Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imesema kuwa wakati ikiadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake bado inakabiliwa na upungufu wa wataalamu wenye ujuzi katika sekta ya usafiri wa anga.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam leo na Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo hapa nchini.
Amesema sekta hiyo ya usafiri wa anga inakuwa kwa kasi lakini ongezeko la wataalamu ni ndogo na haliendani na kasi hiyo hivyo mamlaka hiyo imeendelea kujipanga ili kuhakikisha wanaongeza idadi ya wataalamu.
Aidha katika kusherekea miaka 20 wamepata mafanikio makubwa katika uthibiti wa usalama katika sekta ya usafiri wa anga, mwaka 2003 walikuwa na marubani 234, lakini kwa sasa wapo 603.
Tangu kuanzishwa kwa TCAA wamefanikiwa kuimarika kwa uwezo wa udhibiti katika maeneo ya usalama wa anga pamoja na usimamizi wa wataalam wa usafiri wa anga ambapo katika kaguzi zilizofanywa na Shirika la Usafiri Duniani ufaulu wa Tanzania umekuwa ukiongezeka.
Pia, amesema kwa kipindi kile kulikuwa na ndege 101 kwa sasa kuna ndege 206, kwa kipindi hicho idadi ya abiria kwa mwaka walikuwa milioni 1,521 hadi wanafunga mwaka 2022 abiria walikuwa milioni 5,723 ambalo ni ongezeko kubwa.
Johari amesema wanaendelea kunyambulika kwa sababu Serikali imewekeza sana kwenye sekta ya anga, mwaka 2003 waongozaji wa ndege (marubani wa chini) wanaotumia minara ya kuongoza ndege walikuwa 70 na kwa sasa wapo 154.
Pia, amesema mafanikio mengine ni kwa upande wa wahandisi wa mitambo ya kuongoza ndege umeongezeka mara mbili kutoka 20 ha 44, wataalam wa taarifa za anga wapo 83 kutoka 50, kwa ujumla idadi ya wataalam hao ni 281.
“Aidha Serikali inaendelea na ujenzi wa uwanja mpya wa ndege wa Msalato jijini Dodoma ambao ukikamilika utaongeza idadi ya viwanja vya kimataifa, uboreshaji huu wa miundombinu sio tu kwamba umeimarisha mawasiliano ndani ya Tanzania lakini pia umeiweka nchi kama kitovu cha usafiri wa anga kikanda,” amesema Hamza