MTANZANIA
Sarafu mpya ya shilingi 500 inadaiwa kuhujumiwa na baadhi ya watu ambao huinunua kwa Sh 2,500 na baadaye kuiyeyusha kwa ajili ya kutengenezea mikufu ya fedha (silver).
Taarifa zinaeleza tangu sarafu hizo zilipotolewa kwa mara ya kwanza Oktoba mwaka jana, baadhi ya watu wamekuwa wakizikusanya na kuzifanya kuadimika mtaani.
Imeelezwa kuwa tangu kutolewa kwa sarafu hiyo imekuwa adimu mitaani jambo ambalo si kawaida kwa fedha mpya zinazoingizwa kwenye mzunguko kuadimika kwa kiwango hicho.
“Nimekutana na watu watatu wakitafuta sarafu ya Sh 500 kwa Sh 2,500 hadi 5,000, mwanzoni nilipuuza lakini baada ya kutulia na kufanya utafiti nimegundua kwamba kwanza hii sarafu imekuwa adimu na inatafutwa kwa udi na uvumba,” kilisema chanzo cha habari jijini Dar es Salaam.
Meneja Sarafu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Jovent Rushaka, alisema taarifa hizo wanazo na wanazifanyia kazi.
“Taarifa hizo tumezipata juzi na tunalifanyia kazi suala hilo, kwa sasa tunafanya uchunguzi zinakofanyiwa kazi, zinakouzwa ili tuweze kwenda katika maduka hayo na kufanya uchunguzi,” Rushaka.
Katika hatua hiyo, meneja huyo aliwataka Watanzania kwa yeyote atakayebaini sehemu zinakotengenezwa na kuuzwa atoe taarifa.
Alipoulizwa kuhusu aina ya madini iliyotengenezewa sarafu hiyo ya Sh 500, alisema imetengenezwa kwa madini ya chuma kwa asilimia 94.
“Asilimia sita iliyobaki imetengenezwa kwa madini aina ya nickel plated silver ambayo kidogo unaweza kutengenezea mikufu ya ‘silver’. Sasa ni mtu gani anayenunua madini ya chuma ni vigumu kuwezekana sasa, maswali ya kujiuliza ni je, imetengenezwa na hiyo nickel plated silver?” alihoji Rushaka.
Alipoulizwa sababu za sarafu hiyo kuadimika imetokana na nini, alisema BoT ilitoa sarafu hiyo tangu Oktoba mwaka jana na kwamba bado wanazo nyingi.
Pia aliongeza kuwa Nickel sio miongoni mwa madini maarufu kwa ajili ya kutengeneza vidani vya thamani.
HABARILEO
Serikali imewasilisha mwelekeo wa bajeti kwa Kamati ya Bunge, ambayo inalenga zaidi kupeleka umeme na huduma za maji vijijini, kumalizia miradi ambayo haijakamilika na kutenga fedha kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum alisema wanaandaa bajeti ambayo itasaidia kumaliza mambo yote waliyoahidi, ambayo yameainishwa kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambayo serikali iliahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.
“Bajeti ya mwaka 2015/16 ni ya kipekee. Ni mwaka wa uchaguzi, ni mwaka ambao serikali ya Awamu ya Nne inamaliza muda wake na serikali mpya kuingia madarakani. “Ni mwaka ambao Mkukuta na Mpango wa Kwanza wa Maendeleo ya Milenia ya miaka mitano inafikia tamati, Malengo ya Milenia ya mwaka 2015 yanafikia ukomo na pia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010 unakamilika,” alisema.
Akiwasilisha mwelekeo wa bajeti hiyo kwa wabunge jijini Dar es Salaam jana, Mkuya alisema bajeti ya mwaka huu imejikita zaidi kutathmini na kuangalia changamoto kwenye sekta ya maji, nishati, rasilimaliwatu na kumalizia miradi ambayo haijakamilika.
“Vipaumbele kwenye bajeti hii vimejikita zaidi kwenye kuandaa awamu ya pili ya Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano utakaoanza Juni mwaka 2016, na mkazo zaidi ni kwenye miradi ya umeme vijijini, maji vijijini, kuimarisha rasilimaliwatu na kugharamia uchaguzi mkuu,”Mkuya.
