Majambazi yamemuua polisi wa upelelezi, William Mtika (29) wa jijini hapa wakati wa mapambano kwenye tukio la kutaka kupora fedha za Kampuni ya Export And Trading eneo la Iwambi.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 9:00 alasiri na katika mapigano hayo, jambazi mmoja alipigwa risasi mguuni na baadaye kufariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi.
Akizungumza wakati wa kuaga mwili wa marehemu huyo, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ahmed Msangi alisema Mtika akiwa na askari wenzake walipata taarifa za watu waliotiliwa shaka nyendo zao eneo hilo ndipo wakaelekea kwenye tukio.
“Askari wakiwa eneo la tukio walifanikiwa kuwakamata majambazi waliokuwa kwenye pikipiki baada ya kugonga gari la Polisi kabla ya nyingine kutokea na kuwapiga risasi ambazo moja ilimpata askari wetu Mtika,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Nyerembe Mnasa aliwataka polisi kutorudi nyuma katika mapambano, huku akiwasisitiza wananchi kutoa taarifa za watu wanaowatilia shaka katika maeneo yao.
Mwili wa marehemu Mtika uliagwa jana mchana nyumbani kwake eneo la Ghana Mbeya na kusafirishwa kwenda mkoani Mara kwa ajili ya mazishi.Alisema polisi pia walifanikiwa kukamata bastola moja iliyotengenezwa kienyeji inayotumia risasi za Shotgun na pikipiki mbili.
Akifafanua chanzo cha tukio alisema, awali majambazi walimvamia mfanyakazi wa kampuni aitwaye Madhu Basavaranjappa lakini alipiga risasi juu ambazo ziliwafanya nao wajibu na hatimaye kuamua kukimbia na ndipo walipokutana na polisi.
Kamanda Msangi alisema wanaendelea na msako mkali wa kuwatia nguvuni majambazi hao huku akisisitiza kwamba kifo cha polisi wake katu hakitawavunja moyo polisi bali kitaongeza morali kuhakikisha wanapambana na aina yoyote ya uhalifu.
MWANANCHI
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, Jumapili atachukua fomu ya kugombea urais ndani ya chama hicho na atawaeleza Watanzania sababu ya kuwania nafasi hiyo.
Akizungumza jana, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa chama hicho, Shaweji Mketo alisema, Profesa Lipumba ndiye mgombea pekee wa urais aliyetangaza nia ya kuwania nafasi hiyo.
Alisema muda wa kutangaza nia kwa wagombea urais kupitia chama hicho ulianza Mei 10 hadi Juni 10, mwaka huu.
“Kalenda yetu inaonyesha muda wa mwisho wa kutangaza nia ilikuwa juzi na aliyefanya hivyo ni Profesa Lipumba pekee yake,” alisema.
Alisema muda wa kuchukua fomu kwa nafasi ya urais kupitia chama hicho ulianza jana na utakamika Juni 14, mwaka huu.
“Mkutano huo utakaoonyeshwa moja kwa moja kupitia runinga,” alisema.
Mketo alisema vikao vya Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho vitaanza Julai 11 hadi Julai 12, mwaka huu ili kumpitisha mgombea urais, wabunge na madiwani.
“Wagombea watakaopitishwa na Baraza watasubiri vikao vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vitakavyotoa mgombea mmoja katika nafasi ya urais, ubunge na udiwani,” alisema.
Kama Ukawa itamteua Profesa Lipumba ambaye kitaalamu ni mchumi itakuwa ni mara ya tano kuwania nafasi ya urais.
Akizungumzia nafasi za ubunge, Mketo alisema kati ya majimbo 189 ya Tanzania Bara, wamepata wagombea kwenye majimbo 133.
Alisema majimbo 56 bado hayajapata wagombea na kuwataka wafuasi wa chama hicho wenye sifa kuwania. Mkurugenzi huyo alisema, bado mchakato wa kura za maoni kwa nafasi za ubunge na udiwani zinaendelea katika kanda mbalimbali.
