Takriban watu 7 walifariki na wengine watatu kujeruhiwa vibaya kufuatia maporomoko ya ardhi yaliyotokea Jumanne, Agosti 1, katika eneo la uchimbaji madini linaloitwa seminari, huko Bondo katika mkoa wa Bas-Uele.
Tukio hilo lilijiri majira ya saa tisa na nusu usiku saa za Afrika ya Kati, amesema waziri wa madini wa mkoa na msemaji wa serikali ya mkoa wa Bas-Uele, Ursule Lelo Di-Makungu.
Amebainisha kuwaripoti hii ni ya muda kwa vile utafutaji unaendelea kujaribu kupata wachimbaji ambao bado wamefukiwa chini ya ardhi.
Kulingana na ushuhuda uliokusanywa, wachimbaji 11 hadi 12 walikuwa katika mgodi, wakitafuta dhahabu walipoangukiwa na udongo.
Baada ya zoezi la kwanza la uokoaji, miili 7 ilipatikana na baadhi ya manusura, amesema msemaji wa serikali ya mkoa wa Bas-Uélé, Ursule Lelo Di-Makungu.
Anasema kuwa baraza la mawaziri la mkoa limeanzisha kitengo cha kukabiliana na migogoro. Kitngo hiki kimeajiri watu 1,500 kwenye eneo la tukio huko Baye kuendelea na uchimbaji katika jaribio la kutafuta manusura wowote.
Rais Félix Tshisekedi, katika ujumbe uliotumwa kwenye ukurasa wa twitter ya Ofisi ya rais, anapendekeza kufunguliwa kwa uchunguzi.
“Kwa kusubiri matokeo ya uchunguzi wa kubaini chanzo cha ajali hii, Mkuu wa Nchi anatoa rambirambi kwa familia na wapendwa wa marehemu ambao wako katika huzuni mkubwa kutokana na vifo hivi”, anabainisha katika ujumbe huu.
Félix Tshisekedi anasema kusikitishwa na kutoweka kwa Wakongo wengi kufuatia ajali hii mbaya.