Katibu Mkuu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, alisema Magufuli hawezi kushindana na Ukawa, kwani kwenye jimbo lake la Chato chama hicho kimechukua sehemu kubwa ya uongozi kuanzia ngazi ya mitaa na kata.
Dk. Slaa alisema ikiwa kwenye jimbo lake mwenyewe Ukawa wamempita kwa nafasi hizo, hatakuwa na uwezo wa kushindana nao katika nafasi hiyo ya juu kabisa nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba, alipongeza mchakato wa mchujo uliofanywa na CCM katika kumpata mgombea.
Hata hivyo alisema Magufuli anahitaji msaada wa kidiplomasia kwani utendaji wa mtu akiwa Waziri ni tofauti na wakati akiwa Rais.
“Walikuwa na mchakato mgumu kidogo hasa walipofikia kundi la watano, napongeza walipofikia. Huyo mgombea waliyempata, Watanzania wanamfahamu, ni mchapakazi…lakini utendaji wa mtu akiwa Waziri ni tofauti na akiwa Rais…anahitaji msaada wa kidiplomasia,” Dk. Bisimba.
Mhadhiri mwandamizi wa Idara ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema CCM hawajafanya makosa kumteua Magufuli kuwapeperushia bendera kwani ni mtu ambaye hajitambulishi kimakundi huku akijipatia umaarufu katika utendaji na uchapaji wake wa kazi katika wizara ikiwamo ya Ujenzi.
Alisema, Magufuli ni mtu ambaye anafaa kukiwakilisha CCM kupambana na vyama vya upinzani kwani akiwa Waziri, wizara yake haina historia yoyote ya kashfa katika taarifa za Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salim, aliipongeza CCM kwa kufanikiwa kuvunja makundi yaliyokuwa yametawala kabla ya kupatikana kwa mgombea huyo.
Alisema CCM kumpitisha Dk. Magufuli kumevunja makundi yote yaliyokuwamo, jambo ambalo halikutarajiwa.
NIPASHE
Balozi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (AU) katika Umoja wa Mataifa (UN), Amina Salum Ali na Waziri wa Katiba na sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, wameahidi kumuunga mkono Dk. John Magufuli katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Balozi Amina ameandika historia mpya kisiasa, baada ya kumtangulia kwa kura, Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa (UN), Dk. Asha Rose Migiro.
Mwanadiplomasia huyo kutoka Zanzibar ambaye alipata kura 253 (asilimia 10.5) ya kura zote 2,422 zilizopigwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), amekishukuru chama chake, kwa kumuamini na kumpigia kura zilizompaisha kisiasa na kuangukia nafasi ya pili.
“Niko tayari kumuunga mkono mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli ambaye wajumbe wa Mkutano Mkuu wamemwamini na kumpigia kura za kishindo. Makundi yamekwisha na mie yangu nimeyapeleka kwake ili kukisaidia chama changu kushinda kwa kishindo,” Balozi Amina.
Naye Dk. Migiro ambaye alifanikiwa kupenya kuwamo katika kundi la tatu bora alisema: “Nilipopata taarifa za awali za matokeo, nilimpigia simu Dk. Magufuli. Kwa niaba ya familia yangu kwa sababu unajua mume wangu ni mwalimu wa Magufuli.”
“Niwaombe wagombea wenzangu 42, tuliochukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwania kiti hiki, tuvunje makundi na kumsaidia mwenzetu aliyeshinda katika mchakato ndani ya CCM akibebe chama chetu katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, dhidi ya vyama vya upinzania.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano), Samia Hassan Suluhu, ambaye ndiye mgombea Mwenza wa Dk. Magufuli, amekishukuru Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwapa fursa wanawake.
“Wanawake, tumepewa heshima kubwa, hatuna sababu ya kukaa nyuma, naombeni mnifuate kwa sababu nimewafungulia njia nafasi za juu za madaraka.”
NIPASHE
Halmashauri ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara, imeombwa kupeleka walimu katika Shule ya Msingi Nambaza baada ya baadhi ya walimu kudai kufanyiwa vitendo vya kishirikina kwa kuingiliwa kimwili nyakati za usiku na hivyo kusababisha kuikimbia shule hiyo.
Wakifunga kikao cha mwisho cha madiwani wa halmashauri hiyo mjini Bunda, baadhi ya madiwani akiwamo wa kata ya Nansimo, Sabatho Mafwimbo, alisema kutokana na walimu wawili wa Shule ya Msingi Nambaza kufanyiwa vitendo hivyo vya ushirikina, hivi sasa shule hiyo imepwaya walimu baada ya baadhi yao kukimbia.
“Mkurugenzi, tunaomba halmashauri yako ituletee walimu katika shule hiyo ili zitakapofunguliwa wanafunzi wafundishwe kuziba pengo la wale walioamua kukimbia,” Mafwimbo.
Alisema hivi karibuni walimu wawili wa kike wa shule hiyo, waliingiliwa ndani ya nyumba zao kwa njia zinazoadaiwa za kishirikina na kuwaingilia kimwili bila wenyewe kujitambua hali iliyowafedhehesha walimu hao.
Kufuatia tukio hilo, mwananchi mmoja aliuawa na wananchi wenye hasira kijijini hapo baada ya kutuhumiwa kuwa miongoni mwa ‘wachawi’ waliotenda ushirikina huo huku wengine saba wakazi wa kijiji hicho wakikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa makosa mawili ya kupanga, kutenda kosa la ushirikina na kuwaingilia kimwili walimu hao.
Mwenyekiti wa Halmashauri, Joseph Marimbe, aliwataka wananchi wa kijiji hicho kuachana na vitendo vya ushirikina kwa sababu hali hiyo inasababisha walimu kuogopa kufundisha shule hiyo.
MWANANCHI
Saa chache baada ya Dk John Magufuli kutangazwa kuwa mteule wa CCM kuwania urais, ulinzi umeimarishwa kwa mgombea mwenyewe, nyumbani kwake eneo la Ada Estate, Dar es Salaam na jimboni Chato mkoani Geita.
Muda mfupi baada ya kuwapo taarifa kuwa Magufuli anaongoza kura za wajumbe wa Mkutano Mkuu, aliongezewa ulinzi usiku huo na hadi jana muda wote, alionekana akiwa na walinzi watano.
Jimboni Chato, nyumbani kwake eneo la Rubambambangwe, polisi walionekana wakitanda tangu jana asubuhi tofauti na siku nyingine.
Askari hao wakiongozwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Chato, Alex Mkama walionekana nyumbani hapo tangu asubuhi hata kabla matokeo yaliyompa ushindi Dk Magufuli hayajatangazwa.
Mwandishi wa habari hizi ambaye alikwenda nyumbani kwa Dk Magufuli kuzungumza familia yake, hakuruhusiwa na polisi waliokuwa kwenye lango kuu la kuingilia, walidai wamepewa maelekezo ya kutoruhusu watu kuingia.
“Naomba usiingie ndani wala kupiga picha eneo hili, hayo ndiyo maelekezo ninayokupa na niliyopewa, vinginevyo mtafute RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa) akupe ruhusa,” alisema mmoja wa askari hao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo alisema polisi walikuwa wanatekeleza jukumu lao kwa umma la kulinda raia na mali zao kutokana na wananchi kwa makundi kusherehekea ushindi wa mteule huyo.
Konyo alisema ulinzi huo ulilenga kuweka na kuimarisha usalama kwenye makazi ya familia hiyo.
Hata hivyo, Konyo alipotakiwa kuzungumzia kuzuia watu kupiga picha kwenye makazi hayo alikata simu na hata alipopigiwa tena hakupokea.
Nyumbani kwake, Ada Estate, ulinzi ulianza kuimarishwa mara tu baada ya kiongozi huyo kutangazwa kuwa mgombea wa urais kupitia CCM.
Mmoja wa walinzi hao ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema wameongezwa walinzi wengine wanne mara baada ya matokeo ya mjini Dodoma kutangazwa.
Magari kadhaa yenye namba za serikali na magari ya polisi yalionekana yakiingia na kutoka nyumbani kwa Magufuli.
MWANANCHI
Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Pombe Magufuli ameelezewa na watu mbalimbali kuwa ni mchapakazi, makini, asiyependa uvivu, lakini Rais Jakaya Kikwete amehitimisha yote kwa kumpachika jina la “tingatinga”.
Rais Kikwete alisema hayo baada ya Magufuli kutangazwa kuwashinda makada wengine wawili waliopigiwa kura na Mkutano Mkuu wa CCM baada ya kuzoa kura 2,104, sawa na asilimia 87.08, ushindi ambao alisema unaakisi kumalizika kwa makundi yaliyoibuka kwenye mbio za kuwania kuteuliwa na CCM kugombea urais wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Balozi Amina Salum Ali alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 253 (sawa na asilimia 10.4), wakati Dk Asha Rose Migiro alikuwa wa mwisho kwa kupata kura 59 (asilimia 2.4). Jumla ya kura zilizopigwa kwenye mkutano huo mkuu zilikuwa 2,422 na kura sita tu ndio ziliharibika.
“Kila mtu anaitwa jembe,” alisema Rais Kikwete alipokuwa akianza kutaja sifa za Magufuli ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na pia Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
“Lakini huyu ni zaidi ya jembe. Ni tingatinga… Magufuli ni bulldozer. Magufuli havumili ujinga, ni mtu ambaye anataka kuona kazi zake zinafanyika kama alivyoagiza.”
Kikwete aliendelea kummwagia sifa Dk Magufuli kuhusu utendaji wake akisema kuwa alipokuwa akifuatilia wakandarasi kwenye miradi ya ujenzi, alidiriki kuwatimua pale alipobaini walikuwa wakifanya kazi kinyume na makubaliano.
