Wananchi wanaoishi mwambao wa bahari ya hindi katika kata ya mnyanjani jijini Tanga wameiomba serikali kuweka sheria kali dhidi ya wale wote ambao wamekuwa wakikata miti aina ya mikoko nyakati za usiku.
Hayo yamebainishwa wakati wa shughuli ya upandaji miti aina ya mikoko 250 pamoja na usafi wa fukwe iliyofanywa na wafanyakazi wa Hifadhi ya Bahari ya Silcant Tanga kwa kushirikiana na kamati ya mazingira eneo la sahare ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Bahari duniani.
“kwakweli changamoto zipo nyingi sana tunapanda mikoko lakini bado kuna watu wanakata mikoko nyakati za usiku bado kuna hitajika elimu kwa wananchi waweze kufahamu umuhimu wa utunzaji wa mazingira Pamoja na raselemali za taifa na tunaiomba serikali wahusika watakao kamatwa na mikoko wapewe adhabu kali hata ya kupanda mikoko 1000 pamoja na faini itasaidia kukomesha vitendo hivi’’
Aidha Oriki Msami ambaye ni Afisa maendeleo ya jamii kutoka hifadhi ya Bahari ya Silcant Tanga amesema kuwa dhumuni la kukusanyika na kufanya usafi pamoja na kupanda mikoko kwenye eneo la bandari ya sahare ni katika kuadhimisha siku ya bahari na hivyo kufanya zoezi hilo ni kutokana na changamoto ya uhifadhi wa rasimali bahari ambapo ni pamoja na ukataji wa mikoko nyakati za usiku na hivyo ushirikishwaji na utoaji elimu kwa jamii unahitajika ili kuweza kukabiliana na vitendo hivyo.
“Jamii ielewe kwamba bahari ina fursa nyingi sana kwa jamii na taifa kwani rasilimali nyingi za bahari zikitunzwa vizuri zitawezesha jamii kuweza kujiingizia kipato kwa shuhuli mbalimbali kama za uvuvi pamoja na utalii wa fukwe kwani zita wavutia watalii wengi zaidi kuweza kuja kutembelea eneo hilo.”