MWANANCHI
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeonya kwamba mtu yoyote haruhusiwi kutoa kadi yake ya kupigakura au taarifa za kadi hiyo kwa ndugu, jamaa au mwajiri wake.
NEC imetoa onyo hilo wakati tayari kukiwa na tetesi kuwa baadhi ya wafanyakazi wa umma wakiwamo polisi, wanajeshi na askari magereza wametakiwa kukabidhi kadi zao kwa viongozi wao wa ngazi za juu.
Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara, John Mnyika jana aliitisha mkutano wa Vyombo vya Habari akidai kuna tetesi Serikali imeviagiza vyombo vya usalama, kupeleka namba za vitambulisho vya askari wote kwa wakuu wa vitengo jambo ambalo ni kunyume na utaratibu
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Kailima Kombwey amesema kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ambayo inazungumzia Daftari la Kudumu la Wapigakura, hairuhusiwi na haitakiwi kwa mtu asiyehusika na kadi ya mpigakura kuimiliki kadi hiyo.
Msemaji wa JWTZ, Kanali Ngemela Lubinga alisema taarifa hizo ni za uongo na hazina ukweli wowote kuwa wanajeshi wameombwa nambari za vitambulisho na Msemaji wa Polisi, Advera Bulimba alipopigiwa simu kuhusu madai hayo, alisema hana hizo taarifa, huku Ofisa Mawasiliano wa Magereza, Deodatus Kazinja alisema hizo ni tetesi na wala hazina ukweli wowote.
NIPASHE
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT), Sophia Simba amesema hana mpango wa kukihama chama hicho.
Kauli hiyo ametoa baada ya kuwepo kwa tetesi zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa ana mpango wa kukihama chama na kumfuata Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa.
“Mimi ni mwanachama wa CCM na pia ni mwenyekiti wa UWT, hivyo sina mpango wowote wa kukihama chama changu na kile kinachozungumzwa ni uzushi”– Sophia Simba.
Sophia Simba amesema amejipanga kuongoza timu ya wanawake wenzake ili kuhakikisha wanampeleka Dk. John Magufuli Ikulu.
NIPASHE
Serikali imesema matukio ya uporaji wa silaha na matukio ya mauaji ya askari wa Jeshi la Polisi nchini ya hivi karibuni, yanachangiwa na ulevi, uzembe katika doria pamoja na kukaribisha watu wasiowajua.
“Askari wetu wakati mwingine wanaonekana hawako makini katika utendaji wao wa kazi, lakini matukio ya uporaji wa silaha na mauaji ya askari yaliyotokea katika vituo vya Ushirombo, Stakishari, Mkuranga Mbagala na kwingineko ambako sijakutaja; ulevi na uzembe katika doria ni miongoni mwa mambo yanayoonekana kuchangia,” alisema Naibu waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Ame Silima.
Jambo LEO
Mbunge Andrew Chenge jana alilumbana na wakili wa Serikali kuhusu vifungu vya sheria wakati wakipitia tuhuma zake za kujipatia mgawo wa sh. bilioni 1.6 zilizotoka kwenye Akaunti ya Tegeta ESCROW.
Mbunge huyo amesema msimamo wake ni kwamba hakuna muingiliano wowote wa maslahi kama baraza linavyodai, kwani alipewa fedha kwa kazi aliyofanya.
Chenge ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Serikali ya Rais Benjamin Mkapa, alidai kuwa fedha hizo zinatokana na malipo ya awali kulingana na msaada wa kisheria alioutoa kwa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing ambapo kuliamka malumbano makali ya kisheria kati yake na mawakili wa baraza hilo, hali iliyosababisha baraza kuahirisha suala hilo.
Kwa mujibu Jaji Msumi shauri hilo linaahirishwa kusikilizwa hadi mlalamikiwa atakapowasilisha majibu dhidi ya hati ya malalamiko aliyopata kutoka baraza hilo.
Akijibu swali la wakili wa baraza hilo, Hassani Mayunga lililomtaka kueleza kama aliingiza taarifa za malipo yake kutoka VIP, Chenge alidai hakuona haja ya kuingiza kwenye matamko yake, kwani haikuwa sehemu ya malipo ya mkataba wake.
Alipoulizwa wakati Kampuni ya IPTL inaingia mkataba na Shirika la Umeme Tanzania TANESCO alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni kwa namna gani aliishauri, Chenge alidai kuwa yeye kama yeye hakushauri bali ofisi ya mwanasheria ndiyo iliyoshauri.
“Mimi sikuishauri Serikali bali ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kwani ni taasisi na ina jukumu la kuishauri Serikali si mimi kama Chenge”—Mbunge Andrew Chenge.
MWANANCHI
Mgombea Urais kupitia tiketi ya Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) Chifu Lutalosa Yemba, amemkaribisha aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kujiunga na chama hicho.
Yemba alisema anaufahamu uwezo wa Lipumba katika siasa, ujasiri na uvumilivu wake, hivyo hatakuwa na kinyongo kufanya naye kazi ya kusukuma mbele gurudumu la siasa za upinzani.
“Walinifukuza mwezi wa sita, mwezi wa nane Lipumba amejing’atua kwenye uongozi, watafahamu sasa kuwa kwenye chama kile kuna udhalimu, namkaribisha Lipumba na ninampongeza kwa uvumilivu wake, ingawa ninaumia kuona kiongozi shupavu aliyekuwa na uwezo wa kuhakikisha wananchi wanaamini katika vyama vingine vya upinzani kukatishwa tamaa na watu wachache wenye uroho wa madaraka”– alisema Chief Yemba.
“Mchagueni asiyekuwa mwizi, fisadi, mnyang’anyi asiye na kashfa na hakuna unapoweza kumpata kiongozi wa namna hiyo zaidi ya ADC, pimeni sikilizeni sera zetu, ilani yetu mtuunge mkono”– Chief Yemba.
PAPO KWA PAPO zipate habari zote zinazonifikia za siasa muziki, michezo, maisha, Breaking news na nyingine kwa kujiunga hapa na mimi >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos