Sakata la hatma ya golikipa wa kimataifa wa Hispania David De Gea ndani ya klabu ya Manchester United linazidi kuchukua sura mpya.
De Gea ambaye amekuwa akihusishwa na kutaka kujiunga na Real Madrid, alianza kwa kupigwa benchi kwa mechi mbili za ufunguzi na kocha Louis Van Gaal na taarifa mbalimbali kutoka kwenye vyombo vya habari vya Uingereza zinasema mchezaji huyo aliamuariwa na Van Gaal kufanya mazoezi na timu ya ‘reserves’ na pia alikatazwa kusafiri na United iliyoenda Birmingham kucheza na Aston Villa.
David de Gea alifanya mazoezi na timu ya wachezaji wa akiba na kuambiwa kwamba hatokuwa kwenye msafara wa timu ulioenda kupambana na Villa usiku wa leo.
Sergio Romero aliendelea kukaa langoni mwa United usiku wa leo katika mechi ya ushindi vs Aston Villa.
Siku ya Alhamisi, kocha wa United Van Gaal alikaririwa akisema kwamba De Gea alimwambia kocha wa makipa wa United Frans Hoel Kwamba hataki kucheza mpaka hatma yake itakapojulikana ndani ya klabu hiyo.