NIPASHE
Kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu mkoani Kigoma, imeelemewa baada ya idadi ya wakimbizi kutoka Burundi kuzidi kuongezeka hivyo kuzidi uwezo wake kama inavyotakiwa na sheria za Umoja wa Mataifa (UN).
Mkurugenzi Idara ya Wakimbizi, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Harrison Mseke, alisema bado wakimbizi wa Burundi hawajaanza kurudi nyumbani kwao bali hali imekuwa mbaya zaidi kutokana na idadi yao kuendelea kuongozeka.
Kwa mujibu wa Mseke, hadi sasa wakimbizi katika kambi hiyo kutoka Burundi, wamefikia 71,000 na ndani ya wiki moja iliyopita wameingia wakimbizi 10,000.
Alisema kwa sasa idadi ya wakimbizi wote kutoka Burundi na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), katika kambi hiyo ni takribani 100,000.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, idadi hiyo ni kubwa kupita kiasi kwani sheria za UN kupitia shirika lake la kuhudumia wakimbizi duniani (UNHCR) kambi moja inapaswa kuhudumia wakimbizi wasiozidi 50,000.
“Kuna tatizo kubwa la eneo la kuwaweka kwani wakimbizi wote kutoka Burundi na DRC, bado wanahifadhiwa katika kambi ya Nyarugusu. Kwa sheria za Umoja wa Mataifa, kambi moja inatakiwa kuwa na wakimbizi 50,000, lakini sasa wapo zaidi ya 100,000.
Mseke, alisema hadi sasa serikali inafanya utaratibu wa kujenga kambi nyingine ili kupunguza idadi hiyo na kuangalia uwezekano wa kuwatenganisha wakimbizi hao kutoka nchi hizo.
Ongezeko la wakimbizi kutoka Burundi, limechangiwa na vurugu za kisiasa zinazoendelea nchini humo baada ya Rais wake, Pierre Nkurunzinza, kutangaza kuwania urais kwa kipindi kingine cha tatu hivyo kudaiwa kukiuka katiba ya taifa hilo.
NIPASHE
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amelezea hofu yake juu ya kuwapo kwa fitina zinazofanywa na baadhi ya watu kwa nia ya kuwaharibia wengine katika mchakato unaoendelea wa makada 42 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaowania kuteuliwa kugombea nafasi ya urais kupitia chama hicho.
Pinda ambaye pia ni mmoja wa makada waliochukua fomu kutaka kuteuliwa kuwa wagombea wa urais wa CCM, alisema namna pekee ya kuwaepuka watu wanaofitinisha wenzao ni kutowaunga mkono.
Aidha, Pinda aliwataka pia watangaza nia wenzake watakaoshindwa katika kinyang’anyiro hicho kukubali matokeo na kumuunga mkono yeyote atayeibuka mshindi na pia kutambua kuwa ‘asiyekubali kushindwa si mshindani’.
Pinda aliyasema hayo wakati akihutubia kwenye viwanja vya Mashujaa mjini hapa wakati akifunga sherehe za maadhimisho ya wiki ya Serikali za Mitaa.
Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwapo kwa amani na utulivu nchini hata baada ya uchaguzi kumalizika, huku akiwaasa wanasiasa wote kujiepusha na vitendo vya fujo kwani hazina tija kwa taifa na kwamba siasa ni ushindani ambao kila mtu anatakiwa akubaliane na matokeo.
“Acheni kuweka chuki zisizo na tija, haitowasaidia. Acheni kutaka kuwafanyia fujo wale watakaokuwa wamekubalika katika ngazi mbalimbali kutuongoza, maana wengine kazi yao ni fitina tu na wanataka mambo yaende ovyo. Mzalendo wa kweli ni yule anayekubali, kama kura hazikutosha hazikutosha tu,”.
Alitoa wito pia kwa wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa wanasimamia vizuri uchaguzi mkuu pale mchakato utakapoanza. “Agizo langu kwa wakurugenzi, tunakwenda katika uchaguzi mkuu. Tusifanye mzaha na chaguzi hizi, hakikisheni mnasimamia vizuri kama sheria zinavyoelekeza na kama kanuni zinavyoelekeza,” aliongeza.
