Kiungo mshambuliaji wa klabu ya Liverpool, Raheem Sterling amewachanganya mashabiki na viongozi wa timu hiyo baada ya wawakilishi wake kusema kuwa mchezaji huyo hatasaini mkataba mpya hadi hapo msimu utakapomalizika.
Ripoti zaidi nchini England zinasema kuwa Raheem amegoma kusaini mkataba mpya baada ya kutoridhishwa na kiwango cha fedha ambacho Liverpool imeahidi kumlipa kwa wiki ambapo inadaiwa kuwa klabu hii imetoa ofa ya paundi 100,000/= kwa wiki.
Taarifa kadhaa huko England na barani ulaya kwa jumla zimeendelea kumhusisha Sterling na mpango wa kuihama klabu yake ambayo ilimpa nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza akiwa na umri wa miaka 18 tu.
Real Madrid na Arsenal zimekuwa zikitajwa kuwa na mipango ya kumsajili kiungo huyo ambaye hadi sasa ametokea kuwa sehemu muhimu katika mipango ya kocha Brendan Rodgers.
Kitendo cha Sterling kugoma kusaini mkataba mpya kimepokewa kwa hisia hasi miongoni mwa mashabiki wa klabu hiyo na wachezaji wa zamani ambao wamejenga dhana ya kuwa wachezaji wa kizazi cha sasa wanaendeshwa na tamaa ya fedha na si mapenzi kwa timu zao na mchezo wa soka pamoja na heshima kwa mashabiki na historia ya klabu.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook