Wananchi wa Morocco kwa mara nyingine tena wamefanya maandamano ya kuwanga mkono wananchi wa Palestina ambao wanakabiliwa na hujuma na mashambulizi ya kikatili ya utawala haramu wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, maandamano hayo yalifanyika usiku wa kuamkia leo katika mji wa Tangier, kaskazini magharibi mwa Morocco.
Waandamanaji hao waliokuwa wamebeba bendera za Palestina, walisikika wakikipiga nara za kuwaunga mkono wananchi wa Palestina, sanjari na kulaani jinai zinazoendelea kufanywa na Wazayuni dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza.
Mmoja wa waandamanaji hao mjini Tangier amenukuliwa akisema: Ni wajibu wetu kuwaunga mkono watu wanaoteseka wa Palestina na tutashikamana na ahadi yetu hii hadi mwisho.
Wananchi wa Morocco wameshaandamana na kumiminika mabarabarani mara kadhaa sambamba na kuzichoma moto bendera za utawala haramu wa Kizayuni, kuonyesha upinzani wao dhidi ya hatua ya serikali ya Rabat ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Tel Aviv na kutaka uhusiano huo ukomeshwe.
Desemba 2020, Morocco na utawala haramu wa Israel zilifikia mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida kwa ushawishi wa Marekani. Na kama sehemu ya makubaliano hayo, Rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump alikubali kutambua mamlaka ya Morocco juu ya Sahara Magharibi.