Leo August 6, 2018 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na Balozi wa China hapa nchini Wang Ke ambaye pamoja na kufanya nae mazungumzo amewasilisha barua kutoka kwa Rais wa China Xi Jinping.
Katika mazungumzo hayo Wang Ke amemueleza Rais Magufuli kuwa uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na China umeendelea kukua kwa kasi kubwa hususani katika masuala ya kiuchumi, ambapo miradi mbalimbali ya maendeleo imetekelezwa na inaendelea kutekelezwa na kwamba katika kipindi cha miaka 6 iliyopita uwekezaji wa China nchini Tanzania umekuwa mara kumi kutoka Shilingi Trilioni 1.58 hadi kufikia Shilingi Trilioni 15.82.
Wang Ke amemhakikishia Rais Magufuli kuwa China itaendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo ya Tanzania.
Kuhusu ombi alilolitoa Rais Magufuli wakati meli ya matibabu ya China ilipokuja hapa nchini mwezi Novemba 2017, Wang Ke amesema Rais Xi Jinping ameshafanyia kazi ombi hilo kwa kutoa udhamini wa masomo kwa madaktari 20 watakaosomea ngazi ya uzamili na uzamivu katika matibabu ya ini na uboho (bone marrow) katika Chuo Kikuu cha Shandong cha China, na pia nafasi 30 za wataalamu watakaohudhuria semina ya mafunzo ya usimamizi wa hospitali.
Rais Magufuli amemshukuru Rais Xi Jinping kwa kutoa nafasi hizo za masomo na kwa mchango mkubwa wa China katika maendeleo ya Tanzania, na amemuomba Wang Ke kufikisha ujumbe wake kwa Rais Xi Jinping kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake wa kidugu na kihistoria na China.
Rais Magufuli ametoa wito kwa Wang Ke kuendelea kuwahimiza wawekezaji zaidi kuja kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali kwa manufaa ya pande zote mbili na kwamba Serikali ya Tanzania itakuwa tayari kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara.
Wakati huo huo, Rais Magufuli ameagana na Balozi wa Canada hapa nchini Ian Myles na Balozi wa Ubelgiji hapa nchini Paul Cartier baada ya Mabalozi hao kumaliza muda wao.
Baada ya mazungumzo hayo Mabalozi hao wameelezea kufurahishwa kwao na uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi zao na wamempongeza Rais Magufuli na Serikali anayoiongoza kwa hatua kubwa za kuleta mageuzi ya kiuchumi, kuboresha utendaji kazi wa watumishi wa umma, kupambana na rushwa na kuboresha huduma za kijamii.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi Ezechiel Nibigira ambaye amewasilisha barua kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Burundi Pierre Nkurunziza.
Aidha, Rais Magufuli amefanya mazungumzo na Nibigira, mazungumzo ambayo yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Susan Kolimba na Balozi wa Burundi hapa nchini Gervais Abayeho.