Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu kifungo cha miaka 20 jela wakulima wawili na mfanyabiashara mmoja baada ya kupatikana na hatia katika mashtaka ya kukutwa na nyara za serikali ikiwemo vipande vitano vya Meno ya Tembo.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi sita wa upande wa mashtaka pamoja ushahidi wa upande wa utetezi ambao washtakiwa walijiteta wenyewe.
Waliohukumiwa ni Amir Kigahhey(44) mkulima, Jairan Rashid (33) mkulima na mfanyabiashara Ibrahim Mkande (30).
Katika hukumu hiyo, Hakimu Shaidi amesema upande wa mashtaka umethibitisha makosa pasina kuacha shaka, hivyo mahakama inawatia hatiani washtakiwa kwa mashtaka mawili yanayowakabili. Hata hivyo, washtakiwa wamesema watakata rufaa.
Washtakiwa hao walitiwa hatiani katika kosa la kuendesha mtandao wa kihalifu na kukutwa na vipande vitano vya meno ya tempo vyenye thamani ya Shilingi 65,640,000.Inadaiwa walitenda kosa hilo kati ya January 15 na 22,2016.