MWANANCHI
Mkazi wa Kijiji cha Mpandapanda Kata ya Kiwira wilayani Rungwe, anahojiwa na vyombo vya usalama kwa tuhuma za kujiandikisha mara mbili katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Rungwe, Veronica Kessy alisema jana kuwa tayari suala hilo limefikishwa katika vyombo vya sheria.
“Suala hilo kweli lipo lakini siwezi kuzungumza chochote kwani tulishalifikisha kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na linafanyiwa kazi,” alisema Kessy.
Kwa mujibu wa mitandao, mtuhumiwa alikamatwa akiwa na vitambulisho viwili vilivyotolewa kwenye vituo viwili tofauti katika Kijiji cha Mpandapanda.
Kitambulisho cha kwanza kinataja jina la Veklene B. Mwankenja kikionyesha alizaliwa Aprili 26, 1993 alichokipata katika Kituo cha Shule ya Msingi Kiwira A, akiwa amevalia shati la mistari. Lakini kitambulisho cha pili kina jina la Vekline B. Mwankenja akiwa amezaliwa Julai 26, 1996 akiwa amevaa shati na sweta, alichokipata katika Kituo cha Shule ya Msingi Kiwira B.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema kijana huyo alikamatwa na kupelekwa kwenye vyombo vya sheria.
“Alishakamatwa na amefikishwa mahakamani kwa kosa hilo,” alisema Kamanda Msangi.
Baadhi ya wakazi wa Kiwira walipoulizwa kuhusu kijana huyo alipo kwa sasa, walidai kuwa hawajamuona licha ya kusikia taarifa za kukamatwa kwake.
“Huyu mtu hatujamuona tangu atuhumiwe kwa kosa hilo,” alisema mkazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Kijalo.
MWANANCHI
Polisi Mkoa wa Morogoro inawashikilia madereva 15 wa bodaboda kwa tuhuma za kufanya vurugu katika eneo la Fire zilizosababishwa na mmoja wao kumdhalilisha askari mmoja wa kike.
Ofisa Habari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji katika Kituo cha Fire, Issa Isandekeku alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa tatu asubuhi.
Alisema kabla ya vurugu hizo, dereva wa pikipiki alifanya kitendo hicho kwa askari aliyekuwa akielekea kazini muda huo.
Isandekeku ambaye pia ni Mkaguzi Msaidizi wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, alisema baada ya dereva kufanya kitendo hicho alikimbia, lakini alikamatwa.
Alisema muda mfupi baadaye kulizuka vurugu zilizoanzishwa na waendesha pikipiki wakipinga mwenzao kukamatwa, huku wakirundika mawe na taka katika Barabara ya Mindu, Kata ya Kingo.
Isendekeku alisema hali hiyo ilisababisha shughuli mbalimbali za wananchi kusimama kwa zaidi ya saa moja kutokana na kuhofiwa kujeruhiwa katika tukio hilo.
“Hizi vurugu zimesababishwa na waendesha pikipiki ambao waliweka vizuizi barabarani ili raia wasipite. Lakini muda huo mwenzao alikuwa ameshakamatwa. Tena alimdhalilisha askari akiwa na sare za kazi, hali ambayo ni kinyume cha sheria,” alisema Isendekeku.
Alisema baada ya askari wa zimamoto kuzidiwa nguvu, walitoa taarifa polisi ambao walidhibiti vurugu eneo hilo na kurejea utulivu.
Alisema katika vurugu hizo, polisi Rajabu Seleman alijeruhiwa kichwani kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali.
Kaimu Kamanda wa Polisi, Mussa Maramba alisema mbali na watu hao kukamatwa pia wanazishikilia pikipiki tano zilizotelekezwa katika vurugu hizo.
Kamanda Maramba alisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili baada ya uchunguzi kukamilika.
“Vurugu hizi ukiangalia hazikuwa na sababu ya msingi… sasa sijui hao madereva walifanya fujo kwa masilahi ya nani ?” alihoji Kamanda Maramba.
MTANZANIA
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Steven Masele, ametangaza kumuunga mkono Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa katika harakati zake za kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Masele aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini kabla ya Baraza la Mawaziri kuvunjwa, jana aliibukia katika mkutano wa kutafuta wadhamini wa Lowassa uliofanyika mjini Shinyanga na kusema sasa kada huyo wa CCM anasubiri kupitishwa na vikao vya chama.
Akizungumza katika mkutano huo, Masele ambaye pia ni mbunge wa Shinyanga Mjini, alisema yeye pamoja na wana CCM wenzake wanasubiri Kamati Kuu ya CCM ifanye kazi yake kisha wamalizie kumpitisha Lowassa.
“Tanzania yote inajua,” alisema Masele na kuuliza “inajua haijui…?” huku akijibiwa na wana CCM, “Inajuaaa…”
“Tanzania inajua na dunia nzima inajua kwamba Lowassa yuko hapa. Mimi ni mjumbe wa Mkutano Mkuu, wa NEC wetu wamesema hapa, sisi tumekaa mkao wa kula tunasubiri wafanye kazi yao na sisi tunamalizia kupiga bao tu,” alisema Masele.
Mbali na Masele, mawaziri wengine walioonyesha kumuunga mkono Lowassa kwa nyakati tofauti ni pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na watoto, Sophia Simba na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Nyerere aliyemsindikiza kuchukua fomu mjini Dodoma.
Katika mkutano huo, alikuwapo pia Mbunge wa Msalala ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige ambaye alimsifia Lowassa kwa utendaji bora alipokuwa Waziri Mkuu na hasa kuwaletea maji wakazi wa Mkoa wa Shinyanga.
“Sisi wananchi wa Mkoa wa Shinyanga tuna imani na wewe kwa jambo moja ulilotufanyia. Ulileta maji kutoka Ziwa Victoria. Shinyanga ilikuwa jangwa, lakini ulileta maji, sisi watu wazima tuliona kwa macho,” alisema Maige.
Naye Mwenyekiti mstaafu wa Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita, alisema Lowassa ni miongoni mwa viongozi walioandaliwa tangu enzi za Mwalimu Nyerere.
“Kuna wakati chama kiliwaandaa vijana wake kwa kuwapeleka chuo kikuu ili wawe viongozi wa baadaye, akiwamo Rais Jakaya Kikwete, Lowassa na wengineo nawahifadhi. Sasa umefika wakati wa Lowassa…,” alisema Guninita.
Katika mkutano huo, Lowassa alivunja rekodi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa kupata wanachama 7,014 waliojitokeza kumdhamini.
Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga, Charles Sangula, alisema kati ya wanachama hao, 3,221 walitoka katika wilaya yake, 2,610 Kishapu na 1,183 Kahama.
Naye Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Kanali Maulid aliwataka makada wa chama hicho kutochafuana kwa kashfa wakati huu wa uchaguzi, na kuchagua mtu anayekubalika ndani na nje ya chama.
“Tumchague mtu anayekubalika ndani na nje ya chama chetu. Lowassa anakubalika. Lakini wako baadhi ya makada wanaochukua fomu na kuanza kuwachafua wenzao. Nashukuru Lowassa hakufanya hivyo,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, alisema kulingana na matokeo ya utafiti uliofanywa na asasi yake ya Tanzana Mzalendo Foundation, Lowassa amekidhi vigezo vyote 10 vya uongozi bora.
“Tuna taasisi yetu ya Tanzania Mzalendo Foundation, tumeweka vigezo 10 na vyote Lowassa amepata asilimia 100. Baadhi ya vigezo hivyo ni uzalendo, uvumilivu na kuwa na uamuzi mgumu,” alisema Mgeja.
Akizungumza na wana CCM waliokusanyika katika ukumbi huo, Lowassa aliwashukuru na kurudia sababu yake ya kugombea urais.
“Nimerudi nyumbani kuwaambia kuwa nimeanza safari ya matumaini. Nilikuwa hapa mwaka 1977 hadi 78, mlinilea vizuri.
“Nimegombea kwa sababu nimechoshwa na umasikini. Mwaka 1962, Mwalimu Nyerere alitaja maadui watatu wa Tanzania kuwa ni ujinga, umasikini na maradhi. Lakini hadi leo kuna viongozi wa Tanzania wanajivunia umasikini. Kazi ya kiongozi ni kuwatoa watu kwenye umasikini na kuwapeleka kwenye utajiri,” alisema Lowassa.
Aliwataka pia wana CCM kujiandikisha ili wawe na sifa ya kupiga kura.
Lowassa aliingia Shinyanga saa sita mchana kwa ndege akiwa na msafara wake kisha wakaelekea kwenye ofisi ya CCM mkoa na baadaye ofisi ya wilaya.
NIPASHE
Wabunge wameikosoa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2015/16, wakisema haina jipya na haitekelezeki.
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzania bungeni, Freeman Mbowe, amesema bajeti ya serikali ya mwaka 2015/16 haina unafuu wowote kwa Mtanzania wa kawaida, bali bajeti iliyojaa maneno matamu ya kuhadaa umma.
“Ukipitia baadhi ya vifungu utabaini kuwa vina lengo la kutoa kauli nzuri za matumaini na ahadi zisizotekelezeka, ni bajeti ya kikampeni kwa ajili ya uchaguzi,” alisema na kuongeza:
“Wamedandia hoja ya Kambi ya Upinzani ya kutoa pensheni kwa wazee tangu bajeti 2012/13 na serikali ikasema jambo hili halitekelezeki, leo wanazungumza wataanzisha na hakuna sheria ya utekelezaji na haiko katika sheria zitakazoletwa bungeni, hakuna mzee atakayelipwa pensheni katika mwaka ujao wa fedha,” alisema.
Mbowe alisema ongezeko la kodi ya mafuta ni tishio kwa Mtanzania wa kawaida, kwani kila kitu kitapanda gharama kwa Sh. 100 kwa dizeli na petroli, huku mafuta ya taa ikiongezeka kwa Sh. 150, yataathiri wananchi na kuongeza gharama za maisha
Mbowe alisema katika soko la dunia bei ya mafuta inashuka kila siku, huku Tanzania ikiongeza badala ya kupungua.
Alisema Watanzania wanadanganywa tena kwa fedha za kodi ya mafuta zitakwenda kwenye mfuko wa Umeme Vijijini (Rea), kwani mwaka uliopita fedha zilizoingizwa kwenye mifuko maalum ni fedha zilizotakiwa zisitumike, lakini imezichomoa na kutumia kwa mambo mengine, hivyo siyo kweli kuwa zitatumika kwa umeme.
“Bajeti inaweza ikasomwa ikaonekana ni tamu, tatizo kubwa ni utekelezaji wa bajeti, Chama hiki (CCM) na serikali hii zimeshachoka, hakina uwezo wa kutekeleza bajeti, wamebakiza miezi minne waondoke Ikulu, watuachie sisi tuingie,” alisema na kuongeza:
“Inashangaza kuona bajeti inasomwa leo, lakini nusu ya mawaziri hawapo katika bajeti ya serikali yao, Naibu Waziri wa fedha anaingia wakati waziri anahitimisha bajeti…wabunge wa upinzani hususan wa Chadema wote wameacha majukumu yao kuja kusikiliza bajeti.”
Naye, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, alisema haoni kipya ndani ya bajeti hiyo kwa sababu kila kitu ni kile kile.
“Kwa kweli nilishindwa kufatilia kwa sababu ni maneno yale yale, ya watu wale wale ya siku zote na ya miaka yote…wakitaka fedha ni mafuta na bia, lakini safari hii hawakwenda kwenye maji ila yale yale tu,” alisema.
Kuhusu kupandisha kodi ya mafuta, alisema serikali haijawahi kufikiria vyanzo vipya vya mapato.
Alisema hakuna mji uliojengwa na kuwa chanzo kikubwa cha mapato kama Dar es Salaam kutokana na majengo makubwa yaliyojengwa.
“Hayo majengo ni chanzo kikubwa cha mapato nchi nyingi zinaingiza mapato kwa kutumia majengo makubwa yaliyojengwa,” alisema.
Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustino Mrema, alisema bajeti ya mwaka huu haina tofauti na mwaka jana kwani kila kitu ni kile kile hakuna jipya.
“Ni bora wangekaa wenyewe wakaipitisha, sisi (wabunge) tukabaki nyumbani, kwa sababu kila tunachopitisha hakitekelezeki,” alisema.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Esther Bulaya, alisema bajeti ya serikali haiwezi kumsaidia mwananchi wa kipato cha chini kutokana na kupandisha bei ya mafuta.
“Kwa kawaida mafuta yakipanda ni lazima kila kitu kitapanda bei, hivyo kuwepo kwa ongezeko la mafuta ni kuwafanya wananchi kuendelea kuwa maskini tofauti na ilivyokuwa ikikusudiwa kuwa uenda bajeti ingekuwa ya kuwasaidia wananchi wenye kipato cha chini,” alisema
Aidha, alisema inashangaza kuona kuwa fedha za matumizi zimekuwa nyingi huku fedha kwa ajili ya maendeleo zikipunguzwa.
Naye, Mbunge wa Kisesa (CCM), Luaga Mpina, ameibeza bajeti na kudai kuwa haina jambo lolote ambalo ni jipya kwani kila jambo linaonekana kuwa ni la kawaida.
Alisema serikali haikuwa na sababu ya kuongeza ongezeko katika mafuta kuwa ilikuwa na uwezo wa kutafuta vyanzo vingine vya mapato tofauti na kujielekeza katika mafuta.
Mpina alisema pamoja na serikali kudai kwamba wataweza kupeleka fedha za miradi katika wakala wa Umeme vijini, lakini kimsingi pesa hizo hazipelekwi.
Waziri Kivuli wa Fedha wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, James Mbatia, alisema:
“Ni bajeti ya kufurahisha wapiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kwa sababu upungufu huo unatokana na ongezeko la thamani ya Dola ya Marekani kuchupa kutoka Shilingi 1,650 kwa mwaka jana hadi Shilingi 2,054 kwa viwango vya wiki hii…Bajeti kwa ajili ya matumizi ya serikali ni kubwa kuliko Bajeti ya Maendeleo.”
Mbatia alisema bajeti ya mwaka huu, itawaumiza Watanzania kwa kuwa serikali imepandisha kwa kiwango cha juu mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa huku ikilenga kukopa zaidi ya shilingi trilioni sita na kuongeza kasi ya ukuaji wa deni la Taifa.
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji, Peter Msigwa, alisema bajeti hiyo ni ya kiini macho na haiwezi kutekelezeka kwa kuwa hata bajeti inayoishia Juni 30, mwaka huu imetekelezwa kwa asilimia 28 tu kutokana na wahisani wanaochangia bajeti ya Taifa kugoma.
“Tunasikitika bajeti hii itaiacha nchi ikiwa kapu tupu baada ya uchaguzi mkuu kumalizika. Wamekuja na bajeti ya makusudi kwa sababu wanafahamu wako kwenye kupindi cha mpito cha kukabidhi nchi kwa Ukawa…Hakuna muujiza utakaotokea na kuifanya bajeti iliyoletwa bungeni itekelezeke,”alisisitiza Msigwa.
FELIX MKOSAMALI
Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali, alisema bajeti iliyowasilishwa inalenga kuwafurahisha wasanii na si wananchi kwa kuwa ni bajeti ya maigizo kutokana na hofu ya kuanguka kwa chama tawala na si kupanua wigo wa maendeleo ya Watanzania.
NIPASHE
Serikali imetakiwa kupunguza vizuizi mipakani ili kurahisisha biashara na kuongeza kipato kwa wananchi waishio humo.
Wito huo ulitolewa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Abdulrahman Kinana (pichani), wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Misenyi ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya siku 10 mkoani Kagera.
Kinana ambaye alipokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa kijiji cha Mtukula mpakani mwa Tanzania na Uganda ya kutozwa kodi nyingi, alisema kuweka kodi nyingi mipakani ni kuongeza uingizaji na utoaji wa bidhaa kwa njia ya panya.
“Serikali itambue kuwa wananchi wa mipakani wanategemea kipato kutokana na biashara zinazoingia na kutoka nchini sasa kama wanaweka vizuizi zaidi ya vitano, kuna biashara itafanyika na mwananchi wa mipakani atafaidika vipi? Na ndiyo maana watu wanaamua kupitisha biashara zao kwa njia za panya,” alisema Kinana.
Alieleza kuwa Tanzania ni nchi pekee miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki inayopakana na nchi nane, hivyo ni vyema fursa hiyo ikatumika kuwanufaisha wananchi wa mipakani.
Kinana aliongeza kuwa asilimia 30 ya Watanzania wanaishi mipakani, hivyo wanapaswa kurahisishiwa mfumo wa biashara kwa kuwapunguzia kodi.
“Lazima serikali itambue namna nzuri ya kulinda mipaka yake, haiwezi ikalinda mipaka kwa kukusanya kodi nyingi ambazo zinageuka kuwa kero, watumie akili ya kukusanya na siyo mabavu na uonevu,” alisema Kinana.
Pia aliahidi kulifikisha suala hilo kwa ngazi husika kuanzia kwa waziri mwenye dhamana ili mipaka hiyo igeuke kuwa yenye manufaa kwa wananchi.
Kinana pia alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongela, kukaa na kamati ya ulinzi na usalama, kuona namna ya kupunguza kodi hizo kwa sababu ziko ndani ya uwezo wao.
NIPASHE
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, ambaye anawania uteuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea urais, ameahidi kuwa asipoteuliwa hatakuwa na kinyongo na atarejea kukijenga chama.
Aidha, ameahidi kuwa atalirudisha Jimbo la Iringa Mjini mikononi mwa CCM.
Jimbo hilo kwa sasa linaongozwa na Mchungaji Peter Msigwa, wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Kadhalika, Makamba amemwaga ahadi lukuki kwa wakazi wa mji wa Iringa ikiwamo kuwasaidia vijana wa bodaboda, kupanua uwanja wa ndege mkoani humo, kujenga barabara ya lami kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha pamoja na kufufua viwanda.
Ahadi nyingine ni pamoja na kuhakikisha vijana wanaojiunga na vyuo vikuu, wanapata mikopo bila usumbufu wowote kwa kuwa kupata elimu ni haki yao.
Aliyasema hayo jana alipozungumza na makada wa CCM, kutoka wilaya zote za mkoa wa Iringa, alipokuwa akitafuta wanachama wa kumdhamini.
Makamba alipata zaidi ya wadhamini 600 ambao ni zaidi ya idadi inayotakiwa na chama ambayo ni wanachama 30 kwa kila mkoa.
Aliongeza kuwa mchakato wa kumpata mgombea, hauna uhasama na kwamba hata kama kushinda ama kushindwa atakuwa mtu wa kwanza kuanza kukijenga chama upya ili kurudisha mshikamano.
“Mimi nitakuwa mtu wa kwanza kuanza kukijenga chama baada ya uchaguzi mkuu, wanachama wote wanatakiwa kukaa kama familia moja ili kujenga mshikamo pamoja na kujadili makovu ya uchaguzi,” alisema.
Makamba alisema ana imani kwamba CCM kitapitisha mgombea kwa kujiamini bila kuogopa kusambaratika na wala wanachama wasisikilize watu wanaojipitisha mitaani na kusema kwamba chama kitasambaratika baada ya uchaguzi.
Kabla ya kukutana na wanachama wa CCM katika ofisi za wilaya, Makamba alisema Iringa ni kama nyumbani kwao kwa kuwa aliwahi kuishi hapo wakati baba yake akifanya kazi mkoani humo.
Wakati wa mapokezi yake, vijana waendesha bodaboada waliongoza msafara wake, huku wakiimba nyimbo hadi katika ofisi za wilaya ambako alikabidhiwa majina ya makada waliomdhamini.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.