Mwenyekiti wa Jumuia ya Umoja wa Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi, alisema baadhi ya halmashauri nchini zimefanikiwa kupunguza tatizo la uhaba wa madawati kwa zaidi ya asilimia 80.
NIPASHE
Kwa mara nyingine tena Bunge lilichafuka jana na kulazimika kuahirishwa kwa muda baada ya wabunge wa upinzani kugomea nia ya kuruhusu miswada mitatu ya mafuta na gesi, kuingizwa bungeni na kujadiliwa kwa hati ya dharura.
Kikao hicho cha 41 kilishindwa kuendelea baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, pale Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alipoomba mwongozo baada ya kukabidhiwa orodha ya shughuli za jana, ambayo alisema imekiuka kanuni za Bunge kwa kuweka miswada mitatu kwa ajili ya majadiliano.
Miswada hiyo ni wa sheria ya Petroli, usimamizi wa mapato ya mafuta na gesi na wa sheria ya uwazi na uwajibikaji katika tasnia ya uchimbaji Tanzania; yote ya mwaka 2015.
Mnyika aliomba muongozo huo kwa kutumia kifungu cha 53(6), masharti ya uwasilishaji wa hoja kama hiyo bungeni, na kanuni ya 86 inayoeleza siku ambayo muswada uliokwisha kujadiliwa na kamati umepangwa kwenye orodha ya shughuli, Waziri, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mwenyekiti wa Kamati au Mbunge mwenye muswada husika atawasilisha hoja kwamba muswada wa sheria kusomwa mara ya pili.
“Kipindi cha uhai wa Bunge hili na miswada iliyowahi kuja, hoja ikishatolewa ni lazima ijadiliwe iamuliwe ndiyo ije nyingine, hapa tumeletewa orodha yenye hoja juu ya hoja kwa vyovyote haipaswi kukubalika bali kuondolewa, “alisema na kuongeza:
“Uamuzi wa kuileta miswada hii kwa hati ya dharura umekiuka kabisa msingi wa mwelekeo wa makubaliano kwenye semina iliyofanyika Juni 30, mwaka huu, wabunge kwa wingi walikataa miswada hiyo isiletwe kwa hati ya dharura na utaratibu huu.” alifafanua na kuongeza:
“Naomba mwongozo wako na naomba usiseme utautoa wakati mwingine, ndiyo mana sikutaka kusema tangu mwanzo, kwa sababu ukisema wakati mwingine huku shughuli zikiendelea kuharibika ni jambo lisilokubalika, tunahitaji majibu sasa, kwanini tuendelee na ‘order paper’ iliyokiuka kanuni na makubaliano ya wabunge.”
Aidha, Spika Anne Makinda, alihamaki na kumtaka Mnyika kufuta kauli zenye kumwamrisha ndipo aweze kutoa mwongozo juu ya jambo hilo.
Baada ya Mbunge huyo kuondoa kauli hiyo, Spika Makinda alisema hakuna mtu yeyote anayeweza kumwamrisha na kwamba kanuni zipo sahihi na zimefuatwa hivyo upinzani wanatumia kanuni kudanganya umma.
Baada ya maelezo hayo, zilizuka kelele na Makinda aliwataka waamue wenyewe huku akisisitiza kuwa hakuna kanuni iliyovunjwa.
Palizuka kelele nyingine huku wengine wakirusha maneno kuwa tokeni nje, lakini wapinzani walisisitiza hakuna wa kutoka, hali iliyosababisha kutokusikikizana na Spika kutangaza kuhairisha Bunge huku wabunge wa upinzani wakiimba hatutaki kuibiwa na kutaka kukutana ukumbi wa Msekwa.
Hata hivyo, walishindwa kutumia ukumbi huo baada ya wabunge wa CCM kukubaliana kukutana ukumbi wa Msekwa na kuwalazimu upinzani kubaki ndani ya ukumbi wa Bunge.
