MWANANCHI
Mkuu wa Wilaya ya Rombo Lembris Kipuyo amesema tatizo la ulevi kupindukia Wilayani humo limewaathiri wanaume kiafya na kuwataka watendaji kulivalia njuga.
Kutokana na ulevi huo kuna madai kwamba baadhi ya wanawake wanaoishi kwenye ndoa wamelazimika kutafuta wanaume nchi jirani ya Kenya ili wapate mimba kutokana na wanaume zao kuzidiwa na ulevi hivyo kushindwa kuwahudumia.
Kipuyo alisema tatizo la ulevi limefikia hatua ya hatari zaidi na jitihada za haraka zinahitajika.
Kipuyo alitaja maeneo yaliyokithiri kwa ulevi ni kilelewa ambapo ni mpakani mwa Tanzania na Kenya.
“Imefikia mahali wanaume wengi wanashindwa kumudu kufanya tendo la ndoa na kuwalazimu wanawake zao kukodi wanaume kutoka nchi jirani ya Kenya kwa ajili ya tendo hilo”Kapuya.
Alisema ni vizuri mamlaka husika na Serikali ya vijiji kuhakikisha ulevi unakwisha ili kuepuka Wilaya hiyo kuwa na kizazi cha Wakenya.
MWANANCHI
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaona wafanyakazi wanane wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wanaokabiliwa na tuhuma za kughushi vyeti na kutoa hati za uongo wana kesi ya kujibu.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi, Nyigulile Mwaseba baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi wanane wa upande wa mashtaka pamoja na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo.
Baada ya Hakimu Mwaseba kutoa uamuzi huo, alisema Juni 17 na 18, 2015, washtakiwa hao ambao wanadaiwa kuwa ni watoto wa vigogo wa Serikali wataanza kutoa ushahidi wa utetezi dhidi ya mashtaka yanayowakabili.
Wafanyakazi hao ni Justina Mungai, Christina Ntemi, Siamini Kombakono, Janeth Mahenge, Beatha Massawe, Jacquiline Juma, Philimina Mutagurwa na Amina Mwinchumu.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kughushi vyeti vya kuhitimu kidato cha nne na kutoa hati za uongo kwa mwajiri wao, BoT.
Washtakiwa Mungai, Massawe na Mwinchumu, wanadaiwa kughushi vyeti hivyo mwaka 2001, wakati Ntemi, Kombakono, Mahenge na Mutagurwa wanadaiwa kughushi vyeti hivyo mwaka 2002.
Wanadaiwa kughushi vyeti vya kuhitimu kidato cha nne na kutoa BoT hati za uongo wakionyesha kuwa vimetolewa na Baraza la Mitihani la Taifa wakati siyo kweli. Washtakiwa hao ambao awali waliyakana mashtaka, wako nje kwa dhamana.
MWANANCHI
Mawaziri wawili wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kutoka CUF na wabunge wengine wakongwe wa chama hicho wamepigwa mwereka kwenye kura za maoni za kutafuta wagombea wa nafasi za uwakilishi na ubunge kwa majimbo 50 ya Zanzibar.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa uchaguzi wa CUF, Omary Ali Shehe alisema matokeo hayo ni ya awali.
Walioangushwa ni waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu, Haji Faki Shaali ambaye ameangushwa katika Jimbo la Mkanyageni, sambamba na mbunge wa jimbo hilo, Mohamed Habib Mnyaa na Naibu Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati, Haji Mwadini Makame katika nafasi ya uwakilishi katika jimbo la Nungwi.
Kwa mujibu wa matokeo ya awali, kura hizo zimewatupa waandishi wa habari waliokuwa wamejitokeza kuwania nafasi mbalimbali akiwamo mtangazaji mkongwe wa BBC, Ally Saleh ‘Alberto’ ambaye ameangushwa na mbunge wa sasa wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ibrahim Mohamed Sanya.
