Mabingwa wa zamani wa England na ulaya, Liverpool wamesaini upya mkataba wa udhamini na benki ya Standard Chartered kwa miaka mitatu zaidi baada ya mkataba wa awali kufikia mwisho.
Liverpool na benki hiyo wamekuwa washirika kwa muda wa miaka mitano tangu waliposaini mkataba wa kwanza mwaka 2010 na chapa ya benki hiyo imekuwa kwenye jezi ya Liverpool kwa miaka mitano sasa.
Vipengele vya mkataba huo havijawekwa wazi lakini magazeti ya michezo ya kila siku nchini England yameripoti kuwa thamani halisi ya mkataba huo ni paundi milioni 20 kwa msimu na hii inamaanisha kuwa Liverpool italipwa jumla ya paundi milioni 60 kwa muda wote wa mkataba huo.
Taarifa hizi za kuongezwa kwa mkataba wa udhamini toka kwa Standard Chartered zitakuwa muziki masikioni mwa mashabiki wa klabu hiyo katika kipindi hiki ambapo kocha Brendan Rogers anapiga mahesabu ya kufanya usajili ili kuimarisha kikosi chake baada ya msimu ambao haujawa na mafanikio.