Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina S. Mndeme amewataka akina mama kuachana na mikopo isiyokuwa na tija kwao maarufu KAUSHA DAMU, badala yake yake waende kukopa Benki huku akiwasisitiza kujiunga vikundi ili waweze kudhaminika kwa urahisi zaidi.
Mhe. Mndeme ameyasema haya wakati akijibu ombi lililotolewa na mmoja wa akina mama wa jumuiya ya wanawake wa kiislam mkoa wa shinyanga anayeishi wilaya ya Kishapu aliyeomba msaada ili kuweza kuwadhibiti watu hao wasiokuwa wanaojihusisha na ukopeshaji katika wilaya hiyo ambao huwadharirisha na kuwachukulia vitu vyao vyote mara inapotokea wameshondwa kulipa.
“Niwatake sasa akina mama wenzangu kuachana kabisa na mikopo hii isiyokuwa na afya wala tija kwa maisha yetu, badala yake twendeni tukakope Benki, na kwamba tumekuwa tukihamasishana sana kujiunga vikundi ambavyo inakuwa ni rahisi sana kuaminika na kukopeshwa bila kudharirisha na mikopo hii kausha damu,” alisema Mhe. Mndeme.
Mikopo isiyokuwa na staha wala utu maarufu kama kausha damu inatajwa kuwa na hatima mbaya zaidi kwa wakopaji, ambapo huishia kwa mkopaji kudharirishwa utu wake, kuchukuliwa mali zake kutokana na uwepo wa riba kubwa inayotozwa na wafanyabiashara hao wa mikopo jambo ambalo Mhe. Mndeme pamoja na kumuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kishapu kulifuatilia lakini pia amewashauri kutumia zaidi mikopo itolwwayo na Serikali kupitia Halmashauri zao punde itakapoanza tena kutolewa.
Katika hafla hii, Mhe. Mndeme aliwaeleza wanajumuiya juu ya upokeaji wa fedha zaidi ya trilioni moja kutoka serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kutekeleza miradi mbalimbali sanjali na kuboresha utoaji wa huduma katika mkoa wa shinyanga.
Kwa upande wao wanajumuiya walitoa salamu za pongezi na shukurani kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anawatumikia watanzania wote na kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea maendeleo, huku wakimuahidi kumpatia ushirikiano wakati wote sanjali na kumuombea heri na fanaka katika kazi zake.
Mhe. Mndeme aliandaa hafla fupi ya chakula cha jioni kwa akina mama wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislam Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kufahamiana, kuzungumza mambo mbalimbali ikiwemo na kupokea kero pamoja na kuzitatua ili jumuiya iweze kufanyq shughuli zake vema.