Leo March 21, 2018 stori ninayokusogezea ni kumhusu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Ferdinand Wambali amewataka Mahakimu wapya walioajiriwa katika muhimili wa mahakama kufanya kazi kwa maadili na kutojihusisha na vitendo vya rushwa.
Akizungumza na baadhi ya Mahakimu Jaji Wambali amewaasa Waajiriwa hao kuzingatia misingi ya sheria ya muhimili huo.
“Katika ufanyaji kazi wenu wa Uhakimu, mnatakiwa kuzingatia mambo makuu manne ya msingi, Ujuzi wa taratibu na mazoea ya Kimahakama, uelewa kuhusu Sheria za Msingi Substantive law na Sheria za Mwenendo Procedural Law kuangalia mazingira ya utoaji haki na kadhalika,” -Jaji Wambali.
Pia amewataka Mahakimu hao kufanya kazi kwa kuwaheshimu Wadau wote wanaojumuika nao katika mchakato mzima wa utoaji wa haki, ikiwa ni pamoja na Makarani, Wazee na Baraza na wengineo.
“Heshimuni kila mtu mnayeingia naye Mahakamani, kila mtu ana mchango katika upatikanaji wa haki na moja ya sifa ya Hakimu ni upole lakini upole sio udhaifu, amesisitiza Jaji Wambali.
Naye Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu-Mahakama ya Tanzania, Edward Nkembo amesema kuwa jumla ya Mahakimu wapya 78 kati ya 100 wameripoti kazini.
Nkembo ameeleza kuwa baadhi ya Mahakimu na Watumishi wa Kada watakaoshindwa kuripoti ndani ya siku 14 tangu Machi 20, nafasi zao zitatafutiwa watu wengine watakaoomba na kukidhi vigezo.