Wengine ni Talib Ussi Hamad wa Mwananchi aliyepata kura 31 katika nafasi ya ubunge Jimbo la Magogoni na kutanguliwa na Juma Kombo Hamad aliyepata kura 106 huku mbunge anayemaliza muda wake Kombo Khamis Kombo akiambulia kura 61.
Mwandishi wa Majira, Mwajuma Juma alishika nafasi ya pili, baada ya kupata kura 11 akiwania nafasi ya uwakilishi jimbo la Amani, ambapo Khamis Rashid Abeid aliibuka kidedea kwa kura 22, huku mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima, Maua Mohamed Mussa akishika mkia katika nafasi aliyokuwa akiwania ya ubunge wa viti maalumu, Wilaya ya Mjini.
Mtangazaji wa zamani wa Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ), Najma Khalfan Juma alipata pigo mara mbili baada ya kuanguka katika kura za maoni nafasi ya uwakilishi jimbo la Ziwani na nafasi ya ubunge viti maalumu kupitia Wilaya ya Chakechake, Pemba.
Kwa upande wa uwakilishi wa viti maalumu Wilaya ya Mjini, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Ferej amepenya kwenye tundu la sindano kwa ushindi wa kura moja, baada ya kupata kura 91, akifuatiwa na Nunuu Salim Rashid aliyepata kura 90 na mtoto wa mbunge wa Mji Mkongwe, Rahma Ibrahim Sanya aliyepata kura 30 huku kura nne zikiharibika.
NIPASHE
Watoto wawili ambao ni ndugu wamefariki dunia katika kanisa la ufufuo na uzima, linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima jijini Dar es salaam.
Watoto hao walifariki baada ya kupigwa na shoti ya umeme wakiwa katika ibada juzi jumapili wakati watoto hao wakiwa na waumini wengine wakifuatilia ibada ya kufunga ndoa.
Inadaiwa kuwa watoto hao walipigwa na shoti baada ya kukanyaga nyaya za umeme wakati waumini waliponyanyuka kwenda kuwapokea maharusi wakati wakiingia kanisani hapo.
Baba mzazi wa watoto hao David Oturo ameonyesha hali ya wasiwasi ya kutokukubaliana na mazingira ya vifo vya watoto wake Sara mwenye miaka 10 na Gudluck mwenye miaka minne na kusema ni vifo vya utatanishi.
Alisema siku hiyo kulikuwepo na watoto wengi waliokusanyika katika viwanja vya kanisa hilo lakini ni watoto wake waliofikwa na mauti hayo.
Aliongeza kuwa kabla ya kufikwa na mauti hayo majira ya mchana Sara aling’atwa na nyuki sehemu ya mguu ambao walitokea katika kanisa hilo gafla.
Alisema jioni ndipo watoto hao walipopigwa na shoti na baada ya kuangalia nyaya hizo hazikuwa zimechunika sehemu yoyote wala kuwa na dalili ya hitilafu.
NIPASHE
Wakimbizi wapato 20 wamefariki dunia Mkoani Kigoma kutokana na ugonjwa wa kuharisha na kutapika huku wengine 40 wakilazwa katika hospitali ya Mkoa huo ya Maweni.
Mganga mkuu wa Mkoa Dk.Leonard Subi alisema kati ya waliofariki dunia Warundi ni 18 na wawili ni Watanzania wa kijiji cha Kagunga na waliolazwa ni wakimbizi wa Burundi.
Alieleza kuwa katika kambi ndogo iliyowekwa katika kambi ndogo ya Lake Tanganyika wamelazwa wakimbiza 73 wakati wengine 87 wakiwa wamelazwa katika kambi ya Nyarugusu.
Dk.Subi aliwataka wananchi wa Mkoa huo kuzingatia kanuni za afya kwa kuchemsha maji ya kunywa na kunawa mikono kwa sababu wakati wa kutoka chooni na kuacha tabia ya kula chakula bila kunawa mikono kwa sabuni ili kuepuka magonjwa hayo.
JAMBOLEO
Wanajeshi wa jeshi la kujenga Taifa JKT Ramadhani Hamis anadaiwa kuua mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Salum Omary mkazi wa Mikwanjuni Tanga.
Omary anadaiwa kuuawa kwa kupigwa ngumi ya mgongo na mwanajeshi huyo wakati akisimamia mchakato wa uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa baada ya kutokea hali ya sintofahamu miongoni mwao.
Tukio hilo lilitokea baada ya kutokea ubishani kati ya mama mmoja na askari huyo ndipo marehemu alipojaribu kuamua ugomvi huo ndipo mwanajeshi huyo alipompiga ngumi na kumsababishia kifo.
Kamanda wa Polisi Tanga Zuberi Mwombeki alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema baada ya kupigwa alikimbizwa kwenye kituo cha afya kilichokuwa karibu lakini jitihada za kuokoa maisha yake zilishindikana kutokana na kupata maumivu makali yaliyosababisha kifo chake.
Kwa sasa Mwanajeshi huyo anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za mauaji na anasubiri kukamilika kwa uchunguzi ili kufikishwa mahakamani.
HABARILEO
Kukosekana kwa Sheria ya kutenganisha biashara na uongozi ili kuweka nidhamu kwa viongozi wa umma kumesababisha kuwepo na mmomonyoko mkubwa wa maadili kwa viongozi hao, ambao wamekuwa wakitumia ofisi za umma kwa maslahi binafsi, hivyo kufanya vitendo vya rushwa kukithiri.
Wakichangia mjadala wa hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma bungeni jana, wabunge mbalimbali walisema ukosefu wa sheria hiyo umesababisha kuwepo kwa mianya mingi ya rushwa inayofanywa na baadhi ya watumishi wa umma.
Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Manyoni Mashariki, John Chiligati (CCM) alisema hivi sasa kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili na baadhi ya viongozi wa umma hutumia ofisi za umma kwa maslahi binafsi.
“Kuna mmomonyoko mkubwa kwa viongozi wa umma, na jambo hili lilianza kwenda mrama baada ya kuruhusu viongozi wa umma kufanya biashara, rushwa nayo imeshamiri na utajiri wa ajabu kwa viongozi wetu,” Chiligati.
Mapendekezo ya marekebisho ya kubadili Sheria ya kutenganisha biashara na uongozi kwa mujibu wa Sekretarieti ya Maadili, ilisema inafanya kwanza utafiti kabla ya kutoa mapendekezo ya kuibadili hatua ambayo hadi sasa bado mwafaka wake haujafikiwa.
Akizungumzia rushwa, Chiligati alisema ni jambo la kushangaza kuona kiongozi wa umma ambaye mshahara wake unajulikana, lakini mali alizonazo ni nyingi na hakuna aliyechukua hatua za kuwahoji.
“Hili la rushwa ndio baya, mnafahamu mshahara wa mtumishi wa umma, lakini mali alizonazo ni nyingi kuliko kipato chake, ana maghorofa kedekede, kwa nini hamjamhoji?”Chiligati.
Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine (CCM), alisema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inabidi ipewe meno zaidi ili iweze kuyatumia kikamilifu kupambana na rushwa nchini.
Aliongeza kuwa, wala rushwa nchini ni tatizo kubwa na ndio wanaokwamisha maendeleo ya nchi kwa kujinufaisha wao, na kutaka sheria kali itungwe kuwabana na ikiwezekana, watoa rushwa na wala rushwa wauawe kwa kupigwa risasi.
“Hili la rushwa ni baya, na ni tatizo kubwa nchini itungwe sheria kali itakayowabana watoa na wala rushwa na ikiwezekana wapigwe risasi, Takukuru ipewe meno iwe na nguvu ya kuwafikisha watuhumiwa hao mahakamani na sio kusubiri kibali cha Mwendesha Mashataka wa Serikali (DPP),” Nyangwine.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.