Nahodha wa Manchester United Wayne Rooney anatarajia kukabidhiwa mikoba ya kuongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kwa msimu ujao wa mwaka 2015/2016 ambapo atachezeshwa kama mshambuliaji wa kati nafasi ambayo kwa muda mrefu mchezaji huyu amekuwa akiitazama kama nafasi yake ya asili .
Rooney kwa muda mrefu amejikuta akiwa mhanga wa uwezo wake mwenyewe ambapo amekuwa akichezeshwa kwenye nafasi mbalimbali tofauti na nafasi ya mshambuliaji wa kati jambo ambalo amekuwa akilifanya kwa ufasaha bila kinyongo na ubinafsi.
Msimu uliopita Rooney alitumia karibu nusu ya msimu kwenye nafasi ya kiungo mkabaji na miaka ya nyuma kwa nyakati tofauti amekuwa akichezeshwa kama mshambuliaji wa pili au kiungo mshambuliaji wa pembeni .
Mara ya mwisho Rooney kuchezeshwa kama mshambuliaji wa kati ilikuwa msimu wa mwaka 2010/2011 na mshambuliaji huyu alifunga mabao 30 ukiwa msimu wake wa mwisho kuongoza kwa ufungaji wa mabao.
Kuelekea msimu ujao tayari United imewaruhusu Radamel Falcao na Robin Van Persie kuondoka hali inayoashiria kubaki kwa pengo kwenye nafasi hiyo na kwa mujibu wa ripoti za ndani kocha Louis Van Gaal ameahii kumpa Rooney nafasi hiyo .
Bado inaaminika kuwa United itasajili mshambuliaji kabla ya dirisha la usajili kufungwa na mpaka sasa kwa hali inavyokwenda United italazimika kuwategemea Wayne Rooney , Javier Hernandez Chicharito na kinda James Wilson mwenye umri wa miaka 19.