Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Singida imetupilia mbali kesi ya rushwa iliyokuwa ikimkabili mfanyabiashara, Haider Hussein Gulamali baada ya kutokuwa na kesi ya kujibu.
Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Consolata Singano ambapo amesema amezingatia ushahidi wa mashahidi 9 wa upande wa Jamuhuri waliofika mahakamani hapo ambapo hakuna ushahidi unaomgusa Gulamali moja kwa moja.
Katika kesi hiyo ambapo Mawakili wa Gulamali alikuwa Godfrey Wasonga, Hakimu Singano amesema moja ya sababu ni kutofautiana kwa mashahidi watatu kuhusu bahasha iliyobeba fedha.
Amesema katika ushahidi wao kila shahidi ametaja rangi tofauti ambapo mmoja ametaja Kaki, mwingine nyeupe, huku wa mwisho akitaja Brown jambo ambalo mahakama imeshindwa kuelewa bahasha ipi ilibeba fedha.
Pia amesema hata hatua za ukamataji hazikuanishwa vizuri kwani hakuna mahali iliyoonyesha Pesa ziliwahi kutaifishwa hadi zilipofikishwa mahakamani, pia namna zilivyotunzwa mpaka kufikishwa kama ushahidi.
Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Singano amesema anatupilia mbali kesi hiyo na kumfanya Gulamali ambaye alikuwa ni mgombea wa ubunge wa (CCM) Singida Kaskazini kuwa huru.
Katika kesi hiyo, miongoni mwa mashahidi hao ni Ofisa Usalama mkoa wa Singida, Kiseo Nzowa anayedaiwa kupewa rushwa hiyo ambapo amedai anafanya kazi kwa mujibu wa sheria.
Shahidi huyo amedai kuwa Gulamali alimpa Sh.Mil 2 ili amsaidie kupitisha jina lake kwenye kinyang’anyiro cha ubunge Singida Kaskazini na kwamba yeye hakuwa Mjumbe Kamati ya Siasa Wilaya.