Akifafanua, alisema katika mwelekeo huo wa Bajeti mpya ya mwaka 2015/16, jumla ya Sh takribani trilioni 23 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika matumizi ya maendeleo na ya kawaida.
Alisema katika matumizi ya maendeleo,vipaumbele vitano ambavyo vimetajwa hapo juu (maji, umeme, rasilimaliwatu, kumalizia miradi viporo na kugharamia uchaguzi mkuu). Jumla ya fedha zilizotengwa ni Sh trilioni 5.8.
HABARILEO
Mwanafunzi wa Kidato cha Pili, Jofrey Robert Mwakatenya anatuhumiwa kuuawa kikatili na baba yake mzazi, Robert Mwakatenya baada ya kumkuta akiwa na barua ya mapenzi, inayodaiwa aliandikiwa na rafiki wake wa kike.
Mzazi huyo ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa eneo la Majengo ‘D’ Manispaa ya Sumbawanga, anadaiwa kumwadhibu mwanafunzi huyo, ambaye ni mtoto wake wa kwanza kwa kumpiga ngumi na mateke mfululizo kwa zaidi ya saa tatu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa , Jacob Mwaruanda alithibitisha tukio hilo, lilitokea usiku wa kuamkia Jumapili iliyopita. Alisema bado wanamtafuta mtuhumiwa huyo kwani baada ya kufanya kitendo hicho alitokomea.
Mwenyekiti wa Serikali Majengo D, Antony Nyambo alidai kuwa mzazi huyo alikuwa na tabia ya kumwadhibu mwanawe huyo, akimtuhumu kuwa ni mtoro wa shule .
“Nilitaarifiwa juu ya kisa hiki Jumapili saa mbili asubuhi baada ya kutoka katika ibada na raia mwema, ndipo niliamua kufika nyumbani kwa marehemu, nilimkuta akiwa amelazwa chumbani, nilipomfunua niliona akiwa ametapakaa vumbi mwili mzima huku akiwa amevaa nguo ya ndani tu,”
Inadaiwa kuwa usiku huo wa tukio, mtuhumiwa alianza kumwadhibu kumpiga ngumi na mateke kuanzia saa mbili usiku hadi usiku wa manane.
Mtoto huyo baada ya kupata kipigo hicho, alizimia ambapo baba yake alimwagia maji mwilini hadi akazinduka, kisha akamwamuru alale chumbani humo pamoja na mdogo wake.
Mzazi wa mtoto huyo alidamka alfajiri na kwenda kwenye chumba walicholala watoto hao na kugundua kuwa Jofrey alikuwa mfu.
“Ndipo baba huyo alipoaga nyumbani hapo, akidai kuwa anaenda kutafuta gari ili Jofrey aweze kupelekwa hospitalini kwa matibabu. Mzazi huyo hakurudi tena nyumbani kwake hadi sasa,” .
MWANANCHI
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema endapo vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) vitashindwa kuafikiana katika kuachiana baadhi ya majimbo kabla ya Uchaguzi Mkuu, watawaeleza wananchi kwa kuwa ndiyo kiini cha kuanzishwa kwa umoja huo.
Dk Slaa alisema hayo jana kabla ya kumalizika kwa vikao vya wakuu wa Ukawa ambao wamekubaliana kusimamisha mgombea mmoja kuanzia ngazi ya urais, ubunge na udiwani na kwa siku mbili kuanzia juzi, walikuwa wakijadili ufanikishwaji wa azimio hilo.
Dk Slaa alisema hadi sasa wameshakubaliana kuachiana asilimia 95 ya majimbo yote na kwamba ana matumaini watafanikisha, lakini akaonya kuwa ikishindikana, hawatasita kuwaeleza wananchi.
Mkoani Dar es Salaam, Ukawa imeshafikia muafaka katika majimbo mawili ya Kawe na Ubungo na kubakiza majimbo sita, wakati majimbo matano ya mikoa mingine bado yanaupasua kichwa umoja huo wa vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD.
“ Ukawa ilikuwa ni ombi la Watanzania, ni sauti yao kwa hivyo taarifa zinazoendelea kutolewa siyo sahihi,” alisema akirejea habari kuwa Ukawa, iliyoanzishwa wakati wa Bunge la Katiba inaelekea kusambaratika kutokana na kushindwa kuafikiana kwenye baadhi ya majimbo.
