Mshambuliaji nyota wa kandanda Neymar atafanyiwa upasuaji hii leo nchini kwao Brazil baada ya kupatab jeraha kwenye goti lake la kushoto wakati wa mechi ya timu ya taifa mwezi uliopita, Shirikisho la Soka la Brazil (CBF) lilisema Jumatano.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31, ambaye alijiunga na klabu ya Al Hilal ya Saudi Arabia kutoka Paris Saint-Germain mwezi Agosti, atafanyiwa upasuaji katika hospitali ya Mater Dei iliyoko kusini mashariki mwa mji wa Belo Horizonte na daktari wa timu ya taifa Rodrigo Lasmar, CBF ilisema katika taarifa yake. .
Awali Lasmar alimfanyia upasuaji Neymar kwa kuvunjika mguu mwaka wa 2018.
Neymar alitolewa nje kwa machozi wakati Brazil ilipofungwa 2-0 na Uruguay katika mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia Oktoba 17, baada ya kugongana na kiungo mpinzani Nicolas de la Cruz.
Jeraha hilo linatarajiwa kumweka nje ya uwanja kwa miezi kadhaa, ikiwa ni pamoja na mechi zijazo za Brazil za kufuzu Kombe la Dunia 2026 mwezi huu dhidi ya Colombia na wapinzani wao Argentina.
Ni majeruhi ya hivi punde zaidi kwa Neymar, ambaye alifanyiwa upasuaji mwezi Machi kwa tatizo la kifundo cha mguu lililomweka nje kwa miezi sita.
Matatizo ya utimamu wa mwili yalifunika sehemu kubwa ya misimu yake sita akiwa PSG, ambayo ilimsajili kwa rekodi ya dunia ya $234 milioni (euro milioni 222) mwaka 2017.
Alisajiliwa na Al Hilal kwa kitita cha dola milioni 95 mwezi Agosti.