“Tunaamini kuwa utawaongoza Watanzania vizuri,” alisema Kikwete akimgeukia mbunge huyo wa Chato.
“Tulikuwa na wagombea 338 lakini sasa tunaye mmoja na tuna kundi moja tu la CCM. Timu Magufuli imeshaondoka. Wengi walidhani CCM itafia hapa, lakini ushindi huu ni ishara kuwa CCM ni moja.
“Tunatakiwa kuacha kuteuwa watu kwa urafiki na kujuana ili tushinde kwa sababu imani huzaa imani. Sina shaka kuwa tutashinda lakini ushindi hauji hivi hivi lazima tuwe na mikakati mizuri, mipango thabiti na utekelezaji makini,” alisema.
Rais Kikwete ni mmoja kati ya watu wengi waliohojiwa na Mwananchi kuhusu mteule huyo wa CCM, ambaye hakuwa akitajwa kama kinara kwenye mbio za urais kabla ya kufikia hatua hiyo ya kujadiliwa na vikao vya juu.
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Mussa Iyombe, aliyefanya kazi na Dk Magufuli kwa zaidi ya miaka 10, alisema iwapo atachaguliwa kuwa rais basi wavivu wajitayarishe kukimbia kwani Waziri huyo ni mchapa kazi wa hali ya juu.
MWANANCHI
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Dk Emmanuel Nchimbi ambaye pia alikuwa mwanamkakati katika kambi ya Edward Lowassa katika mbio za urais, amesema kambi yake inamuunga mkono mgombea urais aliyeteuliwa na chama kwa sababu anauzika.
Dk Nchimbi akizungumza na gazeti hili jana alisema Dk John Magufuli ni mgombea anayeuzika tofauti na wengine na kwamba kambi yao inamuunga mkono katika kukiwezesha chama kuendelea kushika dola.
Alisema linapofika suala la maslahi ya chama wote wanakuwa kitu kimoja na kwamba uwezo na utendaji wa Dk Magufuli ni wa hali ya juu, kiasi kwamba ni rahisi kumnadi kwa wananchi.
Dk Nchimbi ambaye baada ya Kamati Kuu kutangaza majina matano ya wanaowania kuteuliwa, yeye na wajumbe wenzake wawili wa Kamati Kuu, Sophia Simba na Adam Kimbisa walitoka hadharani wakisema wanajitenga na maamuzi ya kamati hiyo kwa kuwa imekiuka katiba ya CCM.
Alisema baada ya vikao vya CCM kumpitisha Dk Magufuli, kambi yao imeamua kumuunga mkono kwakuwa ni mtendaji mzuri wa kazi anazopewa na mifano ipo mingi katika wizara alizoziongoza.
Dk Nchimbi alitoa mifano ya utendaji wa Dk Magufuli kwa kuwa ameweza kujenga barabara, kukamata meli za kigeni zinazovua kwa njia haramu katika bahari ya Tanzania na kupambana na ujenzi usiofuata sheria hasa kwenye maeneo ya barabara.
MWANANCHI
Wananchi wa kitongoji cha Bomani wamemkamata kijana mwenye miaka 28 anayedaiwa kukutwa akimnajisi bata.
Shuhuda wa tukio hilo Sacina Nangere alisema akiwa na wenzake walisikia kelele za bata nyuma ya nyumba kwa muda mrefu na kuamua kukimbia kuangalia kuna nini, na alipofika alimkuta mtuhumiwa huyo akifanya kitendo hicho.
“Nilirudi kukimbia kumwita mama akaone na alipofika huyo jamaa alimtupa bata na kukimbilia kwa jirani alikokua amefikia”.
Mmiliki wa bata huyo Susana alisema akiwa jikoni akiandaa chakula mtoto wake alimwita na kumwambia akaone mgeni wa jirani yake anachomfanyia bata wao.
“Sikuamini macho yangu hadi anamtupa bata na kuondoka, tulipiga yowe na wananchi wakanisaidia kumkamata wakati akijaribu kutoroka”.
Balozi wa nyumba 1o alisema mama huyo alifika nyumbani kwake akiwa na bata aliyenajisiwa huku akiomba msaada na alipoangaliwa alikutwa kweli ameharibiwa na kijana huyo.
Kamanda wa Polisi Bukombe George Kyando alithibitisha kukamatwa kwa kijana huyo na kwamba baada ya uchunguzi wa vipimo vya akili vimeonyesha ana akili timamu na taratibu zinafanyika kumfikisha mahakamani.
JAMBOLEO
Akihutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma jana baada ya kupitishwa na CCM kuwania urais, Dk. Magufuli alitangaza vita ya kupambana na wazembe, mafisadi, wala rushwa na wabadhirifu kuwa atapambana nao kwa nguvu zake zote.
Unahitaji chochote nachokipata kikufikie? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook naInstagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.