Klabu ya Azam Fc iko mbioni kumrudisha kocha wake wa zamani Stewart Hall baada ya kumalizana na aliyekuwa kocha wa muda ndani ya klabu hiyo George Nsimbe aliyepewa nafasi ya kuiongoza timu hiyo kwa muda baada ya kufukuzwa kazi kwa Joseph Omog .
Nsimbe alipewa mkataba kama kocha mkuu wa muda mpaka mwishoni mwa msimu wakati timu hiyo itakapofanya maamuzi mengine na tetesi mbalimbali zimemtaja Stewart kama mtu ambaye atakuja kuichukua nafasi hiyo .
Stewart atakuwa anarudi Azam Fc kwa mara ya tatu baada ya kuifundisha timu hiyo vipindi viwili mfululizo hapo awali kabla ya kufukuzwa kazi katikati ya msimu uliopita baada ya kushindwa kuelewana nauongozi wa klabu hiyo .
Azam fc iliamua kumfukuza kazi kocha wake mkuu Joseph Omog baada ya timu hiyo kutolewa kwenye michuano ya ligi ya mabingwa katika mchezo dhidi ya Al Mareikh ya Sudan ambapo Azam ilifungwa 4-0.
Omog alifukuzwa kazi pamoja na msaidizi wake Ibrahim Sikanda kabla ya Nsimbe ambaye alikuwa sehemu ya benchi la ufundi hajapewa kazi ya ukocha wa muda akisaidiwa na kocha wa zamani wa Ndanda Fc Denis Kitambi .
Azam ilijikuta ikishindwa kutetea ubingwa wake wa ligi kuu ya Tanzania bara baada ya kupitwa na Yanga kwenye mzunguko wa pili wa ligi na hadi mwisho wake ilimaliza kwenye nafasi ya pili .