Mfanyabiashara Mustapha Kambangwa (34) amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashtaka manne ikiwemo utakatishaji fedha wa Sh. Bilioni 188.9 kupitia mashine ya Kilektroniki ya EFD.
Kambangwa amesomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Mtenga na
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Christopher Msigwa ambaye amedai ametenda makosa hayo katika siku tofauti kati ya June Mosi ,2016 na November 2, 2018.
Miongoni mwa makosa hayo, anadaiwa katika tarehe tofauti kati ya June Mosi, 2016 na November 2, 2018 maeneo ya jiji la Dar es Salaam mshtakiwa alijifanya kuwa amesajiliwa kukusanya kodi ya VAT Sh.Bil 188.9 kwa kujifanya anakusanya fedha hizo kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Katika kosa la utakatishaji fedha, anadaiwa tarehe na kipindi hicho, maeneo ya jiji la Dar es Salaam alijipatia au kujimilikisha fedha hizo alizozipata kutokana na makato ya kodi ya VAT ambazo zilipaswa kutolewa kwa Kamishna wa TRA na mshitakiwa huyo alipaswa kujua kuwa fedha hizo ni zao la kosa la ukwepaji kodi
Msigwa amedai katika tarehe tofauti kati ya June Mosi,2016 na November 2, 2018 maeneo ya Dar es Salaam kwa vitendo vya makusudi vya kukwepa kodi alitumia mashine ya Kieletroniki ya EFD na huku akijua kwamba hajasajiliwa kama mlipakodi ya VAT aliisababishia TRA hasara ya Sh.Bil 188,928,752,166.
Upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika, Hakimu Mtega amesema mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo hadi itakapopata kibali cha kuendelea na shauri hilo. kesi imeahirishwa hadi December 17, 2018.