Spika wa Bunge Anne Makinda amesema bangi inayolimwa katika Mkoa wa Njombe si kali kama inayolimwa Mikoa mingine kutokana na baridi kali iliyopo Mkoani humo.
Makinda alijikuta akitoa jibu hilo huku akicheka kutokana na swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa viti maalum Christowaja Mtinda ambaye alisema kuna maeneo nchini ukiwemo Mkoa wa Njombe mmea wa Bangi umekua ukiota bila kupandwa na hutumika kama chakula.
“Njombe bangi haioti yenyewe, tulikuwa tunapanda, lakini hata hivyo bangi ya njombe si kali kwa sababu ya baridi” Makinda.
Akijibu kwa niaba ya Waziri wa afya, Juma Nkamia alisema Serikali haipo tayari kuhalalisha matumizi ya bangi kama dawa kwa sababu athari zake ni nyingi kuliko faida.
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete amewaaga rasmi mabalozi 36 wa Tanzania katika mataifa mbalimbali akiwaeleza kuwa hatakuwa madarakani baada ya Oktoba.
Rais aliwaaga mabalozi hao jana wakati akifungua mkutano wa siku tatu utakaohitimishwa leo, ambao pamoja na mambo mengine, utajadili ‘Diplomasia ya Tanzania Kuelekea Dira ya Taifa 2025.’
“Huu ni mkutano wangu wa mwisho kuzungumza nanyi. Mmenisaidia vizuri katika kipindi chote cha utawala wangu na niwaahidi tu kuwa nitaondoka Ikulu baada ya uchaguzi mkuu ujao,” Rais Kikwete.
Pamoja na kuaga, aliwaachia mambo manne ya kuzingatia ili kuifanya Tanzania iendelee kuheshimika kimataifa.
Mambo hayo yanajumuisha; kuwasaidia wawekezaji wa Kitanzania kupata fursa katika nchi wanazoziwakilisha; kuwasaidia Watanzania walioko katika nchi wanakowakilisha kuunda umoja wao; kuzishawishi asasi za kiraia za kimataifa kuja kuwekeza nchini pamoja na kutengeneza marafiki wa Taifa kwa ujumla.
Rais alieleza kuwa wakati Serikali ikitekeleza mpango wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo 2025, tayari kuna wananchi wenye uwezo wa kiuchumi ambao wameshaanza kuwekeza katika baadhi ya nchi Afrika na hata nchi za Magharibi, hivyo ni vyema wakapewa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha azma zao.
“Niwakumbushe tu kuwa mahitaji yamebadilika nanyi pia badilikeni. Kwa sasa ni vyema vipaumbele vyenu vikawa uwezo wa kuleta mitaji nchini, kiasi cha misaada ya maendeleo mlichochangia, masoko kwa bidhaa zetu mliyoyabainisha na wawekezaji wa nje mliowashawishi kuja kuwekeza,”
“Achaneni na ripoti zenu za kila mwisho wa mwezi mnazoleta za malalamiko mara eeeh wanataka mabadiliko kwenye cyber crime (Sheria ya Makosa ya Mtandaoni) au Sheria ya Takwimu. Hayo masharti wanayotoa ndiyo maana ilifikia hatua nikasema kuwa kama hatuwezi kupata mikopo bila masharti ni bora tusipewe tu.”
Rais pia aliwataka mabalozi hao kuzihoji serikali za nchi waliko juu ya mchango wao katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo athari zake zinaziathiri sana nchi zinazoendelea kama Tanzania.
Aliongeza kuwa aliingia madarakani nchi ikiwa haina adui na anaondoka nchi ikiwa hivyo pia na kuwakumbusha kuwa ni vyema kila mmoja akajitahidi katika hilo.
MWANANCHI
Siku kadhaa tangu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete kuwatahadharisha wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC), ya chama hicho kwamba wanapaswa kumteua mgombea wa urais anayekubalika ndani na nje ya chama hicho, Chama cha Wananchi (CUF), kimesema kauli hiyo haina ukweli.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema hakuna mtu anayefaa kuwa Rais ndani ya CCM, kwa kuwa mfumo wa chama hicho hauruhusu uadilifu.