Baada ya wabunge wa CCM na Mawaziri kutoka nje, wabunge wa kambi rasmi ya upinzani kwa umoja wao walibaki ndani ya Bunge na kutoa msimamo wa pamoja baada ya majadiliano ya dakika 20.
Tundu Lissu alisema ndani ya siku sita tangu Juni 27, mwaka huu serikali imeleta miswada 10 yote kwa hati ya dharura, akisema ni kwa ajili ya kuigonga muhuri kwa muundo wa funika kombe wanaharamu wapite.
JAMBOLEO
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali pingamizi nne kati ya nane zilizowasilishwa na kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na nyingine mbili kupinga maazimio ya Bunge kuhusiana na sakata la uchotwaji wa mabilioni ya fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu Tanzania (BoT).
Maamuzi hayo yalitolewa jana na Jaji wa Mahakama hiyo, Gadi Mjemas, akisema anatupilia mbali mapingamizi hayo kwa mujibu wa sheria Ibara ya 100 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayokataza kulipeleka jambo lolote mahakamani linalojadiliwa bungeni.
Jaji Mjemas alifafanua kuwa mihimili miwili, Bunge na Mahakama, haiwezi kuingiliana katika utendaji wake wa majukumu na ndiyo sababu imetupilia mbali pingamizi hizo zilizowasilishwa na IPTL na wapeleka maombi wengine katika kesi hiyo, Harbinder Singh Sethi na Pan Africa Power Solution Ltd (PAP).
Alisema pia kuna pingamizi nyingine nne zilizowekwa na kampuni hizo zilishakataliwa, hakuna sababu ya kuendelea na pingamizi zilizobaki.
Wajibu maombi katika kesi hiyo ya kikatiba Namba 59 ya mwaka 2014, ni Waziri Mkuu, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Spika wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Wapeleka maombi hao walikuwa wakiitaka Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua stahiki za kisheria wote waliotajwa na taarifa maalumu ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)) kuhusika na kashfa ya uchotaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka akaunti ya Tegeta Escrow.
Pia wanadai kuwa kilichofanyika ndani ya Bunge ni kinyume cha Katiba na kina lengo la kugombanisha mihimili mitatu ya dola.
Wanadai Bunge lilijadili suala hilo bila ya kujali kesi zinazoendelea mahakamani.
Licha ya kampuni hizo kutoa pingamizi hizo, Desemba 31 mwaka jana serikali nayo iliwasilisha mapingamizi nane katika mahakama hiyo kupinga maombi ya IPTL juu ya maazimio yaliyopitishwa na Bunge hilo.
HABARILEO
Tanzania imepiga hatua katika mapambano dhidi ya malaria baada ya Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegn kuzindua kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya kuua viluwiluwi vya mbu, jana.
Kiwanda hicho kinachojulikana kama Tanzania Biotech Products Limited kilichopo Kibaha ni cha kwanza Afrika na kitakuwa kikizalisha viuadudu vya viluwiluwi vya mbu katika mazalia yao bila kuleta athari kwa wananchi.
Rais Kikwete katika hotuba yake wakati wa ufunguzi wa kiwanda hicho ambacho ujenzi wake umesimamiwa na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), alisema kiwanda hicho kitaimarisha uwezo wa kukinga na kuzuia maambukizi ya malaria nchini.
Wahenga wamesema daima: “Kinga ni bora kuliko tiba”. Sasa tuna uhakika kuwa mapambano yetu dhidi ya malaria tumeyafikisha mahali pazuri. Nafurahi kuona leo (jana) tunatamka kwa vitendo kuwa “Malaria Haikubaliki,” alisema.
Alisema anajivunia anaondoka madarakani akiwa amehakikisha Watanzania wako mahali salama katika mapambano dhidi ya malaria na kuongeza kuwa nchi imefanikiwa kupunguza maambukizi ya malaria kutoka asilimia 18 mwaka 2007 hadi asilimia 10 mwaka 2012, wakati vifo vinavyotokana na malaria vimepungua kwa asilimia 71.
