RAIA TANZANIA
Jeshi la Polisi Katavi linamshikilia Kulwa Rajabu mkazi wa Mpanda akituhumiwa kukutwa na viungo vinavyosadikiwa kuwa ni vya binadamu pamoja na nyara za Serikali nyumbani kwake.
Kamanda wa Polisi Dhahiri Kidavashari amesema mtuhumiwa huyo amekutwa na mifupa mitatu, mshipa na meno mawili ambavyo vinasadikiwa kuwa ni vya binadamu.
Kamanda huyo wa Polisi amesema mtuhumiwa huyo atafikishwa Mahakamani baada ya upelelezi wa awali kukamilika.
RAIA TANZANIA
Baadhi ya wananchi wa Halmashauri ya Meru, Arusha wamesema wanalazimika kutumia bidhaa nyingine ikiwemo mawe ili waweze kubadilishana na kupata maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
Mkazi wa Kijiji cha Shimbumbu alitoa taarifa hiyo kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana wakati akisoma risala ambayo iliandaliwa na wanakijiji wa eneo hilo.
Akijibu kuhusu malalamiko hayo Katibu Mkuu huyo amesema Mbunge wa Jimbo hilo Joshua Nassari hana uwezo wa kuwatatulia changamoto hiyo kwa kuwa hawezi kuzungumza na Waziri wala Rais Kikwete kwa kuwa aliwatukana.
Wanakijiji hao wamelalamika kuwa wanatumia muda mwingi kuchimba mawe ili wabadilishane na maji kutokana na tatizo la kudumu la maji katika eneo hilo.
NIPASHE
Wadau wa habari nchini wamepinga mpango wa Serikali kupeleka miswada ya habari Bungeni kama hati ya dharura huku Spika wa Bunge, Anne Makinda akipingana na hilo kwa kusema kuwa miswada hiyo ilipokelewa kama miswada na sio hati ya dharura.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wadau wa Habari, Kajubi Mukajanga amesema hawaoni sababu ya uharakishwaji wa miswada hiyo miwili wakati hawajapatiwa fursa ya kuipitia na kuitaka Serikali itumie Mkutano wa 19 wa Bunge kusomwa miswada hiyo.
“Kwa kuwa haki ya kupata habari ni haki wezeshi, hakuna budi kuhakikisha kunakuwapo na ushiriki mpana wa wananchi katika hatua zote za utungaji wa sheria hizi mbili,”– Kajubi Mukajanga.
Alisema serikali inatakiwa kuwezesha upatikanaji wa nakala za kutosha za miswada hiyo kwa umma na kutoa muda wa kutosha kwa wananchi kuchangia maoni yao kikamilifu.
Mukajanga amesema kitendo cha miswada hiyo kupelekwa bungeni kama hati ya dharura inaonyesha dhahiri kuwa serikali haikuwa na dhamira ya upatikanaji wa sheria hizo.
“Tunatarajia bunge litafanyakazi yake ya kuishauri serikali kufuata utaratibu mzuri wa uwasilishaji wa miswada hii na kuchangia miswada hiyo kwa kuzingatia maslahi mapana ya kimataifa wakati muafaka utakapofika”— amesema Kajubi Mukajanga huku akiongeza kuwa wameshangazwa na usiri mkubwa uliopo katika kupelekwa miswada hiyo bungeni.
Mwenyekiti Kituo cha Habari kwa Wananchi (TCIB), Deus Kibamba amesema wadau wamekuwa wakishiriki wakati wote katika upatikanaji wa sheria hiyo, hivyo walitegemea kutakuwa na ushirikishwaji katika miswada hiyo.
NIPASHE
Zaidi ya raia wa kigeni 18 wanaotokea Kenya, Uganda na Burundi walioingia nchini kinyume cha sheria wanadaiwa kujiandikisha katika Zoezi la Vitambulisho vya Taifa linaloendelea mkoani Pwani bila kutambulika na mamlaka husika.
Utafiti uliofanywa na kituo cha msaada wa kisheria na haki za binadamu cha TLF umebaini kuwa raia hao wamekuwa wakiishi kinyemela bila ya kufuata taratibu na sheria za nchi na kujihusisha na uuzaji wa biashara ndogo ndogo ikiwemo kahawa na nguo.
“Baada ya taarifa hizo tuliamua kufanya utafiti mdogo na kubaini raia hao ambao wengi ni vijana wa kiume ambao wanajihusisha na biashara ndogo ndogo ambapo wanawake wasio na kazi hufanya juhudi za kuolewa ili waweze kukaa kihalali nchini bila kuhisiwa,” alisema Mohamed Ngozi, msemaji wa TLF.
