Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa NIDA, Dickson Maimu na wenzake watano wamesomewa mashtaka 100 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ikiwemo utakatishaji fedha wa Sh.Bil 1.17
Mbali na Maimu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Meneja Biashara wa NIDA, Avelin Momburi, Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege na Ofisa Usafirishaji, George Ntalima.
Wengine ni Xavery Silverius maarufu kama Sliverius Kayombo na Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond.
Maimu na wenzake waliachiwa huru January 28,2019 na mahakama hiyo baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP) kusema hana nia ya kuendeleza mashtaka dhidi yao.
Miongoni mwa mashitaka yanayowakabili ni kula njama ya kulaghai, kughushi, kusababisha hasara na matumizi mabaya ya madaraka.
Vigogo hao wamesomewa kesi yao ya uhujumu uchumi namba 7 ya mwaka 2019 mbele ya Hakimu Mkazi, Salum Ally na Wakili wa Serikali, Wankyo Simon akisaidiana na Leonard Swai.
Miongoni mwa mashitaka waliyosomewa ni utakatishaji fedha wa Sh.Bil 1.17 ambapo linamkabili Maimu, Ndege na Ntalima.
Inadaiwa walitenda kosa hilo kati ya July 19, 2011 na August 31, 2015 jijini Dar es Salaam ambapo walijihusisha katika muamala wa Sh.Bil 1.17 ambapo walizitoa fedha hizo kupitia Benki ya CRDB PLC, Vijana Ilala hali ya kuwa wakijua fedha hizo ni zao la fedha haramu.
Katika kosa la kula njama ya kulaghai ambalo linamkabili Maimu, Ndege na Ntalima wanadaiwa walilitenda kati ya July 19, 2011 na August 31, 2015 wakiwa karika maeneo tofauti ya jiji la Dar es Salaam waliidanganya NIDA kwa lengo la kujipatia Sh.Bil 1.17.
Katika mashtaka hayo, Mshtakiwa wa pili( Momburi) na sita(Raymond), wao hawana mashtaka ya utakatishaji.
Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yanayowakabili hawakutakiwa kusema chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi za Uhujumu uchumi isipokuwa Mahakama Kuu pekee.
Upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa shauri hilo, umekamilika na wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomewa, washtakiwa Maelezo ya Mashahidi pamoja na vielelezo(Committal Proceedings). Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 12, 2019.