walikuwa chini ya miaka minne.
Kwa mujibu wa takwimu za 2022 za Taasisi ya Kitaifa ya Afya na Tiba nchini Uingereza, kila siku watu elfu 3 na 473 wakiwemo watoto wenye umri tofauti hufanyiwa upasuaji katika hospitali mbalimbali za nchi hiyo kutokana na kushambuliwa na mbwa, idadi ambayo ni kubwa zaidi kuwahi kuripotiwa katika miaka 16 iliyopita.
Katika kisa cha hivi karibuni zaidi, msichana mwenye umri wa miaka 11 anayeitwa Anna Pawn alishambuliwa na mbwa wa kufugwa nyumbani huko Birmingham, ambapo yeye na waokoaji wake wawili walijeruhiwa vibaya na kukimbizwa hospitalini.
Mbwa aliyemshambulia msichana huyo ni aina ya Bulldog wa Marekani.
Kila mwezi ripoti mbalimbali hutolewa kuhusiana na mbwa wanaofugwa nyumbani kushambaliwa watu ambapo baadhi yao kupoteza maisha. Kuongeza mashambulizi hayo hasa dhidi ya watoto kumepelekea jambo hilo kuwa tishio kubwa katika jamii ya nchi hiyo kwa kadiri kwamba baadhi ya familia zimetaka kupigwa marufuku nchini humo ufugaji wa mbwa walio na uwezo wa kushamblia binadamu.