“Kama ikitokea tumeshindwa kufikia makubaliano mwisho wa safari yetu, hakuna kitakachokuwa siri, tutawaeleza Watanzania,” Dk Slaa.
Hata hivyo, alisema mpaka sasa hakuna dalili zozote za umoja huo kushindwa kuafikiana kwa sababu ya mvutano wa majimbo hayo, kwani mpaka sasa wameshafanikiwa kuyagawana kwa asilimia 95 nchini kote.
Habari za ndani kutoka katika vikao hivyo zinaeleza kuwa uliibuka mvutano mkali kuhusu mgawanyo wa majimbo 17 yaliyobaki mpaka sasa.
MWANANCHI
Siasa za uchaguzi zinaonekana kuingia kwenye ukamilishwaji wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) kutokana na Serikali kuhaha kutaka uzinduliwe kabla Rais Jakaya Kikwete hajaondoka madarakani.
Siasa hizo zimeibuka baada ya kuahirishwa tena kwa tarehe ya kuanza kazi kwa mradi huo hadi Septemba. Mradi huo, unaogharimu Sh419.08 bilioni, ulitakiwa uwe umeshaanza kutoa huduma ya usafiri kati ya Kimara na Kivukoni.
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli jana alizitaka mamlaka zinazosimamia ujenzi wa mradi huo kuukamilisha haraka huku akitwisha mzigo kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Kasi (DARTS) kuharakisha ununuzi wa mabasi ili yaanze kutumia asilimia 75 iliyokamilika ya mradi huo.
Dk Magufuli aliuagiza Wakala wa Barabara (TANROADS) kumalizia matengenezo madogo ya barabara zilizokamilika za Kimara-Kivukoni na Morocco -Magomeni na kuzikabidhi kwa Darts na Tamisemi kwa ajili ya utoaji wa huduma ya usafiri ambayo sasa imekuwa kero kutokana na barabara nyingi kufungwa kupisha mradi huo.
Waziri pia alimtaka mkandarasi wa mradi huo, Strabag kufanya kazi usiku na mchana kukamilisha kipande cha barabara kati ya Fire na Kamata ifikapo Agosti mwaka huu ili kutoa mwanya kwa Rais Jakaya Kikwete kuuzindua.
“Lile eneo lililokamilika wakabidhiwe Tamisemi waanze kutumia, liwe ni jukumu lao kutafuta mabasi haraka kwa sababu kazi yetu ni kujenga, kazi ya kutafuta mabasi hayo ni ya wengine… wakiamua zipite daladala, bajaji au baiskeli sisi hatutalalamika,” Dk Magufuli.
Alimtaka ofisa mtendaji mkuu wa Darts, Asteria Mlambo kuharakisha mchakato wa kununua mabasi ili barabara isikae bila kutumika kwa kuwa imekamilika.
“Hakuna haja ya kusubiri barabara ya Fire ikamilike wakati asilimia 75 imeshakamilika. Tuna mpango wa kumwomba mheshimiwa Rais afungue sehemu iliyokamilika ili hata kama ile iliyobaki ikichelewa Rais atakayekuja naye ajidai nayo,” alisema Dk Magufuli huku akishangiliwa.
Mradi wa BRT umekuwa ukiahirishwa mara kwa mara kutokana na kusuasua kwa mchakato wa ununuzi wa mabasi rasmi kwa ajili ya barabara hizo, ujenzi wa baadhi ya vituo ambavyo makandarasi walishindwa kazi na migogoro ya ardhi.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale alisema mradi umekamilika kwa asilimia 90 na unatarajiwa kumalizwa Novemba na kwamba asilimia 75 iliyokamilika ipo tayari kutumika muda wowote.
MWANANCHI
Wakati Serikali imetangaza mapendekezo ya mfumo wa mapato na matumizi yake kwa mwaka 2015/16 yenye vipaumbele vinne, baadhi ya wabunge, akiwamo Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Dk Festus Limbu wameiponda wakisema haikuwashirikisha wadau katika uandaaji na kwamba haina kipya.