Alisema baada ya kubaini hali ilivyo waliamua kwenda kwa afisa uhamiaji ambaye alisema wanashughulikia, wakaamua kwenda kwa Mkuu wa Mkoa na mkuu wa wilaya ambao wako katika kamati ya ulinzi na usalama lakini wote walidai watafuatilia.
Ngozi amesema waligundua kuna raia mmoja wa Burundi anayejiita ‘mtu wa Kigoma’ ambaye anajihusisha na kuwakaribisha wageni hao zaidi wakiwa Warundi ambao huwapangishia nyumba kwa ajili ya kuwahifadhi na huwaajiri kwa ajili ya kumuuzia kahawa.
Alisema idadi ya Warundi imekuwa ikiongezeka baada ya kuwapigia wenzao simu waje nchini kwa madai kuwa hakuna sheria zozote zitakazowabana na hivyo wengi kuja kwa njia ya panya na kufanya maskani katika maeneo mbalimbali huku wanaotokea Kenya wakijiita Wakurya na hujikita kufanya biashara za nguo bila ya kuwa na wasiwasi na kuendelea kujiandikisha kupata vitambulisho vya taifa.
Ngozi alisema wamegundua kuwa kuna wahamiaji wengine ambao huishi msituni ambapo wamegundulika katika msitu wa Dutumi na kufanya shughuli ya ukataji miti na kuchoma mkaa na wateja huwafauta huko huko msituni.
Alisema kuwepo kwa wageni hao kuna hatarisha hali ya usalama wa nchi kwani wanapokuja hubeba vitu kama silaha na hakuna wa kuwakagua hivyo wanapofika katika jamii huweza kufanya jambo lolote la kuhatarisha usalama wa nchi huku hata wenyeviti wa vitongoji baadhi yao wameonyesha hawajui lolote pia.
Afisa uhamiaji mkoa wa Pwani, Grace Hokororo, alisema hajapata taarifa za kuwapo kwa wahamiaji haramu Mlandizi na kuwa baadhi ya maafisa uhamiaji wako katika zoezi hilo ili kama kuna mtu atatiliwa mashaka asiendelee na zoezi hilo badala yake apelekwe ofisini kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Gazeti la NIPASHE lilimuuliza Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Halima Kihemba kuhusu kuweko kwa wahamiaji hayo na kujiandikisha kwenye zoezi la vitambulisho hivyo, alisema hana taarifa hizo.
MWANANCHI
Mgogoro kati ya Tanzania na Kenya umefikia hatua mbaya baada ya juzi usiku kikao cha makatibu wakuu wa Wizara za Maliasili na Utalii, Wizara za Afrika Mashariki za pande zote mbili kutafuta suluhu kuvunjika.
Kutokana na kuvunjika kwa kikao hicho, jana Waziri wa Utalii wa Kenya, Phyllis Kandie alisusia kikao cha kutafuta suluhu na waziri mwenzake wa Tanzania, Lazaro Nyalandu.
Akizungumzia kuvunjika sakata hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Adelhelm Meru alisema wajumbe wa Kenya wakiwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii, Dk Ibrahim Mohamed na wa Wizara ya Afrika ya Mashariki, John Konchellah walisema suala la kuzuiwa magari ni dogo, lakini wanataka kufumuliwa kwa mkataba wote wa Ushirikiano wa Utalii uliosainiwa mwaka 1985.
“Sisi Watanzania tulipinga kwa kuwa ajenda yetu ilikuwa ni moja, kwa nini magari ya Tanzania yamezuiwa kuingia JKIA na kama kuna matatizo basi ielezwe,” – Adelhelm Meru.
Kuvunjia kwa kikao hicho kumekuja siku chache baada ya Mamlaka ya Anga Tanzania (TCAA) kupunguza safari za ndege kutoka Kenya kuingia Tanzania kutoka 42 hadi 14 kwa wiki.
Mchumi kutoka Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Abel Maganga alisema uamuzi huo utakuwa na changamoto kwa kipindi kifupi kwa watalii ambao tayari walishalipia tiketi za safari kuja nchini na kuongeza kuwa endapo hali hiyo itaendelea kwa muda mrefu, itakuwa na athari kwa Tanzania kwa kuwa sekta ya utalii ndiyo inayoliingizia taifa fedha nyingi za kigeni.