Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya kumbukizi ya Rais wa Serikali ya Awamu ya tatu nchini, Hayati Benjamini Mkapa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu, Benjamin Mkapa Foundation (BMF)Dkt. Ellen Mkondya-Senkoro amesema kumbukizi hiyo yenye jina la Mkapa Legacy Summit inategemewa kufanyika kwa siku tatu kuanzia Julai 29-31ambapo imebeba kaulimbiu isemayo; ‘Kuchagiza uendelevu wa ndani kuelekea upeo mpya’
“Kauli mbiu ya Kumbukizi ya mwaka huu ni ‘Kuchagiza Uendelevu wa Ndani kuelekea kwenye Upeo Mpya’ Kauli mbiu hii inaangazia maono na kazi mbalimbali za Hayati Benjamin Mkapa katika kuongeza chachu ya maendeleo ya ndani ya nchi, kwa kutumia raslimali, sera na mifumo ya ndani katika kuleta maendeleo” Amesema Dk. Mkondya-Senkoro
Hata hivyo ameeleza kuwa Lengo kuu ni kubadilishana uzoefu, maarifa, kubaini fursa za masomo na ajira za ndani na nje ya nchi kwa wataalam wa afya, na pia kupendekeza mikakati ya pamoja ya kupunguza changamoto za rasilimali watu katika sekta ya afya nchini.