Waziri wa Fedha Saada Mkuya alitaja moja ya vipaumbele hivyo vinne kuwa ni Uchaguzi Mkuu, ambao awali alisema haungekuwamo kwenye bajeti ya 2015/16 kwa kuwa fedha kwa ajili ya shughuli hiyo zilishatengwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha unaomalizika.
Vipaumbele vingine ni kuweka msukumo kwenye miradi ya umeme vijijini na maji vijijini na kuimarisha rasilimali watu.
Lakini Dk Limbu alisema Serikali haikuwashirikisha wadau katika uandaaji wa bajeti hiyo ya Sh22.4 trilioni, wala kamati yake kabla ya kuja na mapendekezo hayo.
“Sisemi kwamba kazi yao ni mbaya. Wamejifungia kule wakakamilisha kazi ndiyo wakaileta. Kwa mara ya kwanza mimi kama mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti nimeikuta hii ‘figure’ ya Sh22.4 trilioni humu, nataka nieleze masikitiko yangu,” alisema Dk Limbu.
Mwenyekiti huyo alisema Serikali ilipaswa kuwashirikisha ili kujaribu kupunguza mjadala mkali bungeni na kwenye kamati.
Akiwasilisha mapendekezo ya bajeti hiyo jana, Waziri Mkuya alisema Serikali imepanga kutumia Sh22.4 trilioni katika bajeti ya mwaka 2015/16 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo ikiwa ni ongezeko la asilimia 15 ya bajeti iliyopita iliyokuwa Sh19.8 trilioni.
Kati ya fedha hizo, matumizi ya kawaida ni Sh16.7 trilioni na matumizi ya maendeleo ni Sh5.7 trilioni, sawa na asilimia 25.9 ya bajeti yote.
Alisema jumla ya mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh 14.8 trilioni sawa na asilimia 57.8 ya bajeti yote. Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya Sh13.3 trilioni sawa na asilimia 90.1 ya mapato ya ndani.
Alisema mapato yasiyo ya kodi yatakuwa Sh949.2 bilioni na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri yatakuwa Sh521.9 bilioni.
Aliongeza kuwa washirika wa maendeleo wanatarajia kuchangia Sh1.8 trilioni katika bajeti sawa na asilimia 8.4 ya bajeti ikilinganishwa na asilimia 14.8 ya bajeti ya mwaka 2014/15.
Mkuya alisema Serikali ilipanga kutumia Sh5 trilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika bajeti iliyopita, lakini hadi kufikia Machi, mwaka huu ilikuwa imetoa Sh2.4 trilioni tu.
NIPASHE
Machafuko ya kisiasa yanayoendelea Burundi, yamesababisha mamia ya raia wa nchi hiyo kukimbilia Tanzania kama wakimbizi.
Raia hao walianza kuingia nchini jana kwa ajili ya kutafuta hifadhi mkoani Kigoma
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilithibitisha kuingia kwa wakimbizi zaidi ya 200.
Msemaji wa wizara hiyo, Isaack Nantanga, alisema kuwa wakimbizi hao waliingia mkoani Kigoma kupitia vijiji vya Kagunga, Kakonko, Kijaje na Chakeoya.
Nantanga alisema kuwa baada ya wakimbizi yao kuingia katika maeneo hayo, maofisa wa Idara ya Uhamiaji walikuwa wanaendelea na taratibu za kawaida za kuwapokea wakimbizi.
Mmoja wa maofisa Uhamiaji ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa maelezo kuwa siyo msemaji, alisema kuwa wakimbizi 150 kutoka Burundi waliingia mkoani humo na walikuwa katika kijiji cha Kagunga, wilaya ya Kigoma Vijijini.
Alisema kuwa maofisa wa Idara ya Uhamiaji waliondoka jana kwenda Kagunga kuwachukua wakimbizi hao kwa boti na kuwapeleka katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu kwa ajili ya kuwahifadhi.
Alisema kuwa watakaa kambini hapo hadi hali ya utulivu itakaporejea nchini Burundi.
Burundi imekumbwa na ghasia kutokana na maandamano yanayofanyika katika mji mkuu, Bujumbura na wafuasi wa vyama vya upinzani wanaopinga hatua ya Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza, kutaka kugombea tena urais, baada ya kumaliza muda wake wa mihula miwili.