Profesa Lipumba alisema hayo jana alipokuwa akihutubia wakazi wa Kijiji cha Kayombo wilayani Nzega.
Alisema ndani ya CCM, kuna tatizo la kimfumo ambalo hata akitokea mtu mwadilifu akawa rais, bado atavurugwa na mfumo uliopo na kuwa fisadi.
“CCM kimekosa mfumo wa uadilifu hivyo hakiwezi kutuletea kiongozi wa nchi, kwani hata akitokea mtu mwadilifu akashinda, bado atavurugwa na mfumo huo wa kifisadi,” Lipumba.
Profesa Lipumba ambaye yuko mkoani Tabora kwa ziara ya kuhamasisha wananchi wajiandikishe kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura, alisema kwa hali ilivyo, Tanzania inahitaji Rais mwadilifu ambaye kimsingi, hawezi kutokea CCM.
Alisema uongozi wa CCM hauthamini dira ya Taifa na tatizo hilo ndilo linalofanya wananchi wawe na maisha magumu kwa kukosa uhakika wa matibabu, elimu bora na chakula.
Profesa Lipumba alisema wananchi hawapati matibabu ya uhakika kwa kuwa zahanati na hospitali hazina dawa. Lakini hayo yakiendelea, viongozi wanakwenda kutibiwa nje ya nchi.
Aliwataka wananchi kutambua kuwa uchaguzi ndiyo fursa ya kuitoa CCM madarakani na kwamba hawawezi kupiga kura kama hawajajiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura
MWANANCHI
Chama cha Wamiliki wa vyombo vya Habari Tanzania (MOAT) kimeunda timu maalumu itakayokwenda bungeni Dodoma kuwashawishi wabunge wasiupitishe muswada wa sheria wa vyombo vya habari baada ya kubaini umejaa kasoro.
Muswada huo ulioandaliwa na Serikali na ulitakiwa kuwasilishwa katika kikao kilichopita kwa hati ya dharura jambo ambalo halikuwezekana baada ya kupingwa na wadau na baadhi ya wabunge.
Hata hivyo, muswada huo uliorejeshwa kwa wadau kujadiliwa, unatarajiwa kupelekwa kwa mara nyingine katika kikao cha Bajeti kinachoendelea ingawa si kawaida kwa Bunge la Bajeti kujadili miswada ya sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Moat, Reginald Mengi alisema baada ya kuusoma, wamegundua kuwa kuna kasoro nyingi na miongoni mwake ni adhabu kwa waandishi wa habari ambazo zitawafanya wawe waoga katika kufanya kazi yao.
Alisema wadau wa habari na wataalamu wa sekta hiyo wataendelea kuwaelewesha wabunge juu ya masuala mbalimbali yaliyomo katika muswada huo ili hata wanapoupitia wawe na uelewa wa kutosha wa kitu wanachotaka kukipitisha kuwa sheria rasmi.
Alisema licha ya kasoro hizo, pia kuna hila za kuupitisha kwa haraka kusudi wasitoe mawazo yao juu ya vipengele kadhaa ambavyo vinafinya uhuru wa vyombo vya habari na hata uhuru wa wananchi kupata habari.
“Wanasiasa hawa walitumia sana vyombo vyetu vya habari wakati wakitafuta kura na sasa wameshapata uongozi wanatuona hatufai badala yake wanataka kutukandamiza kwa kutuwekea sheria nzito,” Mengi.
“Huu muswada ukipita, utakuwa ni sheria mbovu ambayo haina manufaa kwa nchi yetu, pia Watanzania watakosa habari za uhakika kwani ikiwa kila ufikapo muda wa taarifa ya habari saa 2.00 usiku wote wanalazimika kutazama Televisheni ya Taifa, sasa hii ndiyo nini?” alihoji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Ltd, Francis Nanai alisema ni vyema magazeti yakatumia nafasi iliyopo kuandika makala maalumu kila siku kuhusu muswada huo ili wananchi wajue matatizo yake.
NIPASHE
Kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) ya Mkoa wa Dar es Salaam, imekubali mapendekezo ya kuongeza majimbo ya uchaguzi katika mkoa huo kutoka saba ya awali hadi kufikia 13.
Kikao kilichofikia makubaliano hayo kilifikiwa licha ya mvutano kutoka kwa wabunge wa upinzani ambao walipinga mapendekezo ya kuongezeka kwa majimbo hayo.
Kwa upande wa Halmsahuri ya Temeke, majimbo mapya yaliyopendekezwa kuongezeka ni Mbagala, na Kijichi na kufikia jumla ya majimbo manne kwa kujumuisha majimbo ya sasa ya Kigamboni na Temeke.
Akifungua kikao hicho Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, alisema wamefanya mapendekezo hayo ili kuwasilisha kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ambayo ratiba yake inataka mwisho wa kuwasilisha mapendekezo hayo kuwa Mei 31, mwaka huu.
Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, Halmashauri ya Kinondoni majimbo mapya yaliyopendekezwa kuongezeka ni Kibamba na Bunju na hivyo kufikia majimbo matano ukiongeza na ya zamani ya Ubungo, Kawe na Kinondoni.
Katika Halmashauri ya Ilala, jimbo moja ndilo lilipendekezwa kuongezeka na kufikia jumla ya majimbo manne pamoja na ya zamani ya Segerea, Ilala na Ukonga.
Pamoja na Kamati kukubali mapendekezo hayo, Wabunge wa Upinzani hawakukubaliana na maamuzi hayo na kusema kwamba wanapanga kupeleka maombi mbadala kwa Nec ya kutokubaliana na utaratibu huo ndani ya mwezi huu.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alitoa wito kwa Watanzania na wadau wengine wasiokubaliana na utaratibu huo wa kuongeza majimbo, kupeleka mapendekezo yao mbadala kwa Tume ili wakati inafanya maamuzi ifanye kwa kuzingatia matakwa ya Watanzania.
“Sioni sababu ya kuongeza majimbo kwa kuwa kama Serikali ingekuwa na nia ya kuleta maendeleo ingeongeza Halmashauri na si majimbo, wanataka kutumia mwanya wa kuongeza majimbo ili kutatua mgogoro uliopo ndani ya Chama Cha Mapindizi (CCM) wa kugombania majimbo kwa hiyo wanajua wakiongeza kila mmoja atakuwa amepata,” Mnyika
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, alisema ni vema tume ikagawa majimbo hayo kwa kuzingatia kama upo uwezo wa kuyamudu majimbo hayo na sio kuangalia tu wingi wa watu na kuanza kugawa bila kutafakari na kupima uwezo wake.
NIPASHE
Nyota ya Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa, imeendelea kung’aa baada ya Taasisi ya Samunge Social Sciences Research Center (SSSRC), kufanya utafiti na kubaini kuwa kiongozi huyo ni chaguo la kwanza kwa wananchi.
Utafiti huo uliofanywa miaka miwili kuanzia 2013 hadi 2015, unaonyesha Lowassa anaongoza kwa asilimia 20.7 dhidi ya wagombea 31.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mtafiti Mkuu wa SSSRC, George Nyaronga, alisema utafiti huo waliufanya kwa kutumia madodoso pamoja na mahojiano kwenye mikoa 18.
Utafiti huo na asilimia walizopata wanasiasa wengine kwenye mabano ni Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema, Dk. Willbrod Slaa asilimia 11.7; Waziri wa Ujenzi, John Magufuli (7.6); Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (7); Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba (4.8); Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba (4.2) na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe 3.4 sawa na Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (2.4) na Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia (1.2).
Alisema pia utafiti huo ulionyesha kuwa Lowassa pekee ndiye anayekubalika na wapiga kura wengi, karibia idadi sawa ya jinsia zote mbili, wanaume 50 na wanawake 49.
Kwa ujumla, Lowassa na vinara wengine 10 wanaotajwa kuwania urais walipata asilimia 67.2, huku asilimia zilizobaki (32.8) zikitwaliwa na wagombea wengine 10 kati ya 20 waliohusishwa katika utafiti huo.
Aidha, Nyaronga alisema hawakuwa na dodoso linaloorodhesha majina ya wanaopendekezwa kuwa Rais ila majina yalitajwa na wajaza madodoso wenyewe kisha wao wakajaza majina kwenye SSSRC.
Kwa mujibu wa dodoso lenye kichwa cha habari cha katika tafiti kuhusu uchaguzi wa mwaka 2015, takwimu zinaonyesha kuwa Watanzania wanamtaka mtu mwenye kufanya maamuzi magumu.
NIPASHE
Kashfa ya Escrow imeibuliwa upya bungeni baada ya wabunge kudai kuna kampuni ya Simba Trust inayomiliki asilimia 50 za kampuni ya Pan Africa Power (PAP), ambayo inadaiwa kuhusika katika ufisadi wa uchotwaji wa zaidi ya Sh.bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Hayo yaliibuliwa jana bungeni na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wakati wa kuwasilisha hotuba yake ya kambi hiyo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka 2015/2016 ya Wizara ya Viwanda na Biashara.
Msemaji wa kambi hiyo, Mbunge wa Ole (CUF), Rajab Mbarouk Mohamed, alisema wakati umma wa Watanzania unataka kuelewa wamiliki wa kampuni ya Simba Trust lakini katika hali ya kushangaza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), umegoma kutoa majina ya wamiliki wa kampuni hiyo.
“Kambi rasmi ya upinzani tunaitaka serikali ieleze kwanini taasisi hii ya Brela iliyo chini ya wizara hii bado inakataa kutoa majina ya wamiliki wa Simba Trust, imekuwa kama ilivyokuwa makampuni yaliyohusika na uchotaji mabilioni ya Epa na fedha za mradi wa Meremeta,” alisema.
Mnyaa alisema hatua ya Brela kukataa kutoa majina ya wamiliki wa kampuni hiyo kuna unganisha na dhana kwamba wamiliki wa kampuni hiyo ni viongozi wandamizi wa serikali ya CCM.
Alisema matatizo ya kiutawala yaliyopo katika sekta ya umma nchini yamesababisha sekta ya viwanda kushindwa kujiendesha kiushindani.
Aliongeza kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa la na Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), limebainisha kuwa viwanda vingi vinaendeshwa kwa hasara kutokana na kuwapo kwa gharama kubwa za uzalishaji, tija ndogo, riba kubwa za kibenki,tatizo la umeme na urasimu.
Mnyaa alisema licha ya kwamba Shirika la Viwango Tanzania (TBS), lipo lakini takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania inaongoza kwa kuwa na bidhaa feki kwa ukanda mzima wa kusini na mashariki mwa Bara la Afrika.
Awali Dk. Kigoda alisema serikali imeandaa utaratibu ambao utawezesha kuwapatia wafanyabishara wadogo maarufu wamachinga leseni maalum ili watambuliwe na kuondokana na adha ya kunyanyaswa katika maeneo wanayofanyia biashara zao
Dk. Kigoda alisema moja ya mikakati ya wizara katika kipindi cha 2015/2016 ni pamoja na kufufua viwanda vilivyobinafsishwa ambavyo havifanyi kazi kikamilifu kikiwamo kiwanda cha matairi cha General Tyre cha jijini Arusha na kiwanda cha nguo Urafiki.
MTANZANIA
Kundi la wana mgambo wa Al Shabaab la Somalia, linadaiwa kuwaua polisi 25 wa Kenya jana baada ya kuvamia magari ya polisi katika eneo la Yumbis wilayani Fafi, Kaunti ya Garissa.
Hadi jana jioni, hakukuwa na taarifa inayoeleza waliko polisi walionusurika baada ya shambulio hilo la kushtukiza.
Taarifa zilizochapishwa na gazeti la Daily Nation, zilisema maofisa watatu walionusurika shambulio hilo walisema magari manne ya polisi yaliteketezwa na wanamgambo hao.
Maofisa hao walikuwa kwenye msafara huowakielekea Yumbis saa chache tu baada ya wenzao wengine kujeruhiwa kwenye shambulio la Jumatatu alasiri.
Katika shambulio la kwanza, maofisa watatu walijeruhiwa baada ya gari lao kukanyaga bomu lililotegwa na wanamgambo hao.
Mwakilishi wa Kata ya Jarajila, Mahat Osman alisema maofisa hao walikuwa wakienda Yumbis wakati gari lao lilipokanyaga bomu katika eneo la Yarey.
Alisema waliojeruhiwa walipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Garissa.
Mkuu wa Wilaya ya Fafi, Geoffrey Taragon alisema hali za askari hao ni mbaya.
Mashambulio dhidi ya askari hao wa Kenya yalitokea ikiwa ni wiki moja tu baada ya Al- Shabaab kuvamia Kijiji cha Yumbis na vingine jirani na kuwahutubia wakazi wake msikitini kwa saa kadha bila mamlaka za usalama za Kenya kujua kilichokuwa kinaendelea.
Kundi hilo lenye uhusiano na mtandao wa ugaidi wa al Qaeda, lilisema liliwashambulia polisi kilomita 70 kaskazini mwa Garissa, mji ambao wanamgambo hao walivamia Chuo Kikuu cha Garisa na kuua watu 148 wengi wao wakiwa wanafunzi, Aprili mwaka huu.
Wanamgambo hao wanaopigania kuiangusha Serikali ya Somalia inayoungwa mkono na nchi za magharibi, wameanzisha mashambulio mengi ndani ya ardhi ya Kenya wakijaribu kuilazimisha iondoe askari wake Somalia.
Mashambulio hayo yamesababisha Serikali ya Kenya izidi kubanwa iondoe askari wake Somalia lakini imeapa kuendelea na operesheni yake sambamba na majeshi mengine ya kulinda amani ya Umoja wa Afrika (AU) nchini humo.
Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta imeendelea na msimamo huo licha ya watu kuendelea kuuawa nchini Kenya kwa mashambulio ya wanamgambo hao huku sekta ya utalii, ambayo ni miongoni mwa vyanzo vyake vikuu vya fedha za kigeni ikiporomoka.
Katika tukio la jana, Jeshi la Polisi lilisema ni askari mmoja tu aliyeuawa katika mashambulio hayo ya Fafi na Yumbis na mwingine alijeruhiwa vibaya, huku watatu wakiwa na majeraha madogo.
“Kundi la maofisa lililopelekwa kuongeza nguvu wakati lilipowasili eneo la tukio lilijikuta likishambuliwa kwa kushtukizwa,” Mkuu wa Jeshi la Polisi, Joseph Boinnet.
MTANZANIA
Uozo na ufisadi ulioigubika Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) uliwekwa hadharani bungeni mjini Dodoma jana. Hayo yalielezwa katika hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Mawasiliano,Sayansi na Teknolojia.
Alisema utata katika umiliki na ukodishaji wa hisa za serikali, mikataba mibovu, madeni na baadhi ya vitu vilivyochangia kampuni hiyo kufilisika.
Akisoma maoni hayo, Mohamed Habib Mnyaa alisema Serikali ilikodisha hisa 35 za TTCL kwa Kampuni ya Mobile System International (MSI) ya Uholanzi na kulipwa Sh bilioni 111 au asilimia 17.5.
Hata hivyo, alisema MSI hawakulipa fedha yote kwa wakati,lakini Serikali ikawapa kibali cha kuongoza Kampuni ya TTCL. “Kambi ya upinzani, inaitaka Serikali iwaeleze Watanzania ni kwa vipi hisa zinaweza kukodishwa badala ya kuuzwa na kununuliwa? Haya ni maajabu katika tasnia ya uchumi na uhasibu.
“Pia tuelezwe inakuwaje mwenye hisa asilimia 35 anakuwa na uwezo wa kuendesha kampuni wakati mwenye asilimia 65 asiwe na nafasi hiyo?” Mnyaa.
Mnyaa ambaye pia ni Mbunge wa Mkanyageni (CUF), alisema hivi sasa kuna mvutano mkali baina ya Serikali na Kampuni ya simu za mkononi ya Bharti Airtel kuhusu hatima ya asilimia 35 ya hisa ambazo kampuni hiyo inazimiliki ndani ya TTCL.
