Kiungo mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania Mrisho Khalfan Ngassa amesaini mkataba wa miaka minne kuichezea timu ya Freestate Stars inayoshiriki ligi kuu ya soka nchini Afrika Kusini maarufu kama PSL .
Ngassa amesaini mkataba huo siku chache baada ya kuisaidia klabu yake aliyoitumikia kwa muda mrefu ya Dar es salaam Young Africans kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya soka Tanzania bara .
Ngassa amekuwa akisakwa na timu hii ya Afrika Kusini kwa muda mrefu ambapo iliwahi kutuma ofa ya kumsajili tangu msimu uliopita lakini Yanga waliikataa ofa hiyo kwa sababu ilikuwa ndogo .
Mrisho Ngassa amekuwa akisakwa na timu nyingi za nje ambazo zimevutiwa na uwezo wake na kwa nyakati tofauti ofa kadhaa zimewahi kutumwa kwenye klabu ya Yanga kwa ajili yake .
Klabu za Al Mareikh ya Sudan pamoja na Seattle Sounders ya Marekani zimewahi kumtaka Ngassa na Sounders wamewahi kumpa nafasi ya kufanya majaribio katika mchezo dhidi ya Manchester United miaka kadhaa iliyopita .
Ngassa huenda akaungana na mchezaji mwenzie wa Yanga na timu ya taifa Simon Msuva ambaye hivi karibuni alifanya majaribio na klabu ya Bidvest Wits na kama timu hiyo ikiridhishwa na kiwango chake huenda akasaini mkataba .