NIPASHE
Jumuiya na Taasisi za Kiisalam nchini, imetoa tamko na kuipa serikali siku 15 kabla ya kufanya maandamano nchi nzima kuelekea Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, wakidai kufunguliwa kwa madrasa zilizofungiwa kwa kuhusishwa na kutoa mafunzo ya ugaidi.
Masharti mengine ni kuachiliwa huru au kwa dhamana masheikh na maimamu waliokamatwa wakituhumiwa kutoa mafunzo na mazoezi ya kigaidi.
Maeneo ambayo madrasa hizo zaidi ya 10 zimefungwa ni katika mikoa ya Kilimajaro, Dodoma na Mtwara.
Tamko hilo pia lilisema jeshi hilo linawatuhumu kwa kukusanya watoto na kuwafundisha elimu ya dini katika mazingira yasiyofaa na kuwapo kwa taarifa za watu wenye milipuko misikitini na kujihusisha na ugaidi.
Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Sheikh Musa Kundecha, alisema jeshi hilo limekuwa likiwakamata watu hao usiku na kuwapeleka katika vituo vya polisi, na kuwahoji.
Alisema jeshi hilo limekuwa likifanya kazi za maofisa wa ustawi wa jamii na elimu, kufanya ukaguzi katika maeneo ambayo watoto hao wanafundishwa elimu ya dini ya kiislamu.
“Mkakati wa operesheni hii unakiuka utu, haki za binadamu, kikatiba na ni uchochezi dhidi ya Waislamu kuwafanya wachukiwe na jamii, tunawatunza yatima katika maeneo jirani na madrasa na kuwapa elimu ya kidini siyo kosa, tunatimiza wajibu wa kidini. Wajibu wa serikali ni kutulinda, lakini tunawekwa katika mazingira ya hatari,” alisema Kundecha.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isaac Nantanga, alisema ulifanikiwa utafiti, kabla ya jeshi hilo kuchukua hatua za kufunga baadhi ya madrasa na kuwakamata watu hao.
“Katika maeneo ya mikoa hiyo ni kweli kuna suala hilo, na watoto ambao wana umri wa kuwa shule walikutwa pale, hivyo tukataka kufahamu na yajulikane mafunzo wanayopewa,” alisema Nantanga.
Alisema kuendelea kushikiliwa kwa baadhi ya watu waliokamatwa na kunyimwa dhamana kunatokana na jeshi hilo kutojiridhisha au kutokamilika kwa taratibu za dhamana.
NIPASHE
Serikali imesema wafanyabiashara kugomea matumizi ya mashine za kielektoniki za ulipaji kodi (EFD’s), ni miongoni mwa sababu zilizokwamisha utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2014/15
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, aliyasema hayo jana wakati akiwasilisha mapendekezo ya mfumo wa mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka 2015/16, jana jijini Dar es Salaam.
Mwaka jana taifa lilikuwa na mgomo wa wafanyabiashara nchi nzima, wakigomea mshine hizo kwa kile walichoeleza bei zinazouzwa, mfumo uliotengenezwa unamfanya mfanyabiashara asione faida bali mauzo ya siku.
Mara kwa mara walikuwa na mazungumzo na serikali, lakini hawakufikia muafaka, na hadi sasa wachache ndiyo wanaotumia mashine hizo.
Mwanzoni mwaka huu, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini, Jonson Minja, alikamatwa na polisi na kupelekwa mkoani Dodoma kwa kile kinachodaiwa alikwenda kufanya mkutano wa kuhamasisha wafanyabiashara wa mkoa huo wasitumie mashine hizo.
Baada ya kukamatwa wafanyabiashara waliendesha mgomo wa siku tatu wakilitaka jeshi la Polisi kueleza aliko kiongozi.
Waziri Mkuya alizitaja changamoto nyingine za kibajeti kuwa ni serikali kulazimika kutoa fedha kwa mashirika ya umma ya kibiashara kama Shirika la Ndege (ATCL), Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), ambazo ziliongeza gharama ambazo zingepaswa kulipwa na mashirika yenyewe.
Nyingine ni mchakato mrefu wa kupata mikopo ya kibiashara.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter,Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.