Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk.Vincent Mashinji amewataka wafuasi wa chama hicho kuudhuria usikilizwaji wa Rufaa ya Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.
Dk.Mashinji ameyaeleza hayo mara baada ya rufaa hiyo kuahirishwa hadi November 30, 2018 kwa ajili ya kutolewa uamuzi na Jaji Sam Rumanyika kama atengue uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ama lah kuhusu kufutiwa dhamana kwa Mbowe na Matiko.
“Suala limesikilizwa na tumeambiwa tuonane kesho saa 5 kwa ajili ya mapingamizi yaliyowekwa na jamuhuri, hivyo naomba viongozi, wanachama na watu wote tukutane hapa kesho saa 5,”amesema.
Katika rufaa hiyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Dk. Zainabu Mango aliwasilisha hoja za pingamizi akidai vifungu vya sheria walivyotumia kuwasilisha rufaa si sahihi hivyo anaomba rufaa itupwe na kuongeza kuwa walitakiwa kuwasilisha rufaa chini ya kifungu cha sheria namba 359 na 361 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai.
Katika majibu yake, Wakili Peter Kibatala amedai kuwa hoja za upande wa jamhuri hizo mashiko kwa sababu mahakama ilishamalizana na suala la nyaraka.
Mbowe na Matiko walifutiwa masharti ya dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Ijumaa wiki iliyopita katika kesi inayowakabili pamoja na wenzao ya mashtaka 13 ikiwemo uchochezi.