Akinukuu kauli ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk. Kamugisha Kazaura kwa Kamati ya Bunge, Mnyaa alisema kutokana na hasara kubwa ya Sh bilioni 334.5 mpaka kufikia mwaka 2013 na kushindwa kukopesheka huku ikibaki na mtaji wa hasi wa Sh bilioni 87.9, kwa sasa ni mufilisi.
Alisema hali hiyoimechangiwa na mbia mwenye hisa kwa asilimia 35 kutofanya uwekezaji mkubwa tangu ubia uanze mwaka 2001, jambo ambalo limesababisha uchakavu wa miundombinu na kupungua kwa ubora wa huduma.
“Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Patrick Makungu alisema Baraza la Mawaziri limeunda jopo la majadiliano na mwekezaji huyo kuzungumzia gharama za kumlipa aweze kuondoka TTCL na kwamba hakuna taarifa kuhusu fedha zilizotajwa.
Alisema hata njia za simu 800,100 walizoahidi hawakuzijenga badala yake zile walizozikuta 270,000 walizipunguza na kufikia 158,000 tu.
HABARILEO
Serikali imewashauri wananchi kutotumia mifuko ya plastiki na vifungashio vyake kuwekea au kuhifadhia chakula cha moto, kutokana na madhara makubwa ya kiafya, yanayoweza kutokea kwao.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Stephen Masele alitoa hadhari hiyo jana bungeni na kutaka jamii itumie vifungashio vya glasi, chuma isiyoshika kutu na vyombo vingine vya asili, kama vile vibuyu.
Hadhari hiyo ya serikali imekuja wakati ambao wakazi wengi, hususani wa mijini, hutumia mifuko hiyo kuhifadhia vyakula mbalimbali vinavyoandaliwa haraka na zaidi, ikiwa viazi vya kukaanga maarufu kama chipsi.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri, madhara yanayoweza kusababishwa na uwekaji wa chakula cha moto katika mifuko ya plastiki ni kuwepo kwa uwezekano wa kemikali, zilizotumika kutengeneza mifuko hiyo kuingia kwenye chakula na kukifanya kuwa na sumu.
Sumu hiyo inaweza kusababisha saratani, kuharibu ukuaji wa mfumo wa uzazi hususani kwa watoto ambao hawajazaliwa, mabadiliko ya kijenetiki, matatizo ya kushindwa kuona, uyeyushaji wa chakula tumboni kuwa taabu au kutokamilika na ini kushindwa kufanyakazi vizuri.
Magonjwa mengine ni pamoja na kuharibika kwa mfumo wa utendaji wa figo na magonjwa yanayohusiana na mfumo wa kupumulia.
Naibu Waziri alisema hayo akijibu swali la mbunge wa viti maalumu, Mkiwa Adam Kimwanga (Chadema) aliyetaka kupata kauli ya serikali kuhusu mifuko ya plastiki na uchafuzi wa mazingira na madhara yanayoweza kusababishwa na uwekaji wa chakula katika mifuko hiyo.
Masele ambaye pia alijibu swali la nyongeza kutoka kwa mbunge wa viti maalumu, Christowaja Mtinda (Chadema) aliyetaka kufahamu ni lini serikali itafunga viwanda vya plastiki, aliwataka wananchi kushiriki kupiga vita mifuko hiyo watu wasiitengeneze au kuingiza nchini kinyemela.
Naibu Waziri huyo alisema serikali inatambua kuwepo kwa uchafuzi wa mazingira, unaotokana na matumizi ya mifuko ya plastiki nchini.
Alitaka kila mwananchi mwenye taarifa ya mahali inapotengenezwa mifuko hiyo midogo, ambayo tayari serikali na viwanda nchini, walishakubaliana kutotengenezwa, aitoe.
Alisema mifuko hiyo laini, yenye unene wa chini ya maikroni 30, ilishapigwa marufuku na akataka wananchi kuachana nayo kutokana na madhara yake kiafya.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.