Rais Kikwete aliieleza NDC kuwa jukumu kubwa lililo mbele sasa ni kuhakikisha kiwanda hicho kinazalisha na kujiendesha kibiashara na kwamba hatarajii kiwanda hicho kujiendesha kwa hasara maana biashara yenyewe ni ya uhakika ndani na nje ya nchi yetu.
Alielekeza Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kukitumia kiwanda hicho katika mipango yake ya kutokomeza malaria katika halmashauri zao kwa kuhamasisha watu na kaya zilizo kwenye maneo yao ya utawala kutumia dawa zinazozalishwa na kiwanda hicho.
Alisema mradi wa kiwanda hicho ni matokeo ya ziara yake nchini Cuba 2009, ambapo alitembelea kiwanda cha Cuba LABIOFAM ambacho kinatumia teknolojia hiyo huharibu mazalia ya mbu.
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Dessalegn akiwa Mwenyekiti wa wa Umoja wa Marais wa Afrika walio katika Mapambano Dhidi ya Malaria (ALMA) aliahidi kufanya kampeni kwa nchi za Afrika kutumia bidhaa kutoka katika kiwanda hicho ili kupambana na malaria katika bara hilo.
“Naamini kiwanda hiki ni muhimu na hatua ya kubwa katika mapambano dhidi ya malaria barani Afrika. Hatua hii itatusaidia kupungua tatizo la malaria mara moja na kwa bara zima,”.
Balozi wa Cuba nchini Jorge Luis Lopez alisema uzinduzi wa kiwanda hicho ni alama ya ushirikiano na urafiki mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili.
Mwenyekiti wa Bodi ya NDC, Dk Chrisant Mzindakaya alisema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha viuadudu wa viluwiluwi vya mbu lita milioni sita kwa mwaka na kuongeza kuwa kiwanda hicho pia kitakuwa kikizalisha aina mbalimbali za mbolea kwa ajili ya matumizi ya ndani na kuuza nje.
HABARILEO
Watia nia wanne waliochukua fomu za kuwania kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa wagombea wa kiti cha urais wametupwa nje ya mchakato huo, baada ya kushindwa kurudisha fomu.
Walioshindwa kurudisha fomu hizo mpaka muda wa mwisho ulipofika saa 10.00 jioni jana ni Peter Nyalali, Helena Elinewinga, Anthony Chalamila na Dk Muzamil Kalokola.
Mmoja wa watia nia hao, Helena mara baada ya kuchukua fomu Juni 25, mwaka huu, alikwenda kumtembelea mmoja wa maofisa wa chama hicho akitafuta ushauri wa namna ya kufanya ili kupata udhamini, lakini baadaye aliamua kutelekeza fomu hizo bila kuondoka nazo.
Jumla ya wanachama 42 walijitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kuomba uteuzi huo ambapo walitakiwa kuwa na wadhamini 450 kutoka mikoa 15, ikiwemo mitatu ya Zanzibar.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Rajab Luhwavi alisema zoezi la kuchukua fomu lilianza Juni 3, mwaka huu na lilitarajia kumalizika Julai 2 saa 10.00 jioni.
Alisema zoezi hilo limefanyika kwa utulivu ambapo kati ya wanachama 42 waliochukua fomu na kutakiwa kuwa na wadhamini kutoka mikoa 15 ikiwemo mitatu ya Zanzibar ambapo kati ya hao ni 38 ndio waliofanikiwa kurejesha fomu.
Alisema hatua itakayofuata ni mchakato wa vikao vya chama kuanzia Jumanne wiki ijayo.
“Mmoja wa wachukua fomu, Helena Elinawinga alitelekeza fomu hizo kwa mmoja wa maofisa wa CCM baada ya kufika kuomba ushauri huku akitaka kupewa kwanza elimu ya siasa kabla ya kuanza kutafuta wadhamini,”Luhwavi.
HABARILEO
Kikongwe Yohana Msumari anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 80, ameuawa kikatili kwa kutenganishwa mwili na kichwa na kisha wauaji hao kukihifadhi kichwa hicho kwenye mfuko wa plastiki chini ya mwembe.
Hata hivyo mtu anayesadikiwa kufanya mauaji hayo, alisakwa na wananchi wenye hasira na kisha kukamatwa na kuonesha mwili wa marehemu huyo na yeye kupigwa na hatimaye kuuawa pia.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea juzi, katika kijiji cha Mamboleo, Kata ya Bwembwera wilayani Muheza mkoani Tanga, ambapo kikongwe huyo aliondoka na kijana ambaye naye hakutambulika jina lake mwenye umri wa kati ya miaka 35-40 wa kabila la Kinyaturu, ambaye alikuwa mfanyakazi za vibarua kwenye mashamba ya watu.
Akisimulia tukio hilo, Katibu Kata wa Chama Cha Mapinduzi kwenye Kata ya Bwembwera, Achi Semhando alisema tukio hilo la kusikitisha lilitokea kwenye kata yao na kwamba polisi walifika baada ya kupewa taarifa hizo na kuchukia maiti.
“Kwa kweli ni tukio la kusikitisha, huyu mzee aliondoka na huyo kijana na kwenda kumuonesha sehemu ya kufyeka shambani kwake, ila hadi jioni huyu mzee hakurudi na ndipo wananchi waliingiwa na wasiwasi na kuamua kumtafuta huyo kijana aliyeondoka naye,” Semhando.
Kijana huyo alipatikana na wananchi walimtaka aseme mzee huyo alipo na ndipo aliwapeleka hadi shambani na kuona maiti ya mzee huyo na ndipo walianza kumpiga hadi umauti wake na kisha kutoa taarifa polisi.
Hata hivyo maiti ya mzee huyo haikuwa na kichwa na polisi walizichukua maiti zote mbili na kwamba ilipofika jana asubuhi, watoto waliokuwa wakiokota maembe kwenye miti waliona mfuko umefungwa na walipouchunguza waliona kichwa na kutoa taarifa kijijini.
HABARILEO
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana imeshindwa kumsomea maelezo ya awali Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima na wenzake wanaokabiliwa na kesi ya kutumia lugha ya matusi na kushindwa kuhifadhi silaha.
Kesi hiyo ilitajwa jana kwa ajili ya washitakiwa kusomewa maelezo ya awali lakini iliahirishwa kwa kuwa Hakimu Mkazi Wilfred Dyansobera anayesikiliza kesi hiyo hakuwepo mahakamani.
Hakimu Mkazi, Thomas Simba aliahirisha kesi hiyo hiyo Julai 20, mwaka huu kwa ajili ya washitakiwa hao kusomewa maelezo ya awali mbele ya Hakimu Dyansobera.
Mbali na Gwajima washitakiwa wengine, ni Mlinzi wake, George Mzava, Msaidizi wake, Yekonia Bihagaze na Mchungaji Georgey Milulu wanakabiliwa na shitaka la kukutwa na silaha pamoja na risasi kinyume cha sheria.
Katika kesi ya kwanza namba 85, Gwajima anadaiwa kati ya Machi16 na 25, mwaka huu katika Viwanja vya Tanganyika Packers Wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam alitoa lugha ya matusi dhidi ya Askofu wa Kanisa Katoliki Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo akimueleza Askofu kwamba ni mtoto, mpuuzi asiye na akili katika namna ya kwamba ingeleta uvunjifu wa amani.
Katika kesi nyingine namba 84 , Gwajima anakabiliwa na mashitaka ya kushindwa kuhifadhi silaha na risasi jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya uhifadhi wa silaha za moto.
Anadaiwa kati ya Machi 27 na 29, mwaka huu, ndani ya Jiji na Mkoa wa Dar es Salaam, alishindwa kuhifadhi silaha aina ya Beretta namba CAT 5802, risasi 3 za pisto na risasi 17 za shotgun.
Katika mashitaka mengine yanayowakabili washitakiwa wengine, inadaiwa Machi 29, mwaka huu katika Hospitali ya TMJ Mikocheni ‘A’ walikutwa wakimiliki silaha na risasi hizo bila ruhusa kutoka mamlaka husika.
MTANZANIA
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambayo iliahirisha uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR) katika Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani hivi karibuni, sasa imesema utafanyika kuanzia Julai 7 hadi 20 kwa Mkoa wa Pwani na Julai 16 hadi Julai 25 kwa Jiji la Dar es Salaam.
Uboreshaji wa daftari hilo kwa Jiji la Dar es salaam na Mkoa wa Pwani uliahirishwa kutokana na kuchelewa kwa vifaa vya uboreshaji kutoka mikoani ambavyo vilipelekwa ili kuongeza ufanisi kutokana na maeneo hayo kuwa na idadi kubwa ya watu wenye sifa ya kuandikishwa kuwa wapiga kura.
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Julius Mallaba aliwataka wananchi wote wa mikoa hiyo kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vya uandikishaji vitakavyokuwa kwenye vijiji, vitongoji na mitaa ili kujiandikisha waweze kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka katika Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba mwaka huu.
Aliwataja watakaohusika na zoezi hilo kuwa ni watu wote waliotimiza umri wa miaka 18 na kuendelea na wale watakaotimiza miaka 18 ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu.
Wengine ni waliojiandikisha awali kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la zamani ili kuhuisha taarifa zao na kupata kadi mpya za kupigia kura.
Aidha Mallaba aliwataja wengine wenye sifa ya kujiandikisha kuwa ni wale wote wenye sifa za kujiandikisha lakini hawajawahi kujiandikisha kwenye daftari hilo.
Alisema wale wote wenye kadi za kupigia kura za zamani wanatakiwa kwenda na kadi zao ili kurahisisha uchukuaji wa taarifa zao na kadi hizo zitarudishwa NEC na watapata vitambulisho vipya.
Wananchi wanatakiwa kujiandikisha katika vituo vilivyopo ndani ya kata zao ili kuweza kupata fursa ya kumchagua diwani, mbunge na rais.
MWANANCHI
Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, January Makamba amesema kuwa ana imani vikao vya kuwachuja wagombea wa urais vitafanya uamuzi kwa msingi wa kujiamini na siyo kwa hofu.
Makamba alisema hayo mjini Dodoma jana baada ya kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa na CCM kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
“Kama chama tumepata nafasi ya kupitia michakato mingi migumu kuliko hata huu, tumefanya uamuzi katika mambo mengi na makubwa na bado tumeendelea kubaki kuwa wamoja. Nina imani hata katika hili pia tutavuka salama,” Makamba.
Alisema wananchi wengi hasa vijana wanaangalia CCM itamteua mgombea wa aina gani na wanataka aina mpya ya uongozi ambao unaangalia mbele na unaoakisi matarajio yao.
Makamba alisema wana-CCM, kama walivyo wananchi wote, wanachukizwa na rushwa na matumizi mabaya ya madaraka na wanachukizwa na chama chao kuhusishwa na masuala hayo.
Alisema CCM wanataka wagombea kwa nafasi za ngazi zote ambao wana mvuto kwa watu na ambao itakuwa rahisi kuwanadi bila kuwatolea maelezo au utetezi kwanza.
Alisema katika kuomba nafasi hiyo ni vyema kutosahau kwamba bado yupo Rais ambaye amefanya kazi nzuri na anaendelea kuifanya iwe nzuri zaidi.
“Tusizungumze kana kwamba hakuna kilichofanyika. Yeyote atakayepata heshima ya kuliongoza Taifa letu ataanzia alipoishia Rais Jakaya Kikwete,” alisisitiza.
Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, alisema nafasi ya urais ni ya hadhi, heshima na dhamana kubwa hivyo ni muhimu kujitafakari kwa kina kabla ya kuiomba.
Lakini pia ni muhimu kuiomba kwa staha, unyenyekevu na hekima na kwa namna inayoendana na hadhi, heshima na dhamana ya nafasi yenyewe.
Unahitaji chochote nachokipata kikufikie? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.