Leo August 6,2018 tunayo story kutokea Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo imemuonya mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko kwa kushindwa kutoa taarifa sahihi kwa mdhamini wake.
Hakimu Mashauri ametoa onyo hilo katika kesi ya kufanya maandamano yasiyo halali inayowakabili Viongozi 9 wa CHADEMA akiwemo Freeman Mbowe, ambayo iliitishwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.
Kabla ya kutolewa onyo hilo, wakili wa serikali Mkuu, Faraja Nchimbi ameeleza kuwa shauri hilo limeitishwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali (Ph), lakini mawakili wa utetezi hawapo mahakamani.
Pia mara ya mwisho mshtakiwa wa 5, Esther Matiko hakufika mahakamani kwa madai alipata dharura, hivyo kwa vile leo amefika mahakamani anaweza kuielezea mahakama.
Matiko amedai kuwa alipigiwa simu ya dharura kwenda shuleni kwa mwanaye nchini Kenya August 1,2018 na akaondoka saa 4 usiku.
“Baada ya kufika shule niliambiwa mwanangu anaumwa, nilipompeleka hospital niliambiwa ana Tetekuwanga na akaambiwa apumzike kwa siku 4,”amedai Matiko.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mashauri alimuhoji Matiko kuwa mbona mdhamini wake alishindwa kuieleza mahakama kwamba amekwenda Kenya kufanya nini.
“Nakupa warning mara nyingine uwe muwazi na mkweli iwe mara ya mwisho, siku nyingine unapaswa kumueleza mdhamini wako ni dharura gani imekupata,”amesema Mashauri na kuahirisha kesi hiyo hadi August 13,2018.
Mbali na Mbowe, washitakiwa wengine ni Katibu mkuu wa CHADEMA, Dk. Vincent Mashinji, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee na Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya.
Miongoni mwa mashtaka yanayomkabili washtakiwa hao ni kula njama kwa nia ya kutenda kosa, kufanya mkusanyiko usio halali, kufanya mkusanyiko wenye ghasia na kukiuka tamko la kutawanyika na kuendeleza mkusanyiko wenye ghasia.
Washtakiwa hao wanadaiwa kati ya February mosi na 16, mwaka huu, Dar es Salaam kwa pamoja na ujumla wao walikula njama ya kutenda makosa ya kufanya mkusanyiko usihalali, mkusanyiko wenye ghasia na kukiuka tamko la kutawanyika.
Pia wanadaiwa wakiwa na wenzao 12 ambao hawapo mahakamani siku hiyo waliandamana isivyo halali wakiwa na lengo la kuvamia ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na kutokana na mkusanyiko huo wa ghasia walisababisha kifo cha Akwilina Akwiline na majeraha kwa askari H. 7856PC Fikiri na E6976 CPL Rahim Msangi.