Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu mmiliki wa Kampuni ya Mabasi ya Muro, Majid Kimaro kulipa faini ya Milioni 115 au kifungo cha miaka 8 jela baada ya kukiri kosa la utakatisha fedha na kuongoza genge la uhalifu.
Muro anadaiwa aliongoza genge hilo la uhalifu ili kuiba mafuta katika bomba linalomilikiwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).
Pia mahakama imeamuru gari aina ya Scania lenye namba za usajili T 856 ADH ambalo lilitumika kuiba mafuta zaidi ya lita 26,875.25 ya Dizeli na Petroli litaifishwe na kuwa mali ya serikali.
Muro alifikishwa mahakamani hapo October, 2018 na kukaa gerezani miezi 2 ambapo alifutiwa mashitaka na kusomewa upya mashitaka hayo na kuyakiri.
Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ambapo alisema mahakama inamtia hatiani mshitakiwa kwa makosa mawili baada ya kukiri kutenda makosa hayo mwenyewe.
Alisema katika mashitaka ya kuongoza genge la uhalifu, Muro anapaswa kulipa faini ya Sh. Milioni tano au kifungo cha miaka mitatu jela.Pia alisema katika mashitaka ya utakatishaji fedha mshitakiwa atatakiwa kulipa faini ya Sh. Milioni 110 au kifungo cha miaka mitano jela.
Awali Wakili wa Serikali, Simon Wankyo akisaidiana na Jacqueline Nyantori na Patrick Mwita waliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa washitakiwa kwa sababu makosa hayo ya wizi husababisha kuathirika kwa uchumi na nchi kukosa mapato.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 81/2018 inadaiwa kati ya July Mosi, 2016 na January 8, 2018 katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kigamboni, Dar es Salaam na maeneo mengine Muro akiwa pamoja na wenzake ambao hawako mahakamani, kwa kujua aliongoza genge la uhalifu kwa lengo la kutoboa bomba la mafuta la TPA na kuiba mafuta ili kupata faida.
Muro anadaiwa katika mashitaka ya pili kuwa, kati ya July Mosi, 2016 na January 8, mwaka huu maeneo tofauti tofauti wilayani Kigamboni, walipata lita 15,950.3 za mafuta ya diseli na lita 10,925.22 za mafuta ya petroli na kusambaza mafuta hayo kwenye vituo vyake vya mafuta na kuyauza kwa watu mbalimbali huku akijua kwamba wakati akipata mafuta hayo, yametokana na makosa ya uhalifu.