Idadi ya waliofariki kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi katika kisiwa cha Sumatra nchini Indonesia imeongezeka hadi 21, huku makumi ya maelfu ya watu wakikimbilia kwenye makazi ya muda ya serikali, maafisa walisema Jumapili.
Mto ulipasua kingo zake na kupenyeza vijiji vya milimani katika wilaya ya Pesisir Selatan ya Sumatra Magharibi mwishoni mwa Ijumaa, Doni Yusrizal, msemaji wa Shirika la Kitaifa la Kukabiliana na Majanga, aliwaambia waandishi wa habari.
Kwa mujibu wa Yusrizal, maiti saba ziliopolewa katika kijiji cha Koto XI Tarusan, huku nyingine tatu zilipatikana katika vijiji viwili vya jirani, na kufanya idadi ya vifo kufikia 21.
Hata hivyo, watu saba bado hawajapatikana.
“Juhudi za kutoa misaada kwa waliofariki na waliopotea zilitatizwa na kukatika kwa umeme, kuziba barabara zilizofunikwa na matope mazito na vifusi,” Yusrizal alisema.
Shirika hilo limesema takriban wanakijiji wawili walijeruhiwa, huku zaidi ya watu 80,000 wakikimbilia kwenye makazi ya muda ya serikali.