Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa mafunzo ya siku tatu kwa waandishi wa habari juu ya mfumo mpya wa uandaaji na utekelezaji wa sera mpya ya fedha utakaosaidia kuongeza ufanisi wa sera ya fedha katika kudhibiti mfumuko wa bei na kuimarisha shughuli za kiuchumi.
“Hii ni kwa sababu mfumo huu utawezesha Benki Kuu ya Tanzania kurekebisha riba kulingana na hali ya uchumi na kuhakikisha kwamba kuna usawa kati ya mahitaji na usambazaji wa fedha,” amesema Naibu Gavana wa BoT (Sera za Uchumi na Fedha), Dkt. Yamungu Kayandabila, wakati anafungua semina hiyo inayofanyika katika Ofisi za Makao Makuu Ndogo ya BoT Zanzibar kuanzia Februari 14 hadi 16, 2024.
Amesema mfumo huo pia utasaidia kuzuia kupanda kwa bei za bidhaa na huduma, ambazo zinaweza kupunguza nguvu ya ununuzi wa wananchi na kudhoofisha ukuaji wa uchumi.
Pamoja na mafunzo kuhusu sera ya fedha, washiriki wa semina hiyo kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, watajifunza kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha, ikiwemo masuala ya mikopo; namna Benki Kuu inavyomlinda mtumiaji wa huduma za fedha; na faida za kutumia mifumo mbadala ya malipo badala ya pesa taslimu.
Akizungumzia kuhusu huduma ndogo za fedha, Dkt. Kayandabila amesema Serikali kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipitisha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha mwaka 2018 ili kurasimisha shughuli hizo.
Ameeleza kuwa siku za karibuni kumekuwepo na malalamiko kwa watu kuwa riba ziko juu hadi kufikia hatua ya baadhi kupewa majina ya mikopo mbalimbali kama kausha damu.
“Kumbukeni mikopo hii inasaidia sana watu, kuipa majina kama hayo inakuwa siyo jambo zuri kwani mikopo hii inasaidia watu kutatua mahitaji yao muhimu, ikiwemo kusomesha watoto”, amesema Dkt. Kayandabila.
Ameeleza kuwa kwa sasa BoT ina kurugenzi inayoshughulikia malalamiko ya walaji wa huduma za kifedha na kwamba watu wakipeleka malalamiko yao huko yanashughulikiwa ipasavyo.
Kuhusu matumizi ya njia mbadala za malipo badala ya pesa taslimu, Naibu Gavana amesema: “Watu wanakwenda kwenye taasisi za fedha wanatoa fedha nyingi wanaweka kwenye begi kitu ambacho siyo salama, hivyo lazima tuanze kutumia mifumo ya kuhamisha fedha ili kuepukana na changomoto za kuibiwa”, amesema Dkt. Kayandabila.