Idadi ya watu waliouawa na mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza inaendelea kuongezeka, huku wizara ya afya ya Palestina katika Ukingo wa Magharibi ikisema kuwa idadi ya waliofariki imepita 8,000, kutokana na data kutoka wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas. IDF imesasisha idadi ya mateka waliokuwa wametekwa na Hamas huko Gaza hadi 239.
Maafisa wa UNICEF waliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa mkutano wa dharura kwamba “zaidi ya watoto 420 wanauawa au kujeruhiwa huko Gaza kila siku.
” Kamishna Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini ameliambia baraza hilo karibu asilimia 70 ya walioripotiwa kuuawa huko Gaza ni watoto na wanawake.
“Save the Children iliripoti jana kwamba karibu watoto 3,200 waliuawa huko Gaza katika muda wa wiki tatu tu. Hii inazidi idadi ya watoto wanaouawa kila mwaka katika maeneo yenye mizozo duniani tangu 2019,” Lazzarini alisema.
IDF ilisema Jumatatu inapanua uvamizi wake wa ardhini ndani ya Gaza, wakati nchi hiyo inaingia katika awamu ya pili ya vita vyake dhidi ya Hamas.
Israel imeahidi kuendeleza “mashambulio yake makubwa, makubwa” katika kuwasaka wanamgambo wa Hamas waliohusika na mauaji ya Oktoba 7.