MWANANCHI
Binti wa Waziri mkuu wa zamani, Edward Sokoine ambaye anaitwa Namelock Sokoine ameshinda kura za maoni kugombea ubunge Jimbo la Monduli kupitia CCM huku mkwe wa Lowassa, Siyoi Sumari akishindwa Jimbo la Arumeru Mashariki.
Namelock ambaye ni mbunge wa Viti Maalumu CCM alipata kura 29,582 akifuatiliwa na Loota Sanare aliyepata kura 8,809 na nafasi ya tatu, ilichukuliwa na Lolinyu Mkoosu aliyepata kura 235 na Payani Leyani akipata kura 226.
MWANANCHI
Wadau wawili wa michezo na burudani Tanzania Yusuf Manji na Said Fella wameibuka kidedea katika kinyang’anyiro cha udiwani katika jimbo jipya la Mbagala jijini hapa.
Manji ambaye ni Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Quality Group, alishinda katika Udiwani katika Kata ya Mbagala Kuu wakati Fella ambaye ni msimamizi wa kazi za wasanii na muasisi wa Kundi la Mkubwa na Wanawe, akishinda katika Kata ya Kilungure.
Fella ni Meneja wa mwanamuziki maarufu nchini, Diamond Platnumz, TMK Family na Yamoto Band.
Kaimu Katibu CCM Wilaya ya Temeke, Rutami Masunu alisema uchaguzi huo ulikwenda vizuri katika maeneo mengi isipokuwa kulitokea changamoto kidogo katika kata moja ambayo itafanya uchaguzi leo.
MWANANCHI
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amezungumzia kukosekana kwa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Willibrod Slaa katika vikao vya chama hicho vinavyoendelea, >>> “Nitazungumzia suala hilo muda muafaka ukifika… Siwezi kusema zaidi ya hapo”- hilo ndio jibu lake alipoulizwa.
Kauli hiyo ya Mbowe haikuondoa wingu zito lililotanda CHADEMA baada ya kutoonekana hadharani kwa kiongozi huyo katika matukio manne muhimu ya chama hicho kikuu cha upinzani, tangu Waziri Mkuu Wa Zamani, Edward Lowassa ajiunge nacho.
Naibu Katibu Mkuu (Bara), John Mnyika alionekana jana kwa mara ya kwanza katika kikao hicho na kufuta uvumi uliokuwa umesambaa kuwa alikuwa na mpango wa kuachana na CHADEMA kama inavyodaiwa kwa Dk Slaa.
Viongozi hao walianza kutoonekana katika shughuli za chama tangu Lowassa alipojiunga na Chadema Julai 28 na kukabidhiwa fomu ya kugombea Urais Julai.
“Suala la kutokuwapo Dk Slaa ni kitu cha kawaida, anafanya kazi nyingine huko, lakini pia kuna wasaidizi wake hapa ambao ni sisi manaibu. Mlikuwa mnazungumzia Mnyika naye haonekani, si huyo. Hatuwezi kuendelea kujibu ‘rumors’ (uzushi) wa kwenye mitandao… nyie subirini si tupo mtaona kama yupo au la”– Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu.
Mbunge Mnyika alionekana katika viwanja vya hoteli hiyo lakini alikataa kuongelea chochote >>>“Siwezi kuzungumza chochote”—Mnyika.
NIPASHE
Wagombea wawili wa kiti cha Ubunge katika Jimbo la Moshi Mjini kwa tiketi ya CCM, ‘wamegoma’ kusaini matokeo ya kura za maoni yaliyompa ushindi mfanyabiashara maarufu wa Dar es Salaam, Davis Mosha.
Waliogoma kusaini matokeo hayo ni Buni Ramole na Patrick Boisafi, ambao walikuwa washindani wakuu wa Mosha kati ya wagombea 12 waliojitokeza kuomba kuteuliwa na CCM kugombea Ubunge Jimbo la Moshi Mjini.
Katibu wa CCM Moshi Mjini, Loth Ole Nessele amesema Buni alikataa kusaini matokeo hayo akidai amepata `presha’ kutokana na mchakato huo wakati Boisafi alimweleza kwamba hawezi kusaini kwa sababu yupo nyumbani peke yake na amechoka kutokana na mchakato huo.
“Ni kweli nimekataa kusaini matokeo na tayari nimewaandikia na kuwakabidhi CCM barua nikiwaeleza kuhusu uamuzi wangu. Rushwa za wazi wazi na upendeleo kwa mgombea mmoja ni hatari na wala CCM isifikiri kwa mwendo huu italikomboa Jimbo la Moshi Mjini”– Buni Ramole.
NIPASHE
Baadhi ya Vigogo wakiwamo Mawaziri, Wabunge wameangushwa katika Kura za Maoni za kutafuta wagombea Ubunge kupitia CCM.
Miongoni mwa waliangushwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe.
Wamo pia Manaibu Mawaziri wa Mambo Ya Ndani ya Nchi Na Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, mawaziri wa zamani, Mkuu wa Mkoa na wabunge.
Kwa upande wa Zanzibar, Wabunge na wawakilishi wa CCM wanaotetea tena nafasi hizo wengi wamejikuta wakianguka.
Wabunge na wawakilishi hao waliotupwa katika kura hizo yumo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim, aliekuwa akigombea Ubunge jimbo la Paje wilaya ya Kusini Unguja.