Mapya yanazidi kuibuliwa juu ya sakata linaloiandama Kampuni ya Reli Limited (TRL) ya uingizaji mabehewa feki nchini, sasa ikifahamika kuwa hata Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), haikushirikishwa kwenye manunuzi hayo.
Kufichuka kwa ukweli huo, ndiko sasa kunaongeza hali ya wasiwasi ndani ya TRL na kuna uwezekano mkubwa sakata hilo litaibua mjadala katika mkutano wa 19 wa Bunge unaotarajiwa kuanza kesho mjini Dodoma.
Ukweli huo uliwekwa wazi mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Luaga Mpina, wakati wa kikao cha kamati yake na PPRA.
Mpina alitoboa siri hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao baina ya kamati yake na PPRA.
Alisema kamati yake iliwahoji PPRA kuhusu ushiriki wao kwenye ununuzi wa mabehewa hayo na kubaini kuwa mamlaka hiyo haikushirikishwa.
“Tunashangaa kwamba hata PPRA hawakushirikishwa kwenye mchakato wa ununuzi wa mabehewa hayo. Hadi sasa ninapozungumza hawajawahi kuitwa kushuhudia mabehewa 150 yaliyobainika kuwa ni feki,” Mpina.
Mpina ambaye pia ni Mbunge wa Kisesa, alisema hali hiyo inaonyesha mambo kufanywa kinyume cha taratibu katika mchakato mzima wa ununuzi wa mabehewa hayo, hali aliyosema imechangia kuingiza hasara serikali kwa kununua mabehewa feki.
Ili kulishughulikia suala hilo sawa sawa, mbunge huyo alisema kamati yake inatarajia kukutana na uongozi wa PPRA chini ya mkurugenzi wake, Laurent Shirima Ijumaa wiki hii mjini Dodoma, kwa ajili ya kupata taarifa zaidi kuhusu ununuzi wa mabehewa hayo feki.
Wakati huo huo, kamati iliyoudwa na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, imewasilisha taarifa ya uchunguzi wake kwa Bodi ya Wakurugenzi wa TRL kama walivyoagizwa na Waziri wa sasa wa Uchukuzi, Samuel Sitta, ambaye anatarajiwa kukabidhiwa ripoti hiyo.
NIPASHE
Serikali imesema kuanzia kesho kituo cha mzani cha Kibaha kitafungwa na magari yote yataendelea kupimwa kwenye kituo kipya cha Vigwaza kilichopo Mkoa wa Pwani.
Pia inatarajia kutumia Sh. bilioni 8 kujenga mizani mipya mitano ya kisasa katika maeneo mbalimbali ikiwamo eneo la Mikese, Dumila, Nala mkoani Dodoma, lengo likiwa ni kupunguza msongamano wa magari katika maeneo ya mizani.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale, aliyasema hayo wakati wa utoaji wa taarifa juu ya kuanza kutumika kwa mzani mpya wa Vigwaza.
Mfugale alisema kesho Serikali itakifunga rasmi kituo cha mzani cha Kibaha na magari yote yataendelea kupimwa kwenye kituo kipya cha Vigwaza.
Alisema kituo hicho ni cha kisasa chenye mtambo wa kuchambua magari yaliyozidisha uzito yakiwa yanatembea.
Pia, alisema kituo hicho kina mzani mkubwa unaoweza kupima gari lote kwa mkupuo.
“Aidha barabara za kuingia kwenye mzani huo wenye urefu wa kilomita 1.8 zimejengwa kwa zege lenye uwezo wa kudumu kwa miaka 50 na una uwezo wa kupima gari moja kwa sekunde 30 badala ya dakika 1.5 kwa mzani wa zamani,” Mfugale.
NIPASHE
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, ametoa siku saba kwa Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam, kuhakikisha inajenga mtaro wa kupitisha maji machafu ili kuondokana na majitaka hayo kuingia kwenye mitaro mipya inayojengwa.
Alisema kama hospitali hiyo itapuuza agizo hilo, ndani ya siku saba, serikali itachukua hatua stahiki ikiwamo ya kuzuia kutoa huduma.
Makonda alitoa kauli hiyo alipotembelea kwenye maeneo ya Mikocheni kukagua miundombinu ya barabara na mitaro inayojengwa ili kudhibiti athari za mvua zinazotarajia kunyesha wakati wowote.
Makonda, alishuhudia mtaro wa majitaka ya hospitali hiyo ukitiririsha uchafu kuelekea kwenye mitaro mipya inayojengwa hali iliyosababisha mitaro hiyo kujaa taka kabla ya kukamilika kwake.
Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni, Mbaraka Mkwiya, alisema miradi ya ujenzi wa mitaro ya maji taka kwenye bonde la mpunga unagharimu takribani Sh. bilioni sita na barabara tano za mitaa ya Mikocheni na Msasani ambazo zitagharimu Sh. bilioni 3.3 ambayo yote, inatarajia kukamilika miezi michache ijayo.
MWANANCHI
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amewaaga wapigakura wake kuwa hatakuwa tena mbunge wao, akisema kuwa kesi ya dhidi ya Chadema ilitupwa na Mahakama Kuu kutokana na baadhi ya majaji kutajwa kwenye kashfa ya escrow.
Chadema ilimvua Zitto uanachama saa chache baada ya Mahakama Kuu kutupa shauri lake alilofungua akitaka chombo hicho cha sheria kimlazimishe katibu mkuu wa chama hicho kumpa nyaraka za mwenendo wa vikao vya Kamati Kuu vilivyomvua nyadhifa zote, huku akifanikiwa kupata amri ya muda ya kuizuia Chadema kumjadili.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Mwandiga mkoani Kigoma jana, Zitto alisema hatakuwa mbunge wa jimbo hilo baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, na akatumia fursa hiyo kueleza safari yake ya kisiasa ndani ya Chadema na mtazamo wake baada ya kufukuzwa uanachama.
“Nimejifunza mengi nikiwa mbunge. Katika utumishi wangu kwenu, bungeni nimejifunza namna nchi yetu inavyoendeshwa. Katika kujifunza huko kuna mambo kadhaa nimefanya ya kujivunia na mengine ni makosa,” alisema Zitto ambaye alikuwa naibu katibu mkuu wa Chadema.
“Nimejifunza kuwa mzalendo zaidi kwa nchi yangu na kuwatumikia watu wa nchi hii. Ndiyo maana hamkunisikia tu nikitetea watu wa Kigoma pekee, bali watu maeneo mengine ya nchi yetu na makundi mbalimbali ya kijamii.”
Alisema safari yake ya ubunge ilikuwa ngumu yenye mafunzo makubwa na imemfanya apevuke kifikra na kupata mafunzo.
Awali, akizungumza na waandishi wa habari, Zitto alisema: “Bado nina nia ya dhati ya kuendelea kuwatumika Watanzania kama mwakilishi wao kupitia jimbo lolote nchini.
MWANANCHI
Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wiki ijayo wanatarajia kuzindua treni ya mizigo ‘block train’ kutoka jijini hapa kwenda nchi wanachama kwa kutumia reli ya kati.
Uzinduzi huo wa treni zenye mabehewa 20 hadi 21 utakwenda sambamba na mkutano wa marais wa EAC utakaofanyika Machi 25-26, Dar es Salaam.
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mawaziri wa uchukuzi wa jumuiya hiyo na kuongeza, uzinduzi huo utaanza na safari ya kwenda Burundi na Rwanda kwa siku hiyo.
Sitta ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Afrika Mashariki kabla ya kuwa Waziri wa Uchukuzi, alisema treni hizo pia zitasafari kutoka Dar es Salaam kwenda Uganda na DRC.
Akitolea mfano wa treni itakayo kwenda Rwanda alisema ikitoka jijini hapa itaishia Isaka ambapo kutakuwa na magari kwa ajili ya kubeba mizigo hiyo hadi Rwanda.
Alisema, utaratibu huo utakuwa endelevu na unalenga kusaidia nchi wanachama kusafirisha mizigo mingi inayoingia na kutoka nje ya nchi kwa haraka lakini hasa zile ambazo hazijapakana na bahari.
Mbali na uzinduzi huo, Sitta alibainisha kwamba wakuu hao watakuwa na mkutano kwa ajili ya kujadili namna ya kuboresha usafiri kwa ukanda wa kati.
Baada ya mkutano wa kwanza, utafuatiwa na mkutanao wa wakuu hao pamoja na wawekezaji.
Waziri wa Uchukuzi wa DRC Justine Kanumba ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa mkutano huo, aliipongeza Tanzania kwa hatua hiyo ambayo alisema itasaidia kurahisisha usafirishaji kwa nchi wanachama.
MTANZANIA
Makundi ya watu wa kada mbalimbali yamezidi kutua nyumbani kwa Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM), yakimtaka achukue fomu ya kuwania urais kupitia CCM muda utakapofika.
Lowassa ambaye pia ni Waziri Mkuu wa zamani, kwa wiki kadhaa sasa amekuwa akipokea wageni wa makundi mbalimbali nyumbani kwake wakimtaka awanie nafasi hiyo ya uongozi wa juu wa nchi.
Kutokana na joto hilo la urais ndani CCM, jana makundi mawili ya wana CCM yalibisha hodi nyumbani kwa kada huyo na kumshawishi kufanya hivyo pamoja na kumkabidhi fedha za kuchukulia fomu.
Kundi la kwanza lilikuwa ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Arumeru ambao waliwasilisha ombi lao kwa mbunge huyo pamoja na kumkabidhi Sh milioni moja za fomu.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti Mstaafu wa Halmashauri ya Meru, John ole Saitabau, alisema wamefikia hatua hiyo baada ya kuona Lowassa ana sifa zote za kuwania nafasi hiyo ya uongozi wa nchi.
“Sisi tumekuja hapa kukushawishi uchukue fomu ya kuwania urais kupitia chama chetu cha CCM… uwezo huo unao na Tanzania inakuhitaji,” Ole Saitabau.
Naye Mathias Manga, ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (MNEC), alisema zaidi ya asilimia 75 ya wajumbe wa NEC wanamshawishi Lowassa awanie urais kwa sasa kutokana na sifa yake ya uchapakazi mbele ya jamii.
Kundi la pili ambalo lilifika nyumbani kwa Lowassa ni la marafiki wa Lowassa, Kanda ya Kaskazini, ambako zaidi ya watu 500 kutoka kada mbalimbali wakiwamo walemavu wa macho na watu wenye albino, walimkabidhi Lowassa Sh milioni 2.5.
Akisoma risala kwa niaba ya vijana waliotoka katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, Protas Soka, alisema kwa sasa Watanzania wanamuhitaji Lowassa aweze kuliongoza Taifa.
MTANZANIA
Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM) amewaomba viongozi wa dini nchini kuendelea kuwaombea viongozi wa serikali wakiwamo wabunge ili wawatumikie wananchi kwa kutanguliza hofu ya Mungu.
Kauli hiyo aliitoa jana wakati wa mazishi ya aliyekuwa mtawa wa Kanisa Katoliki Parokia ya Imiliwaa, marehemu Insetrud Maria.
Alisema viongozi wa dini wamekuwa wakifanya kazi ya kuliombea taifa na watu wake lakini wanasiasa na viongozi wa serikali wamekuwa wakiwatumikia wananchi kimwili hivyo kuna haja ya viongozi wa dini kuendelea kufanya kazi ya kuwaombea viongozi.
“Maandiko matakatifu yanasema; ‘enendeni duniani mkawafanye watu wote kuwa wanafunzi wangu’…chama cha walimu hapa wamesema kuwa Sr.Maria alikuwa mwalimu mzuri hivyo ni wazi alizifanya kazi zote, ya kiroho na kimwili,” alisema.
Kwa kutambua mchango wake alioutoa duniani enzi za uhai wake, mbunge huyo aliahidi kujenga darasa katika shule ya sekondari parokiani hapo kama njia ya kumuenzi zaidi.
Filikunjombe alisema kumbukumbu hiyo itakuwa kielelezo cha mchango wa Sr.Maria katika maendeleo ya Mkoa wa Njombe.
” Sr.Instrud Maria mbali ya kazi yake ya utawa pia alikuwa ni mwalimu na mchango wake katika shughuli zake ni mkubwa hivyo nawaombeni tumuenzi kwa kujenga darasa moja ambalo litaandikwa jina lake kama kumbukumbu ya sasa na baadaye,”alisema Filikunjombe.
DIRA
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili inalalamikiwa kuwa na unyanyapaa kwa wagonjwa wanaofika hapo ili kupata huduma za afya kutokana na madaktari na manezi kuwa na kauli mbaya na zisizofaa kwa wagonjwa.
Baadhi ya wagonjwa wanaopata huduma katika hospitali hiyo inayotegemewa na Taifa ni tia maji tiamaji kwa vile kwa vile ni mbovu na haifai na kusababisha kuishushia hadhihospitali hiyo.
Katika hospitali hiyo wodi inayolalamkiwa zaidi ni ile ya mifupa MOI kwa kudaiwa kujaza watu wengi hadi kulala chini, mashuka hayabadilishwi kwa wakati na pia madaktari hawapiti kwa muda uliopangwa.
“Hii hospitali ni bure kabisa nimemleta mgonjwa hapa hali ikiwa mbaya kabisa,lakini daktari hakuwa na muda zaidi ya kuuliza nimejipanga vipi ili mgonjwa wangu ahudumiwe vizuri, hadi nilipompa pesa ndipo mgonjwa wangu akatibiwa, inasikitisha”.
Aliongeza kuwa hata alipomfikisha mgonjwa wake kitengo cha MOI wauguzi waliokuwepo zamu siku hiyo hawakumpokea wala kumjali mgonjwa na kuendelea na maongezi.
UHURU
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Itimila mkoani Simiyu, kimelitaka Jeshi la Polisi kusitisha msako wa waganga wa jadi wanaopiga ramli chonganishi.
Hatua hiyo imekuja huku Jeshi la Polisi katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa, likiwa katika msako mkali wa kuwakamata waganga wa namna hiyo.
Mbali ya kulitaka jeshi hilo kusitisha shughuli hiyo, pia CCM imetaka waganga hao wa jadi wapewe muda wa kutosha ili wapatiwe leseni za kutambulika kwa kazi zao.
Agizo hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Mohamoud Mabula, wakati wa mkutano wa waganga wa jadi uliofanyikia katika viwanja vya Shule ya Sekondari Lagangabilili wilayani humo mwishoni mwa wiki.
Mabula alimtaka Mkuu wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo, aliyehudhuria mkutano huo, kusitisha shughuli hiyo kwa maelezo kwamba baadhi ya waganga hao wa jadi wamekamatwa kutokana na kukosa leseni lakini hawajihusishi na upigaji wa ramli.
Hata hivyo, alisema anatambua umuhimu wa agizo la Rais Jakaya Kikwete, lakini kuhusu uendeshaji wa operesheni hiyo anaipinga kutokana na waganga wengi kutopewa muda wa kujiandikisha ili kupatiwa leseni.
“Operesheni hii inataka kutukumbusha operesheni kimbunga kwa wahamiaji haramu na kukamata majangili. Operesheni hizi zimeondoka na viongozi wengi wachapakazi, sasa hatutaki Chama kurudia makosa. Tunataka operesheini zifanyike kwa amani na siyo kuwashtukiza watu,” Mabula.
Alieleza kuwa maagizo ambayo yamekuwa yakitolewa na viongozi wao ngazi za juu kwa upande wa serikali, huwaweka katika wakati mgumu viongozi wa Chama ngazi za mkoa na wilaya kutokana na maagizo hayo kutekelezwa kwa nguvu.
“Sisi kama Chama, tumeanza kupata malalamiko kutoka kwa wapigakura wetu. Wanasema CCM inataka kuwafukuza waganga wa jadi…kwa hili hatukubali tulalamikiwe tunachohitaji msako ufanyike lakini kwa amani na watafutwe wapiga ramli tu na siyo waganga wote,” alisema.
Kauli hiyo ya kiongozi huyo wa CCM, ilipokewa kwa shangwe na waganga wa jadi zaidi ya 200 waliohudhuria mkutano huo.
HABARILEO
Mbunge wa Rufiji ambaye pia ni Waziri wa afya Dk. Seif Rashid juzi alichangia kuyaokoa maisha ya mama mjamzito Amina Bakari sliyesota porini kwa saa zaidi ya sita akisubiri usafiriwa kumfikisha hospitali ya Wilaya ya Utete kwa ajili ya kujifungua.
Kabla ya msaada huyo Mbunge huyo aliyekuwa akifanya ziara katika jimbo lake alisema, Amina alikodi pikipiki lakini baada ya kutembea umbali mrefu alishindwa kuhimili mtikisiko wake na kuomba ashushe kwa kuwa uchungu ulikuwa umeongezeka.
Dereva wa bodaboda alikubali kumshusha katika eneo la Nyagolombe lakini kwa zaidi ya saa 6 mama huyo hakupata usafiri mwingine huku akihangaika kutokana na kushikwa uchungu.
“Lakini tukiwa tumeshakata tama na kusubiri miujiza ya Mungu ajifungue lilitokea gari na kulisimamisha kuomba msaada, kumbe ndani kulikuwa na Mbunge wetu, hakuwa na hiyana akakubali kutusaidia kumkimbiza hospitali ulikuwa umbali kama wa km 2o hivi ” alisema mwendesha bodaboda.
Hautopitwa na stori yoyote inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook