Kamanda wa Polisi Kanda Maluum ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa amesema jeshi la polisi limetoa dakika tano (sawa na sekunde 300) kwa ajili ya watu walioruhusiwa kuweza kupiga fataki katika sherehe za mkesha wa mwaka mpya wa 2019.
Kamanda Mambosasa amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa sherehe hizo za mwaka mpya jeshi la polisi limejipanga ili kuhakikisha wananchi waliokuwepo kwenye nyumba za ibada kwa ajili ya mkesha wataabudu kwa usalama na kuzindikizwa nyumbani kwao kwa usalama.
“Kuna matendo yamekuwa yakijirudia rudia miaka ya nyuma ambapo ni uchomaji wa matairi, nawasihi na kuwahasa wenye vitendo hivyo kuacha mara moja sambamba na kuchoma moto kati kati ya barabara,”amesema.
Pia amesema milipuko ya aina yoyote haitaruhusiwa isipokuwa wale walioruhusiwa, kwani zitakazoruhusiwa ni zile nyepesi na sio milipuko itakayowashitua watu kwamba ni bomu ama fataki.
“Muda wa kufanya hivyo maeneo tuliyotoa vibali ni dakika tano tu, kuanzia saa sita kamili hadi na dakika tano tutakuwa tumemaliza atakeyekwenda kinyume na hapo tutahesabu ni utendaji wa uhalifu, “amesema.