Afisi ya kuratibu hali ya kibinadamu ya umoja wa mataifa imesema zaidi ya watoto milioni 2.4, waliokimbia makwao kutokana na utovu wa usalama wanahitaji kupata elimu ya haraka .
Katika kambi ya Kanyaruchinya ambapo raia walioondoka vijijini mwao kwa kuhofia mapigano kati ya waasi wilayani Rutshuru na nyiragongo , idhaa ya Ufaransa imezungumza na familia ya Denise shubahiro ambaye amethibitisha hali wanayoipitia kuwapata watoto wao elimu .
“Shida tunayo ni kuwalinda na kuwaelimisha watoto, nina watoto watatu ambao hawasomi ,ningependa watoto hao wasome maana hata kwangu na kwa wengine wangekuwa msaada kwao , hawana sare za shule, vitabu na vitu vingine vinavyohitajika.” alieleza Denise Shubahiro.
Takwimu mpya zilizotolewa na UNICEF zinaonyesha kuwa kati ya Januari 2022 na Machi 2023, shule zisizopungua elfu mbili Mia moja, katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri zimelazimika kusitisha huduma zake kwa sababu ya kuzorota kwa hali ya usalama.
Ukosefu wa usalama umekuwa umeripotiwa pia kuwaathiri karibia watoto laki mbili, waliokimbia makazi yao hivi karibuni ambao kwa sasa wanaishi katika kambi kubwa karibu na Goma.
Ghasia za makundi yenye silaha zimelazimisha maelfu ya familia kutoroka makwao kutafuta usalama katika sehemu zengine hali ambayo imewazuia watoto wao